The House of Favourite Newspapers

Kijana kuwashtaki wazazi wake kwa kumzaa!

 

KIJANA mwenye umri wa miaka 27 amepanga kuwashtaki wazazi wake kwa kumzaa huko India. Raphael Samuel amesema anajua ni vigumu kwa wazazi kuomba ruhusa kwa mtoto kabla ya kumzaa lakini akasisitiza kuwa haukuwa uamuzi wake azaliwe

Anasema hakuna mtoto aliyekubali kuzaliwa ili aje ateseke na tabu za dunia. Samuel ana mahusiano mazuri na wazazi wake ambao wote wawili ni wanasheria na wanalichukua suala hilo kama kichekesho.

 

Bi Kavita Karnad ambaye ni mama yake mzazi imebidi atoe tamko kutokana na “kadhia aliyoianzisha mwanangu hivi karibuni.”

 

“Kwanza, navutiwa kwa ujasiri aliouonyesha mwanangu kwa kutaka kutupeleka mahakamani akijua fika kuwa sisi ni wanasheria. Na iwapo Raphael atatupa maelezo yenye mashiko juu ya namna gani tungepata idhini yake kabla hajazaliwa, basi nitakubali makosa yangu,” amesema mama huyo kwenye taarifa yake.

 

 

Mwaka mmoja uliopita, alianzisha ukurasa wa Facebook uitwao Nihilanand, ambao una picha kadhaa akiwa na ndevu ndefu za bandia na mabango mengi ya ujumbe wa filosofia yake.

 

“Kulazimisha mtoto azaliwe na kumlazimisha awe na kazi si ni sawa na kumteka na kumfanya mtumwa tu?” ni moja ya mabango yake, ambapo jingine linasema, “Wazazi wako walikuzaa wewe badala ya kunua mwanasesere ama kufuga mbwa. Hawakudai chochote, wewe ni starehe yao tu .”

 

Raphael anasema alianza kuwa na fikra hizo tangu akiwa na umri wa miaka mitano.

 

“Nilikuwa mtoto wa kawaida kabisa. Siku moja nilikuwa na hasira na sikutaka kwenda shule, lakini wazazi wangu walinilazimisha kwenda.

 

“Hivyo nikawauliza: ‘Kwa nini mlinizaa? Baba yangu hakuwa na jibu. Naamini laiti angenijibu siku ile labda nisingeendelea kuwaza hivi.”

 

 

Mawazo hayo yalivyoendelea kukua akaamua kuwaeleza wazazi wake. Anasema mama yake aliyapokea “vyema” lakini baba yake bado “anajifikiria” juu ya wazo hilo.

 

“Mama amesema alitamani kuonana na mimi kabla ya kuzaliwa kwangu, na laiti angelifanikiwa basi nisingezaliwa,” anasema Raphael huku akicheka na kudai kuwa anaona hoja kwenye jibu la mama yake.

 

“Ameniambia kuwa alikuwa bado yu mdogo kipindi ananizaa na hakujua kama alikuwa na chaguo jingine, lakini hiyo ndiyo hoja yangu, kila mtu ana chaguo la kufanya katika maisha yake.”

 

Raphael anasema anaenda mahakamani kwa sababu moja tu kuwa, dunia itakuwa sehemu salama zaidi bila ya uwepo wa wanadamu na si vinginevyo.

 

Miezi sita iliyopita wakiwa wanapata kifungua kinywa, alimwambia mama yake kuwa anajipanga kumpandisha kizimbani.

 

“Amesema hana neno, lakini amenionya kuwa nisifikirie kuwa atanionea huruma mahakamani. Ameniambia ataniangamiza mahakamani. ”

 

Kwa sasa kijana huyo anatafuta wakili, lakini inamwia vigumu kumpata ambaye atamsaidia katika suala hilo.

 

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.