Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-32

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale dada Dorcas aliposhindwa kulala kufuatia kusongwa na mawazo kutokana na vitendo alivyofanyiwa na mama wa Shinyanga pamoja na kijana wake Evance, ambapo alipata hasira na kuchukua uamuzi mzito. Je, ni uamuzi gani huo? Songa mbele na kisa hiki cha kuhuzunisha…

Licha ya kwamba sikuwa na fedha, nilipanga kukicha kuondoka Shinyanga na kwenda Mbeya kwa mama mkubwa ambaye niliamini ndiye aliyechukua nafasi ya marehemu mama.

Usiku huo Emmy akiwa amelala, nilikumbuka mama alikuwa akipenda kumuachia fedha za kutosha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na dharura nyingine, nikaamka na kufungua kabati.

Baada ya kufanya hivyo, niliiona pochi ambayo Emmy alikuwa akihifadhia vitu nikahisi ilikuwa na fedha alizoachiwa na mama, nilipoifungua nikaona ilikuwa na noti za shilingi elfu kumi ambazo sikujua idadi yake.

Kwa kuwa lengo langu lilikuwa kuchukua kiasi cha fedha kwa ajili ya nauli ya kwenda Mbeya, nilizihesabu na kubaini zilikuwa shilingi hamsini na nne elfu, nikachukua elfu thelathini.

Kiasi hicho cha fedha niliamini kingenifikisha Mbeya bila matatizo, sikupenda kuchukua fedha zote kuhofia ningewapa usumbufu wa kukosa fedha za matumizi wakati sikujua mama angerudi lini.

Baada ya kufanya hivyo, nilizihifadhi kwenye moja ya mifuko ya siketi yangu kisha nilichukua karatasi na kuandika ujumbe ambao hadi leo naukumbuka vizuri.
Ujumbe huo niliandika maneno haya: Emmy, mimi Dorcas siyo mwizi na sitakuja kufanya kitendo hicho katika maisha yangu hata kama nitakumbana na wakati mgumu kiasi gani.

Kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wangu nimefungua kabati na kukuta pochi yako ambayo ndani ilikuwa na shilingi hamsini na nne elfu, nimechukua shilingi elfu thelathini.

Najua nitakuwa nimeharibu bajeti yenu wakati huu mama akiwa hayupo lakini naomba mnisamehe kwa sababu sina jinsi nimeamua kuchukua fedha hizo ili nifanye nauli ya kwenda kwa mama mkubwa Mbeya.

Naomba Mungu unisamehe kwa kosa nililofanya kwa sababu sina jinsi, naomba mbaki salama na kwa amani kama Mungu akipenda tutaonana na asipopenda ipo siku tutaonana mbinguni, nakupenda sana Emmy kuliko mama na Evance.

Niombee nifike salama huko niendako, mimi Dorcas.
Nilipoandika ujumbe huo niliuweka ndani ya pochi niliyochukua zile fedha, nikaweka magauni yangu mawili ndani ya begi nikapanda kitandani kusubiri kuche ili nianze safari.

Nikiwa macho, Emmy alijitikisa nikajifanya nakoroma ili asijue kama tangu nilipopanda kitandani sikupata usingizi, akajigeuza na kuangalia ukutani na kuendelea kuuchapa usingizi.

Alfajiri na mapema wote wakiwa wamelala, niliamka nikaoga kisha nikachukua begi langu, nikafungua mlango wa nyumba kubwa nikatoka kisha nikaufunga kwa funguo na kuziingiza ndani kupitia uwazi wa chini ya mlango.

Nilipofanya hivyo, nikafungua geti la kutokea nje kwa uangalifu bila kushtukiwa na kulifunga nikashika njia ya kwenda stendi, kwa kuwa bado kulikuwa na giza nilikuwa na hofu ya kukutana na vibaka.

Nikiwa natembea nikawa namuomba Mungu anipe ulinzi ili niweze kufika salama kwani sikutaka kabisa kuendelea kuishi kwa mama ambaye hakuwa na upendo kwangu.
Wakati nikitembea ghafla nikasikia kengele ya baiskeli, ile nageuka nyuma ikasimama pembeni yangu, moyo ukapiga pa!

Jamaa aliyekuwa akiendesha, kwa sauti nzito akanisalimia kwa Kiswahili chenye lafundhi ya Kisukuma; “Wewe msichana hujambo?”

Huku nikumuomba Mungu anilinde nikaitikia salamu yake na kumwamkia, akasema marahaba kisha akashuka kabisa kwenye baiskeli ambayo nyuma alifunga kiroba na kuchomeka panga kwenye mkanda wa kaptura kubwa aliyovaa.

“Unatoka wapi na unakwenda wapi usiku wote huu?” Dorcas anasema yule bwana alimwuliza.Nilimweleza nilikuwa natoka nyumbani naenda kupanda basi kwani nilikuwa nasafiri, akaniuliza nilikuwa natoka nyumbani wapi, nikamwelekeza mtaa ambao ulipakana na alioishi mama.

Nilipomweleza hivyo akasema sawa na kuniuliza kama nilikuwa nasoma, nikamjibu ndiyo na kumdanganya kwamba nilikuwa naenda Mbeya.
Nilipomwambia hivyo, alichomoa panga na kunikazia macho.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo.

Loading...

Toa comment