The House of Favourite Newspapers

KIJANA ALIA…NAKIONA KIFO CHANGU

 

Mustafa Saidi

INAUMA sana! Kijana Mustafa Saidi (32), mkazi wa Ukonga-Mombasa jijini Dar anadai kukiona kifo chake kutokana na mateso makubwa anayoyapata akisumbuliwa na maradhi ya moyo kwa miaka nane sasa.  Kutokana na ugonjwa huo umemsababisha Mustafa kushindwa kufanya chochote wala kutembea na amekuwa mtu wa kubebwa na kufanyiwa kila kitu.

Akizungumza kwa taabu na Ijumaa Wikienda kwa sababu ya kukosa pumzi, Mustafa alisema alianza kusumbuliwa na ugonjwa huo tangu mwaka 2010. Alisema mara ya kwanza alianza kuona dalili za kuchoka akitembea tu kidogo au wakati wa kulala anapata shida hadi aweke mito mingi ya kulalia ndiyo aweze kulala huku mapigo ya moyo yakienda kasi.

Mustafa aliendelea kueleza kuwa, baada ya kuona hali hiyo mara kwa mara ilibidi aende Hospitali ya Amana ambapo walimfanyia vipimo na kugundulika kuwa ana tatizo la mishipa ya moyo kusinyaa hivyo walimpa barua ya kwenda Muhimbili ili aende wizarani kwa ajili ya kupangwa katika wagonjwa ambao watasafirishwa kwenda nje ya nchi kwa upasuaji.“Nilipofika Muhimbili, baada ya kunichunguza zaidi waliniambia kuwa nisubiri upasuaji watanifanyia hapohapo na walinilaza kama wiki mbili wakinipatia matibabu, baadaye nilitoka nikawa nakwenda kliniki tu,” alisema Mustafa.

Kijana huyo aliendelea kusema akiwa anahudhuria kliniki kwa miaka saba, mwaka huu mwezi wa tisa alipangiwa tarehe ya upasuaji na siku ilipofika wakati anaenda kwa ajili ya maadalizi walimwambia kuwa mishipa hiyo imewasili nchini, lakini ni kwa ajili ya watoto wadogo hivyo aendelee kusubiri mpaka itakapoletwa ya watu wazima.

Wakati akiendelea kusubiri, akiwa njiani anatembea alianguka kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya hivyo alipelekwa Muhimbili na madaktari walivyomuona tu waligundua tatizo limekuwa kubwa ambalo linahitajika kufanyiwa matibabu mapema kwani hali imeshakuwa mbaya.

“Nilivyorudi hospitalini nilikutana na jopo la madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo ambapo walivyoangalia walimuita baba wakamwambia yuko tayari wanifanyie upasuaji, baba alikubali, lakini tulimuita daktari mmoja tukamueleza kwamba hatuna fedha kabisa akasema wanaangalia afya ya mtu fedha baadaye,” alisema. Aliendelea kusema kuwa baada ya kuambiwa hivyo alilazwa kwa ajili ya upasuaji wakati akijiandaa kwenda kwenye chumba cha upasuaji nesi alimuambia kuwa inahitajika risiti ya malipo ya upasuaji huo kwanza ndiyo akafanyiwe ambapo hawakuwa na fedha hiyo.

“Niliumia kuambiwa kuwa siwezi kufanyiwa upasuaji kwa sababu ya kukosa fedha, nililia sana kwa uchungu kwa sababu hali yetu naijua ilivyokuwa duni na hatukuwa na jinsi ilibidi turudi nyumbani huku bado naumwa sana na fedha inayohitajika ni shilingi milioni tatu na laki mbili na nusu, lakini hatuna uwezo nayo kabisa ndiyo maana nasema ninakiona kifo changu.”

Baada ya kuambiwa hivyo walirudi nyumbani wakiwa wanatoa machozi na alijua ndiyo mwisho wake kwani anaenda kufa kwa sababu familia yake haina uwezo na mpaka sasa yuko nyumbani hapo hawezi kutembea wala kulala.

“Sasa hivi nasubiri kifo tu sina uwezo wa kujitibia wala familia yangu kwa sababu zamani kazi yangu ilikuwa ni udereva, lakini ndiyo hivi siwezi kufanya tena, naumia mno ila yote namuachia Mungu ndiyo mwenye uamuzi,” alisema. Kwa yeyote anayeguswa na tatizo la kijana huyu anaweza kumsaidia chochote kwa ajili ya matibabu yake kupitia simu yake ya mkononi kwa namba; 0719 993 736.

STORI: IMELDA MTEMA, DAR

Comments are closed.