The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-33

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Dorcas alipomwambia yule bwana aliyekuwa akiendesha baiskeli kwamba alikuwa akienda Mbeya msibani ndipo jamaa huyo akachomoa panga alilochomeka kwenye mkanda.

Je, kilifuatia nini?

Songa mbele…

Alipochomoa panga, akaliangalia na kulirudisha kwenye hala kisha akaniuliza nilikuwa naenda kwenye msiba wa nani, kwa hofu niliyokuwanayo awali kwamba jamaa huyo alitaka kunidhuru nilivuta pumzi na kuzishusha kwa nguvu.

Japo mama alifariki dunia muda mrefu nilimwambia msiba wa mama, alisikitika sana akachukua begi langu na kulifunga juu ya kiroba kilichokuwa nyuma ya baiskeli yake.

Alipohakikisha alilifunga vizuri akaniambia nipande kwenye bomba la baiskeli kisha nikashika usukani akaisuma kama mita mbili, akadandia na kuanza kuendesha.

Njiani, alinipa pole tena kwa msiba na kuniuliza mbona nilikuwa nasafari peke yangu, nikamdanganya kwamba ndugu zangu wengine walitangulia.

Aliendesha baiskeli kwa kasi hadi sehemu tuliyokuwa tukisubiria magari, kutokana na kunionea huruma, yule bwana hakuondoka mpaka lilipokuja gari aina ya Toyota Land Cruiser ambapo dereva alisema anakwenda Nzega.

Kwa kuwa nilielewa kama ningechelewa kupanda basi huenda Emmy angeamka na kukuta ule ujumbe na kuamua kunifuata, nilipanda gari hilo ambalo ndani kulikuwa na wanawake wawili, mmoja wa makamo, kijana wa miaka 15 hivi, mtoto na dereva.

Nilijua huko mbele ningeunganisha na magari ya kwenda Mbeya, yule bwana aliyenipa lifti ya baiskeli kabla ya kuniaga alinipatia shilingi elfu tatu na kunitakia safari njema ndipo gari likaanza safari.

Gari likiwa limeanza kushika kasi, mama aliyekuwa na mtoto akanisalimia kwa kusema; “Hujambo binti!”

Nikaitikia salamu yake na kumpa heshima yake akasema marahaba ndipo nikakumbuka kwamba wakati napanda garini hatukusalimiana.

Tukasalimiana wote na kuendelea na safari, hatukutembea umbali mrefu, yule mama akaniuliza nilikuwa nakwenda wapi, nikamwambia akasema wao walikuwa wakienda jijini Dar es Salaam lakini watasimama Nzega kwa siku moja kisha kuendelea na safari.

Nilimwambia nikifika Nzega nitaunganisha safari yangu na magari yanayokwenda Dodoma kisha huko ningepanda la Mbeya, akasema sawa.

Kama unavyojua watu mnaposafiri pamoja huzungumza mambo mbalimbali, yule mama aliniuliza jina langu na Shinyanga nilitoka kwa nani.

Aliponiuliza hivyo, sikumjibu kwa wakati akaniuliza mbona nilionekana sikuwa sawa nikamwambia sikuwa na tatizo, akanibishia na kusema alikuwa mtu mzima hivyo nisingeweza kumdanganya na kusisitiza kwa alivyoniona kuna jambo lilinitatiza.

Alipotoa kauli hiyo, dada aliyekuwemo kwenye lile gari akaniambia kama nilikuwa nina tatizo niwaambie kwa sababu kwa wakati ule nilikuwa kama ndugu yao na hata kama lingetokea tatizo wao ndiyo wangenipatia msaada.

Kama vile waliambiana, dereva naye aliniambia kama nilikuwa na tatizