The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-31

0

 

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Dorcas aliyewasili Shinyanga mjini akitokea kijijini alipokutana na watu waliokuwa wakimfahamu na kumwuliza kuhusiana na mabadiliko yake ya afya ambapo alishindwa kuwajibu na kuanza kulia. Je, kilifuatia nini? Songa mbele na mkasa huu wa kuhuzunisha…

Dorcas umepatwa na tatizo gani linalokufanya ulie?” dada aitwaye Jasmini alimwuliza.

“Nyie niacheni tu,” Dorcas aliwajibu.

Licha ya kuwaambia wamuache, Jasmini aliyehisi huenda Dorcas alikuwa na tatizo kubwa akazidi kumbana ili amwambie kilichomliza ndipo aliwadanganya kwamba alimkumbuka marehemu mama yake.

“Ooh jamani kumbe umefiwa na mama yako?” Jasmini alimwuliza.

Dorcas aliwajibu ndiyo ndipo wakazidi kumpa pole na kumwambia alikuwa na sababu ya kudhoofu kwani kufiwa na mama lilikuwa tatizo kubwa.

“Ndiyo hivyo, yaani kila ninapomkumbuka naumia sana,” Dorcas aliwaambia bila kujua kama kilichomliza ni kitendo cha kikatili alichofanyiwa na Evance pamoja na mama yake aliyemtelekeza kijijini.

Kwa kuwa wakati nazungumza na dada Jasmini na mwenzake ambaye sikumfahamu tulikuwa tumesimama, niliagana nao na kuelekea nyumbani.

Nilipokaribia kufika, rafiki zangu  Ester na Kalunde waliponiona walinikimbilia wakanilaki kwa furaha kisha kunipokea begi, tukaongozana kwenda nyumbani.

Marafiki zangu hao, kama alivyofanya dada Jasmini, waliniuliza kama nilikuwa naumwa kwa sababu nilikuwa nimekonda na kubadilika tofauti na nilivyokuwa awali kabla sijaondoka.

Pia walinilaumu kufuatia kuondoka bila kuwaaga, niliwaambia niliondoka ghafla na kwamba hali ya hewa ya nilikokuwa ilinikataa kwani mara kwa mara nilikuwa naugua malaria.

Tulipofika nyumbani, Ester ndiye alibisha hodi na hatukukaa muda mrefu Emmy alifungua mlango, aliponiona alinirukia kwa furaha!

Emmy ambaye naye hakufahamu jambo lililoniondoa pale nyumbani alifurahi na kunieleza alikuwa kanimisi sana, alibeba begi langu na kulipeleka chumbani.

Tukiwa tumeketi sebuleni nilimuuliza alikokuwa mama akaniambia alikwenda Mwanza kwenye shughuli zake za biashara, nilipomuuliza pia kuhusu mama mdogo akaniambia alikwenda Tabora kwa mzazi mwenzake.

Emmy alinifahamisha kwamba pale nyumbani alibaki na mama yake mkubwa, Edina na dada wa kazi ambaye wakati huo alikuwa ametoka.

Wakati tukizungumza, alikuja mama mmoja ambaye sikumfahamu kutokea kwenye korido ya kwenda vyumbani, mimi na akina Ester tulimwamkia.

“Dada Dorcas huyu hapa ni mama mkubwa anaishi Bariadi, mama mkubwa huyu ni dada Dorcas amefika muda mfupi uliopita,” Emmy alitoa utambulisho.

Mama huyo alinipa pole kwa safari na kunikaribisha lakini nilihisi kama alitaka kuuliza jambo fulani akasita, baada ya muda akina Ester waliaga.

Kutokana na uchovu wa safari sikuwasindikiza badala yake Emmy alifanya zoezi hilo, tukiwa tumebaki na mama mkubwa aliniuliza mtoto wangu alikuwa wapi!

Kufuatia swali hilo nilijua alikuwa kaelezwa kila kitu na mama, swali lake lilinikumbusha mwanangu na ukatili niliofanyiwa, nikaanza kulia.

Mama mkubwa aliponiuliza sababu za kulia, nilimfahamisha kuwa mwanangu alifariki dunia siku chache zilizopita, taarifa hiyo ilimhuzunisha akanipa pole.

Nilimuuliza kama hawakupata taarifa ya msiba, akaniambia hakufahamu chochote, nikamwambia hivyo ndivyo ilivyotokea, akanipa pole tena.

Wakati tunaendelea kuzungumza na mama huyo, Emmy alifika ndipo tulisitisha maongezi yaliyohusiana na kifo cha mwanangu, Emmy aliyekuwa akinipenda aliniandalia maji ya kuoga nikaenda chumbani nikabadili nguo na kwenda bafuni.

Niliporejea sebuleni, nilikuta kaniandalia chakula na wakati napata mlo dada wa kazi alirejea tulisabahiana na Emmy akanitambulisha kwake.

Usiku nikiwa chumbani na Emmy, aliniuliza mbona nilirejea nyumbani kabla ya shule kufungwa, nilimdanganya kwamba nilikuwa naumwa hivyo niliomba ruhusa, akanipa pole.

Baada ya kupiga stori za hapa na pale, Emmy alipitiwa na usingizi lakini kwa upande wangu sikuweza kulala kabisa badala yake nilisongwa na mawazo kuhusiana na kitendo nilichofanyiwa na mama pamoja na Evance.

Kutokana na hali hiyo, nikapata hasira na kuchukua uamuzi mzito.

Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, nicheki kupitia namba hiyo hapo juu.

Leave A Reply