Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-17
Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Dorcas alipomaliza kuwasimulia mama zake juu ya mkasa uliomkuta wa kutokewa na paka na yule mama aliyemtokea kichawi ndipo mama yake mzazi akaanza kulia na kusema kama baba yake angekuwepo yote yaliyokuwa yakimtokea yasingetokea. Je, kilifuatia nini? Endelea…
Kufuatia mama kulia, mama mkubwa alimsihi na kumwambia hata kama baba angekuwepo mambo hayo yangetokea kwa sababu hiyo ndiyo ilikuwa tabia ya wachawi.
Licha ya mama mkubwa kutoa kauli hiyo, mama alisisitiza kwamba anaamini baba asingekubali nichezewe namna ile akaendelea kulia jambo lililonifanya nami niungane naye.
Mama mkubwa alifanya kazi ya ziada kutunyamazisha, tukiwa tumetulia alimwambia mama Jumamosi twende tena kwa yule mganga wa Songwe tukamwelezee kilichotokea.
“Kwa hali ilivyo lazima twende tukamuone,” mama alimwambia mama mkubwa.
Baada ya kupata chakula, niliondoka na akina mama kwenda kwenye biashara zao ambapo tulirejea nyumbani saa 12 jioni, tuliendelea na mambo mengine kisha tulilala.
Usiku wa siku hiyo tulilala vizuri hadi kulipokucha ambapo nilijiandaa na kwenda shuleni, nikiwa shuleni baadhi ya walimu waliniuliza kuhusu maendeleo yangu niliwaambia yalikuwa mazuri.
Alasiri niliporejea nyumbani, nilimkuta mama akiwa amejilaza kitandani akilalamika maumivu ya tumbo na juu ya meza ndogo palikuwa na vidonge.
Nilipouliza alianza kusumbuliwa na tumbo muda gani, mama mkubwa alinifahamisha kwamba lilianza kumuuma ghafla wakiwa sokoni kwenye biashara zao.
Kitendo cha mama kuumwa kilinikosesha raha, licha ya mara kadhaa kupenda kwenda kucheza na wenzangu baada ya kutoka shuleni, siku hiyo sikutoka kabisa.
Mama alisumbuliwa na tumbo hilo kwa siku mbili mfululizo, ilipofika Jumamosi tulikwenda kwa yule mganga, alipoangalia kupitia zana zake alibaini mama alitupiwa kitu tumboni.
Mganga huyo alitufahamisha kwamba yule mama mchawi ndiye aliyefanya hivyo na kuongeza kwamba bila ya kutuchanjia dawa mimi au mama tungekuwa tumepoteza maisha.
Aliongeza kuwa siku niliyotokewa na paka alikuwa ni yeye na alipanga kunimaliza lakini alishindwa na baadaye alinifuata nyumbani nikiwa nimelala lakini pia alishindwa kunidhuru.
Mganga huyo aliwauliza akina mama amfanye nini mchawi yule ambaye alipanga kutuletea madhara makubwa, mama mkubwa aliomba kama anaweza ammalize kabisa lakini mama alipinga.
Mganga hakuwa na la kufanya, alimpatia mama dawa ambayo alisema akinywa atatapika na kitu alichorushiwa kitatoka na atakuwa mzima.
Baada ya kufika nyumbani, mama alichemsha dawa aliyopewa ilipopoa alikunywa kikombe kizima, hakumaliza dakika tano alianza kuharisha na kutapika mpaka akaishiwa nguvu.
Alipomaliza mama mkubwa alimpikia uji, alipokunywa alianza kutapika na kuanza kusema shingoni kulikuwa na kitu kilimkaba akaanza kutapika tena ndipo kilitoka kitambaa cheusi kilichofungwa.
Mama mkubwa alipokifungua, wote tulipigwa butwaa kuona ndani mkiwa na mchele, maharage, unga na njugu mawe, jambo hilo lilitushangaza na kuamini kweli duniani kulikuwa na uchawi.
Mama mkubwa alichukua zile nafaka na kitambaa na kwenda kuvichoma moto nje, tangu hapo mama aliacha kulalamika kupata maumivu zaidi kilichomkabili ni mwili kuishiwa nguvu.
Kama alivyofanya awali alimpikia uji akaweka limao, mama alipokunywa hakutapika tena, siku iliyofuata asubuhi na mapema alituambia kwamba aliota ndoto kwamba baba yangu alikuwa Nkasi Rukwa, hivyo alitaka kwenda kumtafuta kwani aliumia sana mimi kuendelea kuteseka bila kumuona baba yangu.
Licha ya mama mkubwa kumshauri kwamba ndoto zilikuwa ndoto asiende lakini mama alisema atakwenda Nkasi kumtafuta baba.
Je, kilifuatia nini? Usikose mkasa huu wa kusisimua wiki ijayo katika gazeti hilihili ili ujue undani wake.