The House of Favourite Newspapers

Kiki za Faragha Ziliwabeba Mastaa Hawa!

MUNGU anawaona! Ndivyo unavyoweza kuwaambia mastaa ambao kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa wakifanya makosa ya kimaadili kisha kuomba msamaha.

Hii ni kwa sababu hakuna ambaye alishawahi kupata adhabu kali kutokana na makosa hayo ambayo wamekuwa wakiyafanya hasa ya kuachia picha chafu, video za utupu, nyimbo zenye maneno ya matusi na makosa mengineyo hasa ya mitandaoni.

 

Ishu hii imeibua mjadala mkubwa kutoka kwa wadau ambao wanaona si sawa kwa jambo kama hilo kuendelea kufumbiwa macho kwani linashusha hadhi na thamani ya mamlaka husika ambazo zipo kwa ajili ya kusimamia mienendo ya kazi za wasanii hao.

 

Miaka miwili iliyopita, kulisambaa video zilizokuwa zikimuonesha staa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz akiwa na mzazi mwenzake ambaye ni raia wa Uganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambapo video hizo zilikuwa zikiwaonesha wawili hao wakiwa faragha, jambo ambalo liliwafanya Basata (Baraza la Sanaa la Taifa) kumuita Diamond au Mondi na kumpa onyo huku akitumia nafasi hiyohiyo kuomba msamaha kwa Watanzania kutokana na video hiyo.

 

Kitendo cha msanii huyo kuachiwa na kutoku-chukuliwa hatua zozote, kwa sababu aliomba msamaha, huenda baadhi yao wame-tafsiri kama ndiyo chanzo cha matatizo haya kwani walifuatia wasanii wengine kama vile Amber Lulu, Gigy Money na Amber Rutty.

KWA NINI WANA-PIGA HIZO PICHA?

Hili ndilo swali la msingi ambalo watu wengi wamekuwa wakijiuliza kwamba ni sababu zipi zinazowasababisha wasanii hao wapige picha wakiwa faragha, mambo ambayo ni siri baina ya watu wawili ambao wameshiriki jambo hilo? Je, wanakuwa wapo kazini kama wale wanaofanya kazi hiyo ya kucheza picha za ngono huko kwenye nchi za Magharibi (strippers)?

 

Jibu ni hapana sasa tatizo linakuwa wapi? Au wanakuwa wametumia vilevi ambavyo huwapelekea wao kufanya mambo bila kujielewa?

Lakini kimsingi, maswali yote ukijiuliza unaona kwamba jibu ni hapana.

 

Baadhi ya watu waliweza kutoa maoni yao kufuatia suala hili ambalo limekuwa likiwakera watu wengi sana ambapo wengi husema kuwa kigezo cha kuomba msamaha na kusamehewa, wamekichukulia kama sababu ya kuendelea kukosea kwa ajili ya kufanya kiki kisha kuomba msamaha.

 

Hapa chini nakuletea orodha ya wasanii hao pamoja na makosa yao waliyowahi kuyafanya hapo nyuma, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao, waliishia kuomba msamaha na mambo yakawa yameisha kwa namna hiyo.

 

MONDI

Huyu ni mmoja wa mastaa wanaofanya vizuri sana kwenye kuusogeza muziki wetu kimataifa zaidi. Pia ni mmoja kati ya wasanii ambao video zao ziliwahi kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Tena kwa Diamond ilitokea mara mbili ambapo ya kwanza alikuwa na Zari baada ya kupewa onyo na Basata akatulia, lakini baada ya muda ikaibuka tena nyingine akiwa na mzazi mwenzake, mwanamitindo Hamisa Mobeto, lakini na hilo likapita tu kwani alipewa nafasi nyingine ya kuomba radhi.

SANCHI

Huyu ni mwanamitindo mwenye shepu matata Bongo. Yeye suala la kujirekodi picha za utupu sio ishu kwake. Amekuwa akifanya na ameendelea kufanya kupitia ukurasa wake wa Instagram na hajawahi kuomba radhi, achilia mbali kukutana na rungu la Basata.

 

GIGY

Gigy Money ni mmoja wa wasanii hao ambao walishawahi kuingia kwenye msala huo kabla hajawa msanii wa kuimba, wakati akiwa video queen. Alikuwa akipiga picha za nusu utupu, hali kadhalika hata kwenye hizo video, alishawahi kuitwa na Basata, lakini hakukuwa na lolote lililofanyika dhidi yake.

 

AMBER LULU

Kama ilivyo kwa Gigy kuhusu kuitwa kwake na Basata hata huyu naye ni hivyohivyo kwani hakuna lolote lililoonekana kama ni hatua iliyochukuliwa juu yao kuhusiana na picha hizo.

 

AMBER RUTTY

Mwanadada huyu ambaye umaarufu wake ulipatikana kupitia video yake chafu ambayo ilisambaa sana mpaka kufikia kukamatwa na polisi, lakini jambo la kushangaza zaidi, muda mchache baadaye ilisambaa tena video nyingine huko mtandaoni ambayo inafanana na ile ya kwanza na yeye mwenyewe aliiachia video hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram iliyomuonesha akichezea nguo za ndani.

 

Ni vizuri mamlaka husika zikaliangalia suala hili kwa jicho la tatu ili wasanii hawa wasitumie kiki hizi kwa makusudi wakiamini wataomba radhi na kisha kusamehewa!

AMMAR MASIMBA

Comments are closed.