The House of Favourite Newspapers

Kilichompata ‘house girl’ huyu

REHEMA Ezekiel, mkazi wa Sinza- Mugabe jijini Dar ni msaidizi wa kazi za ndani (hausigeli) ambaye yamemfika mazito baada ya kutimuliwa ndani ya nyumba na mdogo wa bosi wake aliyefahamika kwa jina la Mama Rose, kisa kumdai mshahara, habari hii ni fundisho kwa wengine.

Kwa mujibu wa Rehema, alifikwa na mazito hayo baada ya kudai mshahara wake huo wa mwezi mmoja wa shilingi elfu hamsini na kujikuta hana pa kwenda kisha kubaki akirandaranda mitaani.

Tukio hilo lilijiri hivi karibuni ambapo Rehema alipewa shilingi elfu ishirini kisha kutupiwa begi lake la nguo na kuambiwa aondoke.

 

Akizungumza huku akiwa nje ya nyumba hiyo ya bosi wake maeneo hayo ya Sinza-Mugabe, Rehema aliliambia gazeti hili kuwa alitinga jijini Dar akitokea Pangani jijini Tanga kwa ajili ya kufanya kazi za ndani na amefanya kwa takriban miezi miwili na kulipwa shilingi elfu hamsini tu.

“Nilikuja hapa (Dar) kwa ajili ya kufanya kazi za ndani kwa dada mmoja anaitwa Mama Rose, lakini nina miezi miwili nyumbani kwake na tulikubaliana kila mwezi atakuwa ananilipa shilingi elfu hamsini, lakini amenilipa shilingi elfu 30 mara ya kwanza.

 

“Mimi nilipoona sipewi kile tulichokubaliana, ilibidi nimuage bosi wangu kwamba nahitaji kuondoka nirudi nyumbani kwa hiyo namuomba hela zangu zote, lakini kwa kipindi hiki yeye amesafiri nipo mdogo wake. Huyo mdogo wake alinipa shilingi elfu ishirini na kunifukuza, akiniambia niondoke.

“Nilimwambia nitaondokaje wakati bado nadai hela ya mwezi mzima? Akanipa shilingi elfu ishirini na kuniambia niondoke.

 

“Nilipomkatalia hadi nilipwe hela yangu yote ndipo akanitupia begi langu na kufunga mlango. Nilikaa uani hadi saa tisa usiku ndipo akanifungulia, nikaingia ndani kulala, akaniambia ikifika saa kumi na mbili alfajiri hataki kuniona.

“Mimi nilimwambia anipe hela zangu niondoke, lakini hakunipa hivyo ninashindwa kuondoka kwani elfu ishirini aliyonipa haiwezi ikanifikisha Pangani.

 

“Ilibidi niende Kituo cha Polisi cha Kijitonyama (Mabatini), nikaambiwa nirudi kwa mjumbe ili nimueleze tatizo langu.

“Kwa hiyo mpaka mpaka sasa sijajua nini cha kufanya kwa kuwa hii hela haitoshi hata nauli na sina pa kwenda,” alisema Rehema akiangua kilio asijue wapi pa kwenda.

Habari hii ni fundisho kwa wadada wanaotafuta kazi za ndani na kwa wazazi wanaoruhusu watoto wao waende mjini bila kujua huko waendako wataenda kuishije.

 

STORI: NEEMA ADRIAN, DAR E SALAAM

Comments are closed.