Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-16

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Dorcas alipokuwa akipiga mayowe baada ya kumuona paka mbele yake ambapo walitokea mama Thabi, mama Elisha, vijana watatu na dada mmoja ndipo mama Thabi aliyekuwa akimfahamu vizuri alimwuliza alipatwa na nini? Je, kiliendelea nini? Songa mbele…

Nikiwa mwenye hofu niliwaonesha paka ambaye bado alikuwa mbele yangu na kuwaeleza alikuwa akinizuia kupita, wakashangaa na kuniuliza paka huyo alikuwa wapi!

Kwa kuwa mnyama huyo alikuwa amesimama karibu kabisa na mama Elisha, nikawaonesha lakini hawakumuona, mzee mmoja akasema huenda malaria ilinipanda kichwani.

Niliwahakikishia kwamba sikuwa na malaria na kusisitiza kuwauliza kama ni kweli hawakumuona yule paka, jambo la ajabu ni kwamba nilipoangalia sehemu aliyokuwepo yule paka sikumuona.

“Dorcas huyo paka mbona sisi hatumuoni?” mama Elisha aliniuliza.

Kwa kuwa paka alikuwa ametoweka niliwaambia aliondoka wakabaki wameduwaa ndipo yule mzee alisema kama kweli nilimuona paka muda ule anaweza kuwa wa miujiza.

Hata hivyo, mama Elisha alimpinga kwamba hapakuwa na paka kwa sababu walipofika hawakumuona mnyama huyo, aliponiuliza tena kama kweli nilimuona paka, nilisisitiza kwamba nilimuona.

Mmoja wa wale vijana aliniuliza nilikuwa najisikiaje, nilimwambia nilikuwa mzima, akasema kama sikuwa na tatizo basi niende nyumbani kisha wakaondoka.

Baada ya wale vijana kuondoka, yule mzee aliwaambia akina mama Elisha, yule dada na mama Thabi kwamba huenda ni kweli nilitokewa na paka kwani isingekuwa rahisi katika hali ya kawaida kupiga mayowe na kusema nilimuona paka.

Mzee huyo alimuomba mama Thabi anisindikize nyumbani, nikaongozana na mama huyo kwenda nyumbani.

Kwa kuwa sikuwa na tatizo, tulipofika aliniaga na kuniambia akina mama wakirudi niwasimulie mkasa wangu nikamwambia sawa.

Mama Thabi alipoondoka, nilitoa kitoweo na vitu vingine nilivyotoka kuvinunua na kuanza mapishi.

Nyama ilipoiva niliipua na kwa kuwa sikuwa nahisi njaa, niliamua kujipumzisha kuwasubiri akina mama warejee ili tuandae chakula cha alasiri kwani walikuwa wanapenda sana kula nyumbani.

Wakati nawasubiri niliingia chumbani kwangu nikajilaza kitandani, nilipoanza kupitiwa na usingizi ghafla nilishtuka nikikabwa shingoni.

Kwa kuwa mle chumbani nilikuwa peke yangu, kila nilipojaribu kupiga mayowe ya kuomba msaada sikuweza kwani mtu huyo aliendelea kunikaba huku akisema atahakikisha ananiondoa duniani.

Mtu huyo ambaye alikuwa amejitanda nguo nyeusi, kila nilipojaribu kujinasua aliendelea kunikaba huku akikwepesha sura yake nisimtambue, nikaanza kusema; ‘Mungu wangu niokoe, Mungu wangu niokoe ndipo  aliniachia na kutoa msonyo wa nguvu na kuniambia nilikuwa nina bahati.

Alipotoa kauli hiyo akatoweka kimuujiza, lakini nikapata wazo la kuchungulia dirishani. Nilipofanya hivyo nilimuona mama mmoja  aliyekuwa kanipa mgongo akitembea.

Mama huyo aliyekuwa amejifunga nguo nyeusi, kwa muonekano wake wa nyuma na tembea yake alifanana na yule mama tuliyekuwa tukimhisi alikuwa akituchezea kichawi.

Nilimwangalia mpaka alipotoweka kwa kukata kona na kuingia kwenye uchochoro ndipo nilitoka pale dirishani na kwenda kukaa kitandani, nikashusha pumzi kwa nguvu.

Baada ya kufanya hivyo, nikaanza kulia na kukohoa nikiwa nimelala kifudifudi, nikiwa katika hali hiyo nilishangaa nimeshikwa begani na mama mkubwa ambaye sikumsikia alipoingia chumbani.

“Dorcas umepatwa na nini mwanangu?” Mama mkubwa alimwuliza.

Nikiwa katika hali hiyo, mama aliingia akapigwa butwaa kuniona nikilia na baada ya kunibembeleza kwa muda nilinyamaza.

Baada ya kuwasimulia kilichonitokea, mama alianza kulia na kusema kama baba yangu angekuwepo nisingepatwa na mambo ya ajabu yaliyokuwa yakinitokea, nami nikaanza kulia.

Je, kilifuatia nini? Usikose mkasa huu wa kusisimua wiki ijayo katika gazeti hilihili ili ujue undani wake.

Loading...

Toa comment