The House of Favourite Newspapers

KILA LA KHERI TAIFA STARS, WATANZANIA TUKO NYUMA YENU

TANZANIA leo Jumapili jioni itashuka uwanjani nchini Lesotho kutaka kuandika historia ambayo vijana wengi wa kizazi kipya hawakuwahi kuiona. Inacheza kuwania kufuzu fainali za Afcon ambazo imethibitishwa zitapigwa mwakani nchini Cameroon.

Stars ipo kundi L lenye timu zenye historia nzuri kisoka za Uganda, Cape Verde na Lesotho. Mechi hiyo ya Stars ni ngumu kwani licha ya matokeo ya jana Jumamosi baina ya Uganda na Cape Verde jijini Kampala lakini Tanzania inahitaji kushinda kwani hata mpinzani wake bado ana nafasi ya kufuzu.

Stars yenye pointi tano licha ya kumkosa straika wake namba moja leo, inahitaji kwa vyovyote vile kushinda ili kujiweka kwenye mazingira mazuri na pengine kumaliza kazi kabisa. Kama Stars ikishinda mchezo wa leo itafikisha pointi nane ambazo hazitaweza kufikiwa na Cape Verde na Lesotho, hiyo ikimaanisha kwamba Stars itakuwa imefuzu hata kabla ya mechi ya mwisho na Uganda.

Cha muhimu ambacho Stars wanapaswa kufanya leo Jumapili ni kutuliza akili uwanjani na kufanya kile vitu sahihi na kuhakikisha ushindi unapatikana ili kumaliza kazi na kuwapa raha mashabiki wa Tanzania. Mashabiki kibao watakuwa kwenye runinga zao jioni ya leo wakiwaombea Stars kila la kheri na ushindi upatikane. Kama kweli wachezaji wakiweza kutimiza azma hiyo ya mashabiki, tunaamini mapokezi ya wachezaji kwenye uwanja wa ndege wiki ijayo yatakuwa ya kihistoria kutokana na furaha ya aina yake ambayo yote itatokana na dakika 90 za leo.Image result for taifa stars

Ni ndoto ya kila Mtanzania na mwana Afrika Mashariki kuona Tanzania na Uganda zinacheza Afcon mwakani kwani Stars katika miaka ya hivikaribuni ilikwama kabisa na kushindwa kufikia hatua hiyo. Kimahesabu Uganda ana nafasi kubwa ya kufuzu kutokana na kuzichanga karata zake mapema kwa kuwatumia wachezaji wake wazoefu wa ndani na nje ya nchi.

Tunaamini kwamba kwa Stars hii tuna kila sababu ya kufuzu kutokana na kuwa na wachezaji wenye uelewa na ndoto za kufika mbali wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta ambaye leo atakuwa jukwaani kuwapa mzuka wenzie kwani ana adhabu ya kadi. Ni jukumu la kila Mtanzania kuiombea timu yetu kila kheri mwenyezi mungu awape wepesi vijana wetu wafanye kile ambacho kila shabiki anakihitaji.

Stars ikifuzu Afcon itakuwa ni mwanga mzuri kwa soka letu na mauzo ya wachezaji wetu kwani ndiyo mashindano makubwa kwenye ukanda wa Afrika ambayo yanatazamwa na mawakala wengi kutokana na ubora na umaarufu wake. Hivyo ni rahisi sana kuyatumia mashindano hayo kuitangaza nchi na wachezaji wenyewe binafsi kwani ni tukio ambalo kwa miaka mingi vijana wa kizazi kipya wamekuwa wakiliona kwenye runinga tu kwa kushangilia timu za mataifa mengine.

Comments are closed.