The House of Favourite Newspapers

Kili Marathon Yaacha Gumzo Moshi Huku Watanzania Waking’ara

0
Naibuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Abdallah Ulega akibonyeza kitufe kuanzisha mashindano ya Mbio za Kilomita 5 zinazodhamiminiwa na Kinywaji cha Gland Malter, mbio hizo ni za kuchangamsha mwili zilifanyika leo Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Maelfu ya wakimbiaji kutoka nje na ndani ya nchi wameshiriki mbio maarufu za Kilimanjaro Marathon 2021 zilizofanyika jana mjini hapa, huku Watanzania wakifanya vizuri katika mbio hizo.

Ikishirikisha wakimbiaji zaidi ya elfu 10 kutoka zaidi ya nchi 55, mkimbiaji wa Tanzania Augustino Sulle ameibuka mshindi katika mbio ndefu za kilometa 42.2 baada ya kutumia muda wa masaa mawili, dakika 18 na sekunde 4.

Baadhi ya wakimbiaji walipofika maeneo ya Kibosho.

“ Nilikuwa nimejiandaa vizuri sana kwa ajili ya kutoa ushindani katika mbio hizi ngumu, ambazo kwa miaka ya nyuma Wakenya ndio wamekuwa wakitawala,” amesema Sulle, anayejiandaa na michuano ya Olimpiki itakayofanyika mjini Tokyo, Japan kati kati yam waka huu.

Alisema Tanzania ina wakimbiaji wazuri wa kushindana na wengine wa mataifa mbalimbali lakini wanakwamishwa na mazoezi hafifu.

Mshindi wa kwanza mbio za Km 42 wanawake, Jackline Juma Sakilu akimaliza mbio kwa masaa mawili dakika 45 na sekunde 44.

Ameongeza kuwa mbio za Kilimanjaro Marathon ni nzuri kwa kujitambulisha na kujitayarisha kimataifa, hivyo akitoa wito kwa wakimbiaji wazawa kufanya maandalizi mazuri.

Watanzania wenzake, Michael Sanga na Charles Sule walimaliza katika muda wa  02:19:21 na  02:20:54  kila mmoja na kushika nafasi ya pili na ya tatu.

Mbio zikiendelea.

Katika upande wa wanawake, mkimbiaji wa kimataifa wa Tanzania, Jackline Sakilu ( 33)  alishinda kwa muda wa 02:45:44 akifuatiwa na washindi wengine kuanzia wa pili hadi wa tisa kutoka Tanzania. Mshindi wa kumi alikuwa Kremer Dominic kutoka Uholanzi.

“ Najisikia furaha sana kwa ushindi huu na mara ya mwisho kushiriki michuano hii ilikuwa mwaka 2014 na nilishinda nusu marathon,” anasema Sakilu, ambaye ameshiriki michuano mingi ya kimataifa ikiwemo ya nchini Colombia mwaka 2018.

Mshindi wa pili mbio za Km 42, Michael Kishiba akiwa kwenye spidi.

Mbio za mwaka huu za Kilimanjaro Marathon zilidhaminiwa na bia ya  Kilimanjaro Premium Lager, ikiwa mdhamini mkuu katika mbio kubwa za kilomita  42, Tigo Tanzania ( Half Marathon), na kinywaji cha kuongeza nguvu cha Grand Malt, kikidhamini wakimbiaji wa mbio za kujifurahisha na kuboresha afya za kilomita 5.

Wengine ambao walidhamini utoaji wa maji kwa wakimbiaji wakati na baada ya mbio ni Uniliver Tanzania, Simba Cement, TPC Sugar, Kilimanjaro International Leather Company Limited, Kibo Palace Hotel na watoa huduma rasmi  wakiwemo Garda  World Security, Keys Hotel na CMC Automobile.

Mshindi wa kwanza Km 42, Augustino Paulo Sulle katikati akiwa na mfano wa hundi baada ya kukabidhiwa na Naibu Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Abdallah Ulega na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Irene Mtiganzi (kushoto).

