The House of Favourite Newspapers

Kila utakayemuona ana upungufu, cha msingi ridhika

f6a55__Lover-Couple-HD-Wallpapers-1080p-1024x5761

Na Erick Evarist

KAMA kawaida yetu waungwana, kila Jumamosi inapowadia tunakutana katika safu hii ili kuweza kujifunza mada mbalimbali za uhusiano. Wengi wanateseka kwenye mapenzi kwa kutofuata kanuni rahisi kabisa ambazo hazihitaji uwe umehitimu elimu ya chuo kikuu ndiyo uweze kung’amua.
Umri wa kusaka mwenza wa maisha unapowadia, kila mmoja anakuwa na mtazamo wake.

Kila mmoja anakuwa na matarajio yake kwa mwenza wake anayetaka kuwa naye. Mwingine atakwambia anamtaka mwanaume anayejiweza kiuchumi, mwingine atakwambia anataka mwanaume tajiri.
Haridhiki tu. Anaweza kumpata tajiri lakini akasema si ‘handsome’. Anataka mwanaume ambaye ana hadhi ya kumtambulisha kwa mashosti zake. Mwanaume ambaye mashosti zake wakimuona waseme ‘yeah, shosti kapata jembe la ukweli.’
Anafikiri ni sifa. Hajui inaweza kuwa chachu ya ushawishi wa marafiki zake na wao kumtaka. Akizubaa tu anajikuta ameibiwa mwanaume na kuanza kulaumu marafiki zake.
Hilo si kwa wanawake tu, hata wanaume. Wapo wanaume ambao nao wanamtaka mtu kwa tamaa. Anakuwa kama amepagawa pindi anaposaka mwenza. Leo atamtaka mwenye fedha, kesho atatokea mwingine mwenye umbo namba nane, anahamisha matamanio yake huko.
Hiyo inakuwa ndiyo staili ya maisha yake. Anajikuta anakuwa mtu wa kubadilisha warembo kila uchwao. Haridhiki. Mara aone mweupe ndiyo kila kitu, mara atake mwenye maji ya kunde na wakati mwingine atataka mweusi wa kung’aa.
Moyo wake kila siku una chaguo jipya. Hana msimamo. Akikutana na msichana barabarani, atasema ndiyo amefika. Akienda kazini, sekretari wake anamuona ndiyo sahihi zaidi kwa sababu huenda ana makalio makubwa tofauti na msichana wake waliyekutana naye baa.
Anajikuta anakuwa na listi kubwa ya wanawake kwani kila mmoja anamkosoa kwa lake. Huyu ana makalio makubwa mwingine hana. Huyu ‘wife material’ lakini anapoteza sifa kwa sababu hana muonekano wa kutembea naye barabarani. Eti anaona aibu kutembea naye.
Anachagua mwanamke utafikiri anachagua nyanya sokoni. Anafikiri atampata mwanamke atakayekuwa na sifa zote anazozitaka kwa pamoja.
Eti atampata mzuri wa sura, umbo, miguu mizuri, tabia na mwenye kujiweza kiuchumi. Mwanamke ambaye akikatiza mtaani kila mtu anavutiwa naye.
Marafiki zangu, ukweli ni kwamba hawezi kutokea mwanamke wa hivyo. Hawezi pia kutokea mwanaume ambaye mwanamke atakuwa na sifa zote kwa pamoja. Kuridhika ni jambo la msingi kuzingatia.
Kwa mtu ambaye anataka kuwa na uhusiano imara, anapaswa kujifunza kuridhika. Hakuna mtu spesho wa aina hiyo lakini suala la msingi ni kuangalia tabia. Hakikisha mwenzi wako unayetaka kuanzisha naye safari ya uhusiano ana tabia njema.
Mambo mengine yatajitengeneza taratibu. Ridhika kwa hali ambayo umemkuta nayo. Kama hana uwezo wa kiuchumi, isiwe sababu ya wewe kumuacha na kutafuta mwenye nazo. Wapo wengi ambao wameanzisha uhusiano kwa kigezo cha fedha na hata kufikia hatua ya kuoana lakini matokeo yake wameambulia mateso ndani ya ndoa.
Ridhika kwa hali uliyonayo. Ridhika kwa hali aliyonayo huyo unayetaka au tayari ni mpenzi wako. Vitu vingine ni matunzo tu. Kama umeshaona mwenzi wako ana tabia njema, ishi naye. Wekeni mikakati mizuri ya kufika pale mnapopataka.
Kama mpenzi wako hana muonekano mzuri, ridhika. Jukumu la kumfanya aonekane mzuri ni la kwako. Wewe ndiyo unatakiwa uwe wa kwanza kumuona mzuri hata kama wengine wakimuona wa kawaida. Haiwahusu.
Mvalishe mavazi yatakayokufurahisha wewe na si walimwengu. Mapenzi ya kweli yanajengwa na kuridhika. Unaposumbuliwa na tamaa, hakikisha ‘unazikontroo’. Jilazimishe kuridhika kwa mpenzi wako hata kama unaona kuna vitu hajakamilika, ni jukumu lako kumkamilisha na maisha yaendelee.
Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri ya kusisimua!

Comments are closed.