visa

Kijiji Chawatimua Watatu kwa Uchawi

WANANCHI wa kijiji cha Mahulu wilayani Makete mkoani Njombe, wamewatimua kijijini hapo wananchi watatu waliopigiwa kura nyingi wakiwatuhumu kuwa ni wachawi.   Katika mkutano wa dharura  uliofanyika Februari 13, 2020, wananchi hao wamefikia hatua hiyo kutokana na vitendo vya kishirikina wanavyofanyiwa walimu na wananchi kudai kuwa wanakabwa na kufanyiwa vitendo vingine vya ushirikina usiku.  

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ngao Ndelwa, katika mkutano huo amewaeleza wananchi hao kwamba sababu ya kuitisha mkutano huo ni kutokana na ombi la wananchi wengi kijijini hapo kutaka upatikane muafaka baada ya kuona vitendo vya ushirikina vinazidi kwa walimu pamoja na wananchi wenyewe.  
 
Baadhi ya wananchi wametoa maoni yao kuhusu vitendo vya ushirikina kijijini hapo kwa kueleza namna wanavyofanyiwa hasa nyakati za usiku ambapo mmoja wao, Mary Sanga, amesema yeye huwa anatolewa kitandani na kulazwa chini na mumewe kujikuta amelala na mwanamke mwingine.
 
Mmoja wa walimu katika Shule ya Msingi Katenga (jina linahifadhiwa) ameleza alivyojikuta amekatwakatwa miguuni kishirikina usiku na kujigundua baada ya kuamka asubuhi.   Pia, aliainisha changamoto iliyompata mwalimu mwenzake wa shule hiyo na mtoto wake mchanga kufanyiwa ushirikina baada ya kuwaadhibu viboko vitatu wanafunzi waliochelewa shule na hivyo mwalimu huyo kuapa kutomchapa mwanafunzi yeyote hata kama atafanya kosa.  
 
Maoni mengi ya wananchi hao katika mkutano huo yakawa ni wao wapige kura za siri na wale watakaopigiwa kura nyingi watakuwa na maamuzi juu yao. Baada ya zoezi la kupiga kura kufanyika ukafika muda wa kutangaza matokeo ya kura hizo, kama ilivyotangazwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Happy Mahenge.  
 
Maamuzi ya mkutano huo yakawataka watuhumiwa watatu waliopata kura nyingi kuliko wenzao waondoke kijijini hapo haraka iwezekanavyo huku wale waliopata kura chache wakitakiwa kuonana na viongozi wa kijiji na kata mara baada ya mkutano huo kumalizika.  
 
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Kipagalo, Hebron Mahava, amesema hana pingamizi na maamuzi hayo ya wananchi katika mkutano huo dhidi ya watuhumiwa na taarifa hiyo ataichukua na kuipeleka ngazi za juu.
 
Toa comment