Katika mbio za half marathon kwa upande wa wanaume, Abel Chebet kutoka Uganda alishinda kwa muda wa  01:03:17, akifuatiwa na Watanzania  Gabreil Geay, Emmanuel Giniki na Calvin Sarakikya, walioshinda nafasi ya pili, tatu na nafasi ya nne baada ya kumaliza kwa muda wa 01:03:18, 01:03:31 na 01:04:12 kila mmoja.

Kwa upande wa wanawake, Watanzania waling’ara huku Failuna Matanga akishinda kwa muda wa 01:16:17, akifuatiwa na Angelina Tsere ( 01:17:43) na Anastazia Dolomongo ( 01:18:12).

Mamia ya washiriki pia walipamba mbio za kilomita 5 za Grand Malt wakiongozwa na Naibu Waziri Abdallah Ulega.

Wakimbiaji wa mbio za kujifurahisha Km 5 wakianza mbio zao.

Akiziungumza kabla ya sherehe za utoaji zawadi zilizofanyika katia chuo Cha Ushirika, meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi amesema ni furaha kwao kuendelea kuwa wadhamini wa mbio hizo kubwa kwa muda wa miaka 19 mfululizo tangu zilipoanzishwa mwaka 2003.

Mbali ya kudhamini mbio ndefu kupitia bia ya Kilimanjaro, kampuni yake ya Tanzania Breweries Limited (TBL) pia imekuwa ikidhamini mbio za kilomita tano kupitia kinywaji chake cha Grand Malt.

‘Tutaendelea kuwa sehemu ya mafanikio yam bio hizi na tumekuwa tukitoa msaada mkubwa katika kuzitangaza ndani na nje ya nchi,”

Wawakilishi wa Tigo wakimpa hundi mshindi wa pili mbio za Km 21, Gabriel Gerald. Naibu Waziri Ulega (katikati mwenye fulana ya njano) akishuhudia.

“Kupitia kampeni yetu ya ‘Twenzetu’, tumesafiri na treni kutoka Dar es Salaam mpaka mjini Moshi kwa kutoa matangazo mbalimbali, huku tukishirikiana na wateja wetu wakubwa wenye mabaa katika kuhakikisha zinakuwa na tija kimichezo na hata kiuchumi,” alisema.

Angelina Pesha, ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Tigo Pesa kutoka kampuni ya Tigo amesema toka mwaka 2015, kampuni yake imekuwa ikidhamini mbio hizo.

Na kupitia kampeni yao ‘Tigo Green for Kili-One Step One  Tree’ wamefanikiwa kupanda miti katika wilaya ya Hai ikiwa ni jitihada za kukuza mazingira kwa ustawi wa Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko wote barani Africa.

Sehemu ya mashabiki waliofurika Uwanja wa Chuo cha Ushirika kushudia tukio hilo.

Pia amewashukuru wadhamini wenza kwa ushirikiano wa kuzifanya mbio hizo kuwa kubwa zaidi nchini na hata nje ya nchi kwa kuendeleza utalii kupitia michezo ( Sports Tourism).

Katika mbio za jana, wakimbiaji walipata fursa ya kuuona bila kikwazo chochote Mlima Kilimanjaro, ambao ulijitokeza bila kufunikwa na ukungu.

Akitoa hotuba yake, Naibu Waziri wa Michezo, Abdallah Ulega alisema serikali inajivunia sana uwepo wa mbio hizo na kutoa ushirikiano katika kuhakikisha zinazidi kuwa na manufaa kimichezo na kiuchumi.

Amesema mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ukifaidikika katika sekta mbalimbali kama vile za usafiri, utoaji huduma za hoteli na chakula kwa migahawa na mama lishe ambao hufanya biashara kubwa wakati wa msimu wa mbio hizi.

Hivi ndivyo burudani ilivyokuwa.

Pia amewasifu washiriki, wadhamini, waandaaji kampuni ya  Kilimanjaro Marathon Company, waratibu, Executive Solutions na serikali ya mkoa wa Kilimanjaro kwa uboreshaji na ukuaji wa mbio hizo,

Washindi wa mbio hizo walijishindia vitita vya pesa pamoja na medali kutoka kwa waaandaji vilivyotolewa na wadhamini.

Mbio za Kilimanjaro Marathon 2021 zimeandaliwa na Kampuni ya Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa kitaifa na Kampuni ya Executive Solutions.

Leave A Reply