The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-20

0

sad mood

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale mama mkubwa alipomuuliza Dorcas kama alikuwa tayari kwenda kwa rafiki yake wa Shinyanga. Kutokana na akili za kitoto, Dorcas akakubali ndipo alimweleza asubiri mpaka atakapowasiliana na mjomba wake. Je, kilifuatia nini? Songa mbele…

Wiki moja tangu tulipozungumza na mama mkubwa kuhusu safari ya kwenda Shinyanga, nilianza kuugua tumbo ambalo halikuwa la kawaida.

Kufuatia maradhi hayo, nilipelekwa hospitali ambapo nilifanyiwa vipimo jambo la kushangaza sikupata nafuu.

Ugonjwa huo ulikwenda sambamba na kuweweseka usiku na kupiga mayowe jambo lililomchanganya sana mama mkubwa ambaye aliamua kunipeleka kwa yule mganga wa Songwe.

Aliamua kunipeleka huko kwa sababu alikuwa anaamini sana mambo ya kishirikina, tulipofika kama kawaida yule mganga alituambia kwamba ugonjwa wangu ulikuwa wa kurogwa.

Hata hivyo, kabla ya kuendelea kunitibu alimuuliza mama mkubwa mbona mama hakuwepo, swali hilo lilisababisha ukimya wa sekunde kadhaa ndipo alimuomba samahani kwa kutomfahamisha.

Mganga huyo alipouliza kufahamishwa kitu gani, mama mkubwa alimweleza kwamba mama alikwishatangulia mbele za haki, mganga akashtuka.

Kwa kuwa nilikuwa nimekumbushwa kifo cha mama, nilijikuta natiririkwa na machozi ndipo mama na yule mganga wakaanza kunibembeleza ninyamaze.

Niliponyamaza, mganga aliyekuwa ameguswa sana na kifo cha mama alimwuliza mama mkubwa kilichomsibu mama, akamwelezea kila kitu lakini cha kushangaza akasema kifo chake hakikuwa bure.

“Kwa maelezo yako kuhusu kifo cha mwenzako na jinsi huyu binti anavyoumwa siyo bure, ngoja niwaulize wakubwa wangu (mizimu),” Dorcas alimkariri yule mganga.

Baada ya kutoa kauli hiyo, mama mkubwa alimuunga mkono na kusema ndiyo maana alifunga safari kumfuata ndipo yule mganga alivaa zana zake za kazi na kukaa sehemu aliyokuwa akifanyia kazi yake.

Akiwa hapo alishika tunguri, usinga akawa anazungumza maneno ambayo hatukuyaelewa kisha akatikisa kichwa na kusema kwamba yule mbaya wetu alipanga kutumaliza.

Aliongeza kuwa, hata kifo cha mama kilisababishwa na yule mama mbaya wetu kwa kushirikiana na wenzake aliowaalika kutoka mbali kisha akasema apewe ruhusa ya kumuadhibu.

Kwa kuwa mama aliyekuwa akipinga kulipa kisasi hakuwepo, mama mkubwa alikubali mganga akasema mtu anayefikia hatua ya kuua watu bila sababu naye anapaswa kuuawa bila huruma.

Baada ya mganga kutoa kauli hiyo alisema kwa kuwa nilifika kwake angenipatia dawa ambayo ingeniponya ndipo alivua nguo za kazi akamuita mkewe aliyekuwa akianika mbona ya majani iliyokuwa imetwangwa.

Alipofika alimpa maelekezo ya kutengeneza dawa kisha aliomba amwite msaidizi wake, kijana huyo alipofika alimwambia amchinje kuku mweusi ambaye angechanganywa na dawa.

Baada ya saa moja dawa iliyochanganywa kwenye supu ya kuku ililetwa kwenye bakuli kubwa, mganga huyo alimimina supu na baadhi ya kitoweo kwenye bakuli tatu.

Alipofanya hivyo, bakuli moja alimpatia mama mkubwa, lingine mimi na iliyobaki ilikuwa yake akatuambia dawa ilikuwa tayari hivyo tunywe, naye akawa anakunywa iliyokuwa kwenye bakuli lake.

Tulipomaliza, mkewe alikuja na dawa nyingine iliyokuwa kwenye chupa akamkambidhi mumewe ambaye aliniambia ninywe kwa muda wa siku tatu mara tatu.

Baada ya kutupa maelezo hayo, alitufahamisha kwamba zisingepita siku nyingi tungepata taarifa kuhusiana na mchawi aliyekuwa akitusumbua ambaye alipanga pia kuniondoa duniani.

Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, nicheki kupitia namba hiyo hapo juu.

Leave A Reply