Kilichojificha mgogoro wa Zanzibar -3
Kama tulivyoona wiki iliyopita aliyetangaza Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964 ni John Okello, nilipata simu za wasomaji wakitaka kujua huyu mtu alitoka wapi.
John Okello alikuwa akiishi Pemba tangu Juni 22, 1959 ambako alitokea Mombasa lakini alikuwa raia wa Uganda, alikuwa seremala, asiyejua Kiingereza. Ndani ya Zanzibar Okello alipata umaarufu kwa vijana ambao wengi wao walikuwa ni makuli na wachukuzi katika meli zilizoingia na kutoka bandarini Zanzibar.
Kundi la John Okello lilikutana kwa siri. Okello aliwapa matumaini ya mabadiliko watu wake hawa, wafuasi ambao walifanya kazi pamoja kwa muda mrefu, mara nyingine katika mazingira ya hatari na walikuwa tayari kufuata amri za kiongozi yeyote ambaye angeweza kuwalipa. Wao walikuwa waasi wanaotafuta makazi.
Mchafuko wa kisiasa ulikuwa ukiongezeka ndani ya Zanzibar na Pemba tangu kifo cha Sultani Khalifa katika mwaka 1960. Sultani Khalifa alitawala Zanzibar kwa karibu miaka 50, tangu mwaka 1911.
Baada ya udanganyifu mkubwa kwa majimbo ya uchaguzi na mseto katika chaguzi kuu mbili za mwaka 1961 vyama vikuu vilishindwa kujipatia wingi wa kura kwa kila kimoja. Waingereza waliondosha majeshi yao kikiwemo kikosi maalum cha Kiairishi ambacho kilikuwa kimewekwa karibu na uwanja wa gofu na mpaka wa Mji Mkongwe mapema mwaka 1963. Wakati mfalme mpya, Jemshid akipandisha bendera ya Taifa huru la Zanzibar Desemba 12, 1963, aliadhimisha uondokaji wa Gavana wa Kiingereza Zanzibar na mwisho wa ukoloni Zanzibar.
Uchaguzi mwingine uliofanyika mwishoni mwa mwaka 1963 ukiupa ushindi mdogo wa kura muungano wa vyama viwili vya ZNP (Chama cha Kizalendo Zanzibar) na ZPPP (Chama cha Watu wa Pemba na Unguja).
A.S.P (Chama cha Afro Shirazi) kilikuwa kiwe kipo katika serikali iliyo chini ya nusu ya wabunge kwa mtindo wa bunge la Kiingereza na Sultani akiwa kama ni mtawala tu lakini siyo mtawala mwenye maamuzi ya mwisho. Taifa hili la Zanzibar ambalo lilikuwa mwanachama kamili wa Jumuia ya Madola na mwanachana mpya wa Umoja wa Mataifa lilidumu kwa siku 33 tu.
Itaendelea wiki ijayo.