The House of Favourite Newspapers

Kilichojificha mgogoro wa Zanzibar -2

0

Naendelea kufafanua kilichojificha katika mgogoro wa kisiasa Zanzibar:

Kwa hakika, kinyume cha baadhi ya watu walivyoandika, hapakutokea mauaji ya kimbari wakati wa Mapinduzi Zanzibar Januari 12, 1964. Aliyeanzisha uvumi huo alikuwa John Gideon Okello aliyeandika kwenye kitabu alichokiita “Revolution in Zanzibar” yaani Mapinduzi ya Zanzibar kwamba watu zaidi ya elfu kumi waliuawa.

Simulizi ya  Okello na wengine waliokuwa Raha Leo wakiwemo vijana kutoka Sakura na Kipumbwi tutaifanya baadaye, kwanza tukumbushe kwamba mkesha wa Januari 12, mwaka 1964, Zanzibar haikuwa na jeshi. Kulikuwa na polisi waliokuwa wakiongozwa na Waingereza. Wengi wa askari polisi hao walikuwa raia wa Tanganyika.

 Serikali iliyopinduliwa haikuwa na jeshi kwa sababu ilikataa kuandikiana mkataba wa kijeshi na Uingereza kwa sababu ilihisi mkataba huo ungeonekana kuwa wa kikoloni.

Kwa vile hakukuwa na upinzani, Serikali ya Shamte ambayo mama mmoja alinipigia simu wiki iliyopita alisema ilikuwa ni ya kibaraka Sultan Jamshid Abdullah iliyokuwa madarakani, iliporomoka kirahisi.

Sasa tuwaangazie wanamapinduzi waliokuwa Raha Leo, makao makuu ya Mapinduzi, kwanza tumuangalie John Gideon Okello ambaye sauti yake ndiyo iliyokuwa ikivuma kwenye Redio Zanzibar.

Hakuna uhakika wa nani alimpeleka Okello Raha Leo kutangaza Mapinduzi. Wapo wanaosema ni Yusuf Himidi, wengine wanasema ni Seif Bakari aliyetoa rai atumiwe kutoa matangazo kwenye redio kwa vile sauti yake ilikuwa na lafudhi ngeni na ilikuwa ya kutisha.

Uhakika uliopo ni kwamba Okello alipotokea Raha Leo na bastola yake kiunoni, tunaambiwa Sheikh Aboud Jumbe alishtuka akauliza: “Nani huyu? Katokea wapi?”

Okello wakati huo akiwa na umri wa miaka 27 hakujulikana kabla ya Mapinduzi. Hakuwa na sifa za uongozi na wala hakuwahi kushiriki katika vuguvugu lolote la kisiasa Zanzibar.

Akijibandika cheo cha juu kabisa cha kijeshi cha Field Marshall  ni yeye aliyetangaza kwamba Serikali ya ZNP/ZPPP imepinduliwa.

Kwa hakika, kazi hiyo ya kutangaza kufanikiwa kwa Mapinduzi kwanza alipewa Ramadhan Haji, mmoja wa wanamapinduzi lakini alikataa.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply