The House of Favourite Newspapers

Kikuku cha Dada Muuza Soseji-14

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA WIKIENDA:

Alichokifanya Dan ni kumpa dakika mbili tu akiamini kama ni wa kuaga, atashuka na kuondoka, akawa amekaza macho kwenye kioo cha pembeni cha gari aliangalia gari la Abas kwa kutumia kioo hicho.

SASA JIACHIE MWENYEWE…

Alipoona dakika mbili zimepita, Dan alishuka kwenye gari lake kwa hasira tele na kulifuata gari la Abas ambapo kwa mbali, aliweza kuwaona wawili hao wakiwa wameng’ang’aniana uso kwa uso wakila denda zito bila kujali mazingira.

Mwanga wa taa za kwenye dashibodi ndani ya gari hilo ulimsaidia Dan kuwaonesha huku akichanganyikiwa kwa alichokuwa akikiona ambacho hakukitegemea.

Aliuvaa mlango wa gari upande wa abiria, akaufungua na kumvutia nje Salama mpaka akaanguka puu…

“Mungu mkubwa, sasa ndiyo nimejua siri ya yale yaliyokuwa yakifanywa na nyie mbele yangu kule baa, mimi si mjinga nilijua kuna kitu. Tangu lini mke akakataa nyama ya mume wake akaikubali ya shemejiye?” alisema Dan huku akimpokonya simu Salama na kuanza kukimbia kwenye gari lake na kuondoka zake eneo hilo tena kwa kasi ya kutimua vumbi.

Salama alijaribu kumkimbilia Dan kwa kumfukuzia lakini alimkosa, gari lilishaondoka, akarudi kwenye gari la Abas akitembea kwa kuchechemea kwani aliumia kidogo baada ya kuanguka kwa kuvutwa. Muda wote huo, Abas alikuwa ametumbua macho akiuangalia mchezo huo kwa moyo uliojaa wasiwasi na hofu kuu lakini pia na kaaibu juu…

“Darling, rafiki yako kaondoka na simu yangu, itakuaje sasa? Mimi bila simu siwezi kurudi nyumbani ujue,” alisema Salama huku akiwa anamwaga machozi chapachapa mpaka yakakusanyika katikati ya kidevu…

“Da! Kwani meseji zangu zipo ndani ya ile simu?” aliuliza kwanza Abas baada ya kushtuka na kukaa sawasawa kwenye siti…

“Zimejaa tele, tena mbayambaya kabisa. Yaani sijui itakuaje?”

“Salama mimi ndiyo nimechanganyikiwa kabisa hapa nilipo. Kwanza najua urafiki wangu na jamaa ndiyo umevunjika na jamaa nimetoka naye mbali sana. Yaani sijui nani atasuluhisha mgogoro huu mzito na wa aibu?” alisema Abas akilalia usukani wa gari lake…

“Mi sina wasiwasi na urafiki wenu kufa wala kuvunjika, ila sasa wasiwasi wangu je, mume wangu akipiga simu na kupokea yeye itakuaje? Maana anaweza kupokea akasema anayoyajua kuhusu mimi, si itakuwa balaa Abas…pana ndoa kweli hapo? Hivi ni kwa nini lakini Dan amenifanya hivi…

“Halafu nilishasema mimi sijawahi kusaliti ndoa yangu jamani, ni mara yangu ya kwanza tangu nifunge ndoa. Matokeo yake ni haya sasa, yaani najutaje,” alisema Salama kwa sauti ya kulalamika sana huku machozi yakiendelea kumchuruzika mpaka kwenye kifua sasa.

“Ngoja nimpigie simu kwanza, mjinga sana naye. Sasa tatizo kama hili yeye anakimbilia kuchukua simu ya mwanamke kwa ajili ya nini?” alihoji Abas akiseti simu sawasawa, akampigia Dan.

Simu ya Dan iliita wee bila kupokelewa hata aliporudia mara mbilimbili akajua kwa nini hapokei…

“Hapokei,” alisema Abas, Salama akahisi haja ndogo ikitaka kumtoka yenyewe. Ukimya ulipita, Salama alilalia siti ya gari, Abas yeye aliendelea kuegemea usukani…

“Sasa?” aliuliza Abas kwa sauti ya uchovu…

“Mi ngoja niende, lakini alichonifanyia ndugu yako siwezi kusahau,” alisema Salama huku akishuka kwenye gari la Abas na kuanza kutembea kwa mwendo wa kusuasua.

Akiwa anaelekea nyumbani kwake sasa, Salama alipata wazo kwamba, ni vyema kama atamfuata Dan nyumbani kwake akachukue simu tu na si vinginevyo la sivyo ni balaa kwa mume wake…

“Nyumbani kwake si napafahamu bwana. Sasa kwa nini nisiende?” alijiuliza akichanganya miguu kwenda huko na bila kupitia kwake.

* * *

Dan akiwa ndani kwake, sebuleni, simu ya Salama iliita, kwenye kioo lilisomeka jina la My Huz! Akajua ni mumewe Salama anapiga. Alitaka kupokea ili amtukane lakini akaona atakuwa ametenda kosa kubwa kwa mtu ambaye hajamkosea, akaiacha iite tu.

Mume wa Salama kule alikokuwa alishangaa sana mkewe kutopokea simu wakati si kawaida yake…

“Yaani huyu vipi leo? Ndiyo mambo ninayoyakataa haya,” alisema moyoni mwanaume huyo.

