
Kikongwe Regina Mbawala, mkazi wa Bunju B, Kata ya Mabwepande jijini Dar aliyewahi kuripotiwa na gazeti hili akihitaji msaada, amelishukuru Gazeti la IJUMAA WIKIENDA na wasamaria wema wote waliojitokeza kumsaidia huku akitoa neno la huruma kwa wanawe waliomtelekeza.
Kikongwe huyu baada ya tembelewa kwa mara nyingine na mwandishi wetu, aliwashukuru wasamaria wema waliojitokeza kumsaidia chakula, matibabu na mambo mengine.
Alipoulizwa kuhusu wanawe wanaodaiwa kumtelekeza alisema kuwa, hakuna mwanawe hata mmoja aliyejitokeza kumuona. Bibi huyo aliwalaumu watoto wake hao aliosema amewalea kwa kujinyima na kumalizia kwa kusema yote hayo anamuachia Mungu.
“Mimi hapa wanaoendelea kunilea ni hawa majirani na ndiyo nnaowaona kama ndugu zangu, wanangu wa kuwazaa wao wananioana kama bwege tu, lakini waache tu Mungu yupo,” anasema kikongwe huyo kwa uchungu.
Baada ya taarifa za kikongwe huyo kurushwa na vyombo vya habari vya Global, wasamaria wema kutoka pande mbalimbali ulimwenguni walijitokeza na kumsaidia bibi huyo sehemu ya misaada ambayo ilipokelewa na Diwani wa Kata ya Mabwepande, Muhajirina Kassim Obama.
Akiwa ameshaanza kusaidiwa mambo hayo, Diwani Obama alisema kilichobaki hivi sasa ni kumjengea bibi huyo chumba kinachoeleweka ili aweze kulala mahali pazuri na kuepukana na mvua zinazomnyeshea kwenye kibanda cha mabati huku kikiwa hakina mlango.
Watoto wa kikongwe huyo wanadaiwa kumtelekeza mama yao na kwenda kuponda raha na familia zao ambapo mwanawe wa kiume anaishi Chanika jijini Dar na wa kike ameolewa na anaishi na familia yake huko Bagamoyo mkoani Pwani.
Diwani Obama aliwaomba wasamaria wema kuendelea kumchangia kikongwe huyo kupitia namba ya simu; 0658 858 562 yenye jina la MUHAJIRINA KASSIM OBAMA.
Stori; Richard Bukos, Dar

