The House of Favourite Newspapers

Kila Kitu Kuhusu Sanchi Kubadili Dini

0

NI maarufu mno kwenye mitandao ya kijamii. Umaarufu wake umetokana na umbo lake matata linalovunja watu shingo wamuonapo.

Mwanzo alijulikana kwa jina la Sanchoka, lakini baada ya umaarufu akabadili jina, akawa anajiita Sanchi.

 

Huyu ni mwanamitindo wa Bongo ambaye ni maarufu zaidi mitandaoni (sosholaiti).

Jina lake halisi ni Jane Rimoy, mzaliwa wa mkoani Kilimanjaro.

 

Kabla ya kubadili dini kutoka Ukristo na kuwa Muislam, kisha kubadili dini na kujiita Surraiya, ilikuwa akiposti picha yake moja tu kwenye ukurasa wake wa Instagram, watu wote wanakaa kimya. Si kwamba alikuwa anawazuia wasiongee, bali aina ya picha alizokuwa akiziposti na kumuonesha sehemu kubwa ya mwili wake wazi.

 

Lakini kuna usemi usemao; kila jambo na wakati wake, hivyo ndivyo ilivyo kwa Sanchi, amewashangaza wengi na kuwafanya wasiamini kabisa kile alichoamua baada ya kubadilisha dini. Kubwa kuliko ni uamuzi wake wa kubadilisha kabisa mavazi yake aliyokuwa akivaa na kumuonesha tofauti kwenye jamii inayomzunguka.

 

Gazeti la IJUMAA kama ilivyo desturi yake kukusogezea kila staa anayevuma, ndivyo linafanya kwa Sanchi.

Katika mahojiano maalum (exclusive) na Sanchi, mwenyewe anafunguka kwa undani kabisa nini kilimfanya abadili dini, jina na mavazi yake;

 

IJUMAA: Mambo vipi Sanchi?

SANCHI: Poa kabisa.

IJUMAA: Umejificha siku hizi. Ni Corona au ndiyo mambo yako yamebadilika kabisa kuanzia mavazi na hata namna ya kuishi?

 

SANCHI: Corona ndiyo kubwa zaidi iliyonifanya nisionekane na niwe kimya, lakini kila kitu changu kipo mitandaoni.

IJUMAA: Sasa hivi kila kitu chako kimebadilika, kuanzia dini, jina hadi mavazi, kuna utofauti gani kwenye maisha uliyokuwa ukiishi kabla ya kubadili dini na haya ya sasa?

 

SANCHI: Utofauti ni mkubwa sana. Kwanza siwezi kuishi maisha ambayo yapo nje ya maisha ya Dini ya Kiislam hasa suala la mavazi yangu niliyokuwa nikivaa.

IJUMAA: Nani alikushawishi au ilikuwaje ukaamua kubadili dini?

 

SANCHI: Unapoamua kitu ni vizuri uamuzi utoke ndani ya moyo wako na siyo shinikizo la mtu. Mimi nisingeweza kukubali mtu ndiyo aniambie nibadilike.

 

IJUMAA: Huko nyuma ulikuwa ukivaa mavazi yasiyo na maadili kabisa na kubwa ulikuwa ukiposti picha mbaya kwenye mitandao ya kijamii, ila kwa sasa umekuwa mtoto wa Kiislam, una la kujutia kwenye hilo ukilinganisha na ulivyo sasa?

 

SANCHI: Siku zote wanasema, usipochafuka huwezi kujifunza. Kwa hiyo, sina la kujutia kwa sababu kuna vitu vingine lazima uvipite ili uwe mpya!

IJUMAA: Kuna tetesi kuwa umefanya hivyo kwa sababu umempata mwanaume ambaye anataka ubadilike ili aweze kukuoa, hivyo alitaka uwe tofauti na ulivyokuwa, unazungumziaje hilo?

 

SANCHI: Sidhani kama ni sahihi na kama mtu anakupenda, hawezi kukupa masharti hayo. Pia kama mtu moyo wake haujabadilika na kuamua kufanya jambo, hawezi kubadilika.

 

IJUMAA: Kuna baadhi ya picha zako bado zipo kwenye mitandao, kama umeamua kubadilika, kwa nini usizifute?

SANCHI: Ni vyema kuwepo, ipo siku kuna watu hawataamini kwamba nilitoka wapi na niko sehemu gani maana kuwaaminisha binadamu ni shida sana.

 

IJUMAA: Vipi kuhusu familia maana uamuzi wako ulikuwa wa ghafla sana, ukizingatia wewe umetoka kwenye familia ya Kikristo?

 

SANCHI: Hakuna tatizo kwenye familia yangu. Kikubwa ni kwamba, wanajua ninafanya nini. Isitoshe huo ni uamuzi wangu na mimi ni mtu mzima sasa. Kwa hiyo, hilo kwangu halikunipa shida kabisa, ukiangalia ndugu zangu wote Wakristo.

 

IJUMAA: Kwa sasa unaingia msikitini kusali?

SANCHI: Ndiyo na hata Sikukuu ya Idd nilikwenda msikitini.

IJUMAA: Nani alikupa jina la Surraiya?

SANCHI: Nilichagua mwenyewe.

 

IJUMAA: Kwa nini uliamua kuchoma nguo zako za zamani ulizokuwa ukivaa?

SANCHI: Ni kwa sababu siwezi kuzivaa tena na wala sikupenda kumpa mtu avae aonekane kama mimi.

IJUMAA: Ukitazama picha zako za sasa hivi unazoposti, hazina ‘likes’ kama zamani, hilo unalizungumziaje?

 

SANCHI: Hilo halinipi shida, wale watu wangu watanifuata tu, lakini kama walikuwa wana sababu kwenye ukurasa wangu, basi haina shida wakisepa.

IJUMAA: Kuna kipindi uliwahi kuonesha kiwanja kikubwa ulichonunua kwa ajili ya kujenga, vipi nyumba imekamilika?

 

SANCHI: Nikikamilisha kila kitu nitakiweka wazi, naona kama bado ni mapema mno kusema.

IJUMAA: Kipindi cha Mfungo wa Ramadhani ulikuwa ukiposti picha zako mbalimbali, lakini ulikuwa ukionekana umejiremba sana japokuwa umevaa kwa kujistiri, jambo ambalo halitakiwi, unasemaje kuhusu hilo?

 

SANCHI: Kwanza watu wajue nilifunga mwanzo mpaka mwisho, lakini ukweli ni kwamba, kufunga hakunifanyi nionekane hadi kwenye sura.

IJUMAA: Unawaambia nini mastaa wengine ambao hawajaamua kubadilika na kuchukua uamuzi kama wewe?

SANCHI: Unajua wakati wa kubadilika ukifika watabadilika, mimi nawaombea tu.

Makala: Imelda Mtema, Bongo

Leave A Reply