The House of Favourite Newspapers

KIJANA ADAIWA KUUAWA NA POLISI

BUKOBA: Mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Salehe Ally Mujaheji (pichani) anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi mara baada ya kutoroka katika Kituo cha Kayanga, wilayani Karagwe mkoani Kagera.

 

TUJIUNGE NA CHANZO

Kwa mujibu wa chanzo, marehemu Salehe alifikishwa kituoni hapo baada ya kukorofishana na rafiki yake ambapo baada ya kufikishwa kituoni alitakiwa kufanyia ukaguzi ndipo akatoroka.

 

“Aliamriwa kuvua mkanda na viatu ili kuwekwa sero, kitu ambacho kilimshtua marehemu na kuamua kukimbia kutoka hapo kituoni kuelekea ilipo mahakama ya mwanzo mjini Kayanga. “Nyuma yake akiwa anafukuzwa na askari asiyekuwa na silaha, marehemu alipishana na askari wengine wawili waliokuwa wamebeba silaha wakiwa doria, ndipo askari mmoja alikoki bunduki na kumpiga risasi moja mguuni na nyingine kiuno,” kilisema chanzo.

 

NDUGU ANENA

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mjomba wa marehemu aliyefahamika kwa jina moja la Thomas alisimulia kuwa, awali aliletewa malalamiko kuwa marehemu amemkashifu rafiki yake, hivyo kama mjomba mtu achukue hatua, lakini mjomba huyo akachukulia kawaida na kumtaka mlalamikaji (rafiki wa marehemu) wakayamalize wao kama vijana.

 

“Baada ya hapo sikujua nini kimeendelea, kumbe mlalamikaji hakuridhishwa na majibu yangu, hivyo akaamua kwenda Kituo cha Polisi cha Kayanga kufungua mashitaka,” alisema mjomba huyo. Thomas anaendelea kusimulia kuwa, ilipofika jioni wakati anatoka kufanya mazoezi, alipigiwa simu nyingi pamoja na meseji zilizokuwa zikielezea Salehe kupigwa risasi na kufariki dunia.

 

“Nilimuomba rafiki yangu, Charles Mitumba anipeleke Kayanga kituoni, kufika pale nikawakuta askari lakini hawakunipa ushirikiano zaidi ya kuniambia yupo Hospitali ya Nyakahanga. “Kitendo cha kufika hospitali nikashuhudia kweli mdogo wangu Salehe amefariki na yupo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti,” anamaliza kusimulia mjomba huyo.

KAMANDA ANASEMAJE?

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, SACP Augustino Olomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa siku ya tukio marehemu alifikishwa na mwenzake kituoni kwa kosa la kumdhuru mwili. “Walikuwa kwenye starehe na marehemu (Salehe) alikuwa amemdhuru mwenzake hivyo akaenda kumripoti polisi akiwa na msaada wa mgambo. Akiwa kituoni hapo marehemu aliamuriwa kufanyiwa upekuzi ndipo akakimbia,” alisema Olomi na kuongeza;

 

“Baada ya kukimbia, askari walipuliza filimbi zilizowafikia askari wengine wa doria waliokuwa wakijiandaa kwenda kulinda kwenye mabenki. “Katika kumtuliza mtuhumiwa walipiga risasi hewani lakini hakusimama, kwa kuwa askari wetu waliacha watuhumiwa wengine wa ujambazi pale kituoni na mwenzao ameomba msaada kwa kupiga filimbi, walimpiga kijana yule risasi, bahati mbaya ikampata kiunoni; ni risasi moja tu wala siyo mbili; alipopelekwa hospitali baadaye alifariki dunia,” alisema Olomi.

Comments are closed.