KIKOKOTOO CHA WASTAAFU SIASA ILIINGIA!

NCHI ilikuwa katika mjadala mkubwa juu ya suala la kanuni za mafao yatokanayo na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wastaafu, kanuni zilizotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), kabla ya Rais John Pombe Magufuli kutengua, zililalamikiwa sana na wananchi, lakini pia na baadhi ya wanasiasa, hasa baadhi ya wabunge.

 

Kanuni hizo zilitaka malipo ya mkupuo kwa wastaafu (Lumpsum) kupungua kwa zaidi ya asilimia 50, kutoka asilimia 50 ya mapato yote ya pensheni iliyokuwa awali, mpaka asilimia 25 tu ya malipo yote ya pensheni. Jambo hili lilizua mjadala mkubwa nchini, hasa malalamiko kutoka kwa wafanyakazi ambao ndiyo walikuwa waathirika.

 

Ukweli ni kwamba hifadhi ya jamii ni haki ya msingi kwa wananchi wote, ni nyenzo ya kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa na uhakika wa matibabu kwa wote (Universal Health Care) kwa kupitia fao la matibabu, ni njia rahisi ya kupata mikopo na kuongeza mtaji kwa biashara za wananchi na ni akiba ya mafao kwao na wategemezi wao.

 

Kwa maana hiyo hifadhi ya jamii siyo tu ni uwezeshaji bali ni ukombozi kwa wananchi hasa wa hali ya chini. Pensheni, kwa tafsiri rahisi ya hapa Tanzania, ni kama kibubu cha fedha za akiba ambacho kila Mtanzania aliyeko kwenye sekta rasmi ya ajira anaweka, yeye na mwajiri wake. Kwa sasa nchini mwetu kuna Watanzania milioni 2.1 wanaofanya kazi katika sekta rasmi ya ajira ambao moja kwa moja wanaguswa na suala hili la pensheni.

 

Hivi sasa wazee wastaafu kwenye utumishi wa umma na wale wa kwenye sekta binafsi wengi wao walikuwa ni wanachama wa NSSF. Kapu hili hatimaye hutumika kulipa watu mafao wanapostaafu ikiwemo ya kila mwezi na yale ya mkupuo.

 

Mafao hulipwa kwa kanuni maalum au kwa lugha ya sasa kikokotoo. Lengo la pensheni ni kumfanya aliyekuwa mfanyakazi kutoanguka kwenye umaskini baada ya kupoteza nguvu. Pensheni humwezesha mstaafu kuishi maisha ya kawaida na yenye furaha. Ifahamike kuwa Watanzania wengi sana hivi sasa ambao ni wazee wanaishi maisha ya shida sana kwa sababu nchi yetu haina pensheni kwa wote.

 

Mjadala mkubwa ulikuwa juu ya kanuni maalum inayotumika kukotoa mafao ya wastaafu wetu, kanuni hiyo ndiyo huitwa kikokotoo. Wastani wa mishahara ya miezi 36 ya mwisho anayolipwa mfanyakazi anayekaribia kustaafu ndiyo inayotumika kukokotoa pensheni yake kwa jumla. Asilimia 50 ya mafao yake ndiyo hutolewa kama mafao ya mkupuo (Lumpsum) na kinachobaki hulipwa kama pensheni ya kila mwezi, lakini hilo likapinduliwa na kuwa asilimia 25.

 

Mjadala wa kanuni zilizotungwa na SSRA kama takwa la marekebisho ya mwaka 2018 ya Sheria ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zilileta shida kwani kikotoo kilipunguzwa mafao ya jumla ya mkupuo ya mstaafu kwa asilimia 50, kutoka asilimia 50 aliyokuwa anapewa zamani mpaka asilimia 25 iliyopangwa, ilihuzunisha wengi.

 

Hata baada ya marekebisho ya Sheria ya mwaka 2014 bado iliyokuwa mifuko ya PSPF, GEPF na LAPF ililipa wastaafu wake asilimia 50 ya jumla ya mafao yao kwa mkupuo.

Mfuko pekee ambao ulilipa asilimia 25 baada ya Sheria ya mwaka 2014 ni NSSF, jambo ambalo lilipingwa na vyama vya upinzani bungeni wakati huo, lakini baadhi ya wanasiasa waliingiza siasa na kufumbia macho hili kwa sababu ni jambo lililowahusu wastaafu wachache wa sekta binafsi, jambo ambalo lilizalisha ubaguzi kati ya wastaafu na ndiyo maana nasema ilikuwa siasa za siasa.

 

Tulitarajia kanuni mpya ziwainue hawa wastaafu wachache wa sekta binafsi kutoka kupata mafao ya mkupuo ya asilimia 25 mpaka asilimia 50 ambayo wastaafu wengi walikuwa wanapata, lakini hata wale waliokuwa wanapata asilimia 50 nao walipunjwa na kupewa asilimia 25 sasa.

 

Kwa mfano kama jumla pensheni ya mfanyakazi wakati wa kustaafu itakuwa ni Shilingi 11 milioni, kwa kutumia kikokotoo mfanyakazi huyu kupewa asilimia 50 ya mafao yake yote, ambayo ni Shilingi 5.5 milioni kwa mkupuo wa kwanza mara tu pale anapostaafu. Na Shilingi 5.5 milioni, asilimia 50 zilizobaki angepewa kidogokidogo kila mwezi kwa maisha yako yote atakayobaki hai.

 

Kile ambacho kilipitishwa na SSRA kabla Rais Magufuli hajatengua mfano wake ni huu, kama jumla ya pensheni ya mfanyakazi wakati wa kustaafu ingekuwa ni Shilingi 11 milioni, kwa kutumia kikokotoo walichopitia SSRA mfanyakazi huyu angepewa asilimia 25 ya mafao yake yote, hivyo angepata shilingi 2.75 milioni kwa mkupuo wa kwanza mara tu pale anapostaafu na asilimia 75, yaani shilingi 8. 25 milioni zilizobaki angepewa kidogokidogo kila mwezi kwa maisha yako yote atakayobaki hai. Hii ilikuwa hatari sana.

 

Kanuni hii ilitungwa kisiasa zaidi na ndiyo maana Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama (Mb), analaumiwa kwa kupitisha dhulma hii ambayo Rais Magufuli ameiona na kutengua haraka sana.


Loading...

Toa comment