The House of Favourite Newspapers

KIJANA: NAKUFA NA JIONA AELEZA ANAVYOTESEKA, INAUMA SANA

KIJANA Lusubilo Sinunu (18), mkazi wa Kata ya Kisegese-Busokelo Wilaya ya Rungwe mkoani hapa ametamka maneno mawili; “Ninakufa ninajiona.”  Lusubilo alitoa maneno hayo hivi karibuni alipokuwa akielezea jinsi anavyoteseka akiwaomba watu kumsaidia kufuatia kupata balaa.

Lusubilo alijikuta akivunjika uti wa mgongo baada ya kuanguka kwenye mti alipokuwa akipunguza matawi mapema mwezi Januari, mwaka huu.Kijana huyo kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya baada ya kukosa pesa za kusafirishwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar kwa ajili ya matibabu zaidi.

Lusubilo alisema aliombwa na jirani yake kumsaidia kupunguza matawi katika miti, lakini alifanikiwa kukata tawi moja tu na alipokata tawi la pili ndipo alipopata ajali hiyo. “Kwa hali ilivyo na hapa sina msaada, nakufa huku ninajiona,” alisema Lusubilo. Akizungumza kwa taabu na gazeti hili huku akibubujikwa na machozi, Lusubilo alisema yeye hana baba, mama ndiye anayemuuguza baada ya kuuza mifugo yote na nyumba waliyokuwa wakiishi.

Kwa upande wake, mama mzazi wa Lusubilo, Ndisi Kyeja (43) alisema alilazimika kuuza kila kitu, lakini bado juhudi zake zimegonga mwamba baada ya kukosa pesa za kumsafirisha kwenda Muhimbili kiasi cha shilingi milioni moja na laki moja zikiwa ni pesa za mafuta kwa ajili ya gari la wagonjwa na pesa za kujikimu dereva.

Kyeja aliiomba jamii ya Watanzania kumsaidia ili kuokoa maisha ya mtoto wake. Mama huyo mjane mwenye watoto nane alisema hajui hatma ya watoto wake kwa kuwa mashamba yote na vitu vyote ikiwemo nyumba wanayoishi na watoto ameshauza.

Katika kuhangaika, Katibu wa Chama cha Maofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mbeya, Gerald Mwaulesi, baada ya kumuona mama huyo alimshirikisha mwenyekiti wa chama hicho, Mustafa Mjema ambapo waliamua kuchangishana pesa ili kukomboa nyumba kuwanusuru watoto ambapo juhudi zao zilizaa matunda na kufanikiwa kukusanya shilingi laki tatu.

Viongozi hao walikabidhi pesa hizo kwa mnunuzi wa nyumba hiyo, Julius Mwakyoma, mkazi wa Kisegese na kuirejesha nyumba hiyo. Akipokea pesa hizo, Mwakyoma alisema hakuwa na lengo la kununua nyumba hiyo bali ni huruma kumsaidia mama huyo ambaye hana msaada wowote.

Pamoja na jitihada zilizofanywa na maofisa ustawi wa jamii kukomboa nyumba hiyo, bado Mwakyoma anadai shilingi laki moja alizotoa kwa ajili ya kumsafirisha mgonjwa kutoka kijini hadi Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya. Wakati Lusubilo akiwa hospitalini hapo, maofisa hao walikuwa wakijitolea kumlipia malazi na chakula, lakini kwa sasa wamekwama hivyo mama huyo kulazimika kulala nje ya hospitali akisubiri muujiza wa kumsafirisha mwanaye kwenda Muhimbili.

Baada ya kuona hakuna kinachoendelea, Lusubilo aliruhusiwa kurudi nyumbani, lakini akiwa njiani hali ilikuwa mbaya, akakimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe ambao nao walimrejesha Rufaa kupitia Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Rungwe, Yohana Kibona.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busokelo alisema alipata taarifa ya tukio hilo na kuahidi kushirikiana na Maofisa Ustawi wa Jamii na wao wanafanya changizo ingawa alisema kwa sasa halmashauri haina fungu la mafuta kwa ajili ya kumsaidia kumsafirisha mgonjwa. Wadau wanaombwa kuchangia kwa hali na mali kuokoa maisha ya kijana huyo ambaye amefanyiwa upasuaji na kupata ulemavu. Kufuatia ulemavu huo, kinahitajika kiti au baiskeli ili aweze kukaa. Kama umeguswa na habari hii unaweza kuchangia chochote kwa namba ya simu; 0756 448824.

STORI: Ezekiel Kamanga, Mbeya

Comments are closed.