Kwa upande wake, Salama alitembea hadi nyumbani kwa Dan na kugonga geti kubwa kwa busara. Pombe zote zilikata na alijua akileta mchezo simu hataipata…

“Wamenifuata?!” alishangaa Dan baada ya kusikia geti likigongwa, akatoka kwa hasira. Alipanga akishafungua geti tu amvae Abas kwani ndiye mbaya wake…

“Ye anajua demu ni wangu kwa nini afanye vile? Kuna siku mimi nimetembea na demu wake yeyote?” alijiuliza Dan akifungua geti.

Alishangaa kumwona Salama peke yake, akigonga getini huku akimkazia macho tu. Wakakaziana…

“Dan nisamehe sana mpenzi wangu,” alianza kusema Salama…

“Kwa lipi?”

“Kwa yaliyotokea.”

“Unajua wewe Salama huna akili timamu. Yaani unajua kabisa kwamba jamaa ni rafiki yangu halafu unakwenda kufanya mauchafu kama yale, ni sahihi kweli?” alikuja juu Dan, mara simu ya Salama iliita ndani…

“Haya simu inaita. Lazima itakuwa mume wangu,” alisema Salama…

“Ingia ndani ukapokee,” alisema Dan akiliweka wazi geti.

Salama aliingia mbio hadi sebuleni kwa Dan, akachukua simu, kweli alikuwa mume wake…

“Haloo…”

“We mbona hupokei simu?”

“Nilikuwa chooni baba nanihi. Samahani sana.”

“Oke, kesho asubuhi nenda ofisini kuna mzigo nimeutuma ukauchukue.”

“Sawa.”

“Nipe Zuhura niongee naye.”

“Zuhura amelala.”

“Haamki? Haya poa, nitaongea naye asubuhi.”

“Sawa.”

Salama alipomaliza kuzungumza na simu na mumewe, alikata simu lakini asingeweza kutoka kwa sababu, Dan alifunga mlango mkubwa…

“Sikia Salama, lete hiyo simu maana nilikuwa sijaiifanyia kazi. Nimekuruhusu kuichukua kwa sababu hata mimi nilijua aliyepiga ni mumeo kwani alishapiga. Nilitaka kuipokea halafu nimtukane lakini nikasita kwa sababu zangu.”

Salama aliposikia ujumbe huo kwamba, kumbe Dan alitaka kupokea simu halafu amtukane mumewe alihisi kufakufa, kwani alishindwa kupata picha nini kingetokea.

“Sasa jamani Dan, mpenzi wangu si nimeshakwambia samahani lakini?” alisema Salama…

“Hata kama. Kama unataka amani ya ndoa yako leo ulale hapa kwangu.”

Salama akahamaki kusikia tamko hilo. Alihisi Dan alipania kumharibia na si bure…

“Baby haitawezekana. Kwani haijawahi kutokea.”

“Itatokea leo, kama haiwezekani nenda lakini hii simu inabaki hapa na mumeo akipiga nitamtukana sana mpaka akome kuzaliwa,” alisema Dan kwa sauti isiyotania huku akiingia chumbani kwake na funguo za mlango alikuwa nazo.

Salama alisimama sebuleni kwa dakika kama tatu akijifikiria aamueje, lakini akasikia simu yake ikiita, akakimbia kuingia chumbani…

“Nipe simu.”

Lakini kabla hajaiweka sikioni, simu ilikata alipoangalia kwenye kioo alibaini aliyepiga ni Abas…

“Kwa hiyo Abas ana namba yako siyo?” Dan aliuliza kwani hata yeye kabla hajampa simu Salama aliangalia kioo ili kuona namba iliyopiga…

“Ndiyo.”

“Kumbe na wewe una namba yake! Maana hapa naona umeisevu kwa jina la Shemela. Shemela ndiyo nini? Abas anaitwa Shemela?”

“Shemela ni kifupi cha shemeji langu.”

“Salama,” aliita Dan huku uso ukionekana kuumia kwa majibu ya Salama…

“Abee,” Salama aliitikia kwa sauti ndogo sana…

“Hizi namba mlipeana wapi?”

“Pale baa tulipokaa siku ile.”

“Muda gani?”

“Ulivyokwenda chooni,” ilibidi Salama awe mkweli kwani alijua akileta kujua, ataharibikiwa na mambo mengi hata ndoa.

“Kwa hiyo mlipeana kwa siri siyo?”

Salama alinyamaza kimya…

“Nakuuliza Salama, unajua unaweza kutoka ukiwa maiti humu ndani, mimi sina hasara, sina mtoto, sina mke, we unajua,” alifoka Dan, Salama akajua ni kweli.

“Ni yeye ndiye aliyeniomba namba za simu wakati wewe umekwenda chooni. Akasema wewe usijue.”

“Oke, mmeshawasiliana mara ngapi? Na naomba tena useme ukweli Salama, usinidanganye.”

“Mara nyingi na amekuwa akinipigia simu hasa usiku.”

“Kwa kitu gani hasa, salamu au?”

“Mimi ninavyojua amekuwa akinitongoza sana akisema ananipenda,” alisema Salama huku akijua ukweli wote toka moyoni mwake…

“Umeshalala naye kimapenzi?”

Je, unajua nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda, siku ya Jumatatu ijayo.

Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam

Comments are closed.