The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-18

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale mama yake Dorcas alipoamka asubuhi na kuwaeleza mama mkubwa na mwanaye kwamba aliota ndoto kwamba baba Dorcas alikuwa Nkasi hivyo alipanga kwenda kumtafuta jambo lililopingwa na mama mkubwa kwamba halikuwa halisi bali ni ndoto tu.

Je, kilifuatia nini?

Songa mbele…

Kwa kuwa alikuwa na fedha, baada ya maandalizi ya siku mbili aliondoka kuelekea Nkasi na kuniacha na mama mkubwa, tangu alipoondoka sikupatwa na tatizo lolote.

Wiki mbili baadaye, tulipata taarifa ya kuhuzunisha kuhusu kifo cha mama kilichotokana na ajali ya gali, siku hiyo nililia sana, kwa upande wa mama mkubwa aliishia kuzungumza peke yake jinsi alivyompoteza mtu muhimu maishani mwake.

Ukweli sitakaa nisahau siku hiyo ambayo kila ninapoikumbuka huwa nalia, baada ya taarifa hiyo tuliondoka na mama mkubwa kwenda Mpanda kwenye msiba.

Nilipofika nilipokelewa vizuri na ukoo wa mama ambao siyo mkubwa, baada ya kumaliza msiba wiki moja baadaye mama mkubwa aliwaaga tayari kwa kurejea Mbeya.

Hata hivyo, bibi na mjomba wangu mmoja walimuomba mama mkubwa aniache kule kijijini lakini alikataa na kuwaeleza kwamba kwa kuwa rafiki yake alifariki dunia yeye atanilea na kunisomesha hivyo wasiwe na wasiwasi.

Baada ya kuwaeleza hivyo, hawakuwa na kipingamizi ndipo tuliondoka na mama mkubwa tukarudi Mbeya kuendelea na maisha ya upweke.

Siku za mwanzo nilikuwa katika wakati mgumu sana lakini kwa kuwa binadamu tunasahau, kadiri siku zilivyosonga mbele nilizoea na kumchukulia mama mkubwa kama mama yangu mzazi.

Wakati huo nilikuwa sielewi kama katika maisha yangu ningekumbwa na masaibu ambayo yangenifanya niichukie dunia na kutamani kumfuata mama yangu.

Baada ya kurejea kutoka msibani, nilikaa mwezi mmoja bila kupata tatizo lolote, siku moja usiku nikiwa nimelala nilishtuka usingizini nikakiona kimvuli cha mtu kikiwa kimesimama pembeni ya mlango.

Kutokana na uwoga niliokuwanao nikaamua kumuita mama mkubwa lakini katika hali ambayo mpaka leo nashindwa kuielewa sauti haikutoka, ghafla nikajikuta nakabwa shingoni huku mtu aliyenikaba akisema nitamtambua.

Kila nilipojitahidi kumuita mama nilishindwa ndipo nikaanza kumuomba Mungu kimoyomoyo kwa kusema; Mungu nisaidie, Mungu nisaidie, niliendelea kusema hivyo ndipo yule mtu akaniacha na kutoa msonyo.

“Leo ningekuulia mbali mweu wewe na ipo siku nitafanikiwa, eti unamuita Mungu wako, nani ambaye hana Mungu?” mtu huyo alitoa  kauli hiyo na kutoweka.

Baada ya kutoweka, nilimuita mama mkubwa ambaye alikuja chumbani kwangu na kunikuta nalia, aliponiuliza sababu nilimweleza kila kitu, nikahamia chumbani kwake.

Kulipokucha alinifahamisha kwamba alivumilia sana vitimbi vilivyokuwa vikitokea kwenye ile nyumba na kusema kodi yake ikiisha angetafuta nyumba sehemu nyingine.

Nilimshukuru sana kwa uamuzi huo, baada ya kujiandaa nilikwenda shuleni ambapo muda mwingi nilikuwa namuwaza mama na kujiuliza hivi ni lini nitaacha kusumbuliwa na wachawi ili nami nilale kwa amani!

Nakumbuka siku ya Jumamosi nikiwa nyumbani alifika yule mama rafiki yake mama mkubwa wa Shinyanga, mama mkubwa alipomkea kwa furaha.

Baada ya salamu, alimwuliza mama alikuwa wapi, badala ya kumjibu mama mkubwa alinitazama usoni kisha akamtazama yule mgeni na kuishia kuguna.

Mgeni alipomuuliza sababu za kuguna alimwambia basi tu, alipotoa kauli hiyo nikajikuta natiririkwa na machozi na kuanza kujifuta kwa kutumia viganja.

Kitendo hicho kilimshtua yule mama akamwuliza sababu za kulia, akamfahamisha kwamba mama alifariki dunia na kulia kwangu kulisababishwa na kumkumbusha kifo chake.

Leave A Reply