The House of Favourite Newspapers
gunners X

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-22

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale mama mkubwa wa Dorcas na rafiki yake walipokubaliana Dorcas aende Shinganga ndipo yule mama wa Shinyanga alifurahi na kumweleza shoga yake kwamba anakwenda Malawi akitoka huko akute amechukua uhamisho shuleni. Je, kilifuatia nini? Songa mbele…

Kutokana mara kwa mara yule mama kupendelea kufikia hotelini, kabla ya kwenda kulala mjini alimpatia mama shilingi 15, 000 kisha alituaga akaelekea mjini.

Siku iliyofuata alikwenda Malawi na baada ya kupita siku sita alirejea na kukuta mama kishachukua uhamisho, alifurahi sana na siku iliyofuata alfajiri tuliondoka Mbeya kuelekea jijini Dar es Salaam alikotueleza alifuata mzigo wa biashara.

Tulipofika jijini Dar es Salaam mazingira yalikuwa tofauti na Mbeya nikawa nashangaa kila nilichokiona wakiwemo watu wengi, magari na uwingi wa nyumba.

Ingawa mama huyo alinifahamisha kuwa Dar alikuwa na ndugu zake, hatukufikia kwa mtu badala yake tulifikia katika hoteli moja iliyopo karibu na stendi ya mabasi yaendayo mikoani.

Kutokana na uchovu baada ya kuoga na kula tulilala na kesho yake asubuhi tulikwenda Kariakoo, huko nilizidi kulishangaa Jiji la Dar jinsi lilivyokuwa na watu wengi, majumba ya ghorofa nk.

Kabla ya kuanza kufanya manunuzi, tulikwenda katika benki moja ambapo mama huyo alichukua fedha tukaanza kuingia madukani ambako alinunua nguo za akina mama, watoto, mashuka na mablanketi kadhaa nami alininunulia viatu, nguo za ndani na magauni matatu.

Baada ya kuzunguka sana tukiwa na mizigo yetu tuliingia katika hoteli moja tukala kisha alikodi gari tukarudi hotelini Ubungo kwa ajili ya kupumzika, jioni tulikwenda kwa ndugu yake aliyekuwa akiishi Kimara.

Tulikaa huko hadi usiku na baada ya kula tulirudi hotelini ambapo tulilala na alfajiri tuliondoka Dar kuelekea Shinyanga ambako tulifika saa tatu na nusu usiku.

Tulipofika stendi tulipokelewa na kijana mmoja aliyekuwa na gari dogo, baada ya salamu alipakiza mizigo yote ndani ya gari tukaelekea nyumbani kwa mama huyo eneo la Majengo

Siku hiyo nilifurahi sana kubadili eneo la kuishi kwani sikuwahi kufika Shinyanga zaidi ya kuisikia tu, wenyeji wetu nao walifurahi sana kutuona.

Mama alinitambulisha kwa dada mmoja niliyemkuta pale nyumbani, msichana mmoja ambaye alisema alikuwa mwanaye aliyeitwa Emmy na kijana ambaye alisema alikuwa ni mtoto wa kaka yake.

Alinitambulisha pia kwa wenyeji wangu hao kisha alinifahamisha  kwamba mwanaye aitwaye Evance alikuwa masomoni katika chuo kikuu kimoja kilichopo jijini Dar.

Kama unavyofahamu mtu anapokuwa mgeni anavyokuwa mgeni kwa kila jambo, nami ilinichukua siku kadhaa kuzoeana na wenyeji wangu na mazingira.

Baada ya kukaa nyumbani siku nne, ndipo mama huyo ambaye nilimchukulia kama mama yangu mzazi alinipeleka shule iitwayo Town School bila kujua huko Shinyanga ndiko ungekuwa mwanzo wa kuharibikiwa kimaisha.

Nilifurahi sana kuhamia katika shule hiyo kwani niliweza kupata marafiki ambao walinipenda, kutokana na uwezo wangu mzuri darasani hata walimu hasa wa darasa letu walikuwa wakinipenda pia.

Maisha yaliendelea bila kujua masaibu yaliyokuwa mbele yangu lakini kama ningejua wala nisingekubali kuhamia Shinyanga, kwa ujumla nyumbani kwa yule mama sikupungukiwa na kitu.

Ninaposema sikupungukiwa na kitu namaanisha alikuwa akininunulia nguo, viatu na kwa upande wa chakula nilikula kila kilicholiwa pale nyumbani tofauti na familia zingine zinavyofanya hasa kwa watu ambao siyo wanafamilia wa damu.

Kwa kuwa nilihamia Shinyanga Oktoba ilipofika Desemba mwanzoni tulifunga shuleni kwa ajili ya mapumziko ya Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Wakati huo mama wa Shinganya alikwenda Mbeya mara mbili ambapo alikuwa akinieleza kuwa mama mkubwa alikuwa akiendelea vizuri na alikuwa akinisalimia.

Kufuatia kufunga shule, Evance mtoto wa kiume pekee wa mama huyo alifika na kunikuta ambapo mama alimtambulisha.

“Evance huyu ndiye Dorcas niliyekuwa nakupa habari zake mara kwa mara, Dorcas huyu ndiye kaka yako Evance niliyekwambia anasoma jijini Dar es Salaam,” mama alinitambulisha kwa mwanaye.

Baada ya kutambulishwa, Evance ambaye wakati huo alikuwa mwaka wa kwanza chuoni kwao alinikaribisha kwa furaha na kusema alifurahi kupata dada mwingine kwenye familia yao.

Evance aliyeambiwa kwamba nilikuwa nina maendeleo mazuri shuleni alinipongeza na kusema anapenda sana watu wanaopenda kujisomea na kufanya vizuri shuleni kama mimi.

Nilimshukuru ndipo aliniambia kwa kipindi ambacho atakuwa pale nyumbani atautumia muda huo kunifundisha masomo mbalimbali, nilifurahi sana kusikia hivyo.

Maisha yaliendelea huku nikiwa na furaha na kaka Evance ambaye nilimchukulia kama kaka yangu wa damu akiwa karibu nami kwa kila jambo hususan kunifundisha masomo mbalimbali.

Likizo ilikuwa nzuri sana na Januari tulifungua shule ambapo niliingia rasmi darasa la saba, nilifurahia sana hatua hiyo na wiki mbili baadaye kaka Evance alikwenda kuendelea na chuo Dar.

Nakumbuka baada ya kufungua shule sikukaa muda mrefu nilivunja ungo, mama alinifundisha namna nilivyopaswa kuwa msafi na mambo mengine yanayotuhusu wanawake tukiwa katika hedhi.

Kama kawaida, aliendelea kunijali na kuhakikisha kila mwezi ananinunulia vifaa vinavyohitajika kipindi cha hedhi, yaani alinijali mno hadi nilijisikia raha!

Nikiwa katika kipindi hicho nilianza kunawiri na kuonekana mrembo na kuwa na shepu nzuri ya kike ambapo vijana wengi walikuwa wakinisifia kwamba nilikuwa mzuri.

Kwa kuelewa jambo hilo, mama aliniketisha chini na kunisihi niwe makini na wavulana wasije kunirubuni na kuanza kushiriki mambo ya mapenzi.

Hakuishia hapo, alinipa mfano wa wasichana ambao walipata mimba wakiwa shuleni na kuharibu maisha yao, nilimshukuru mama kwa ‘darasa’ hilo.

Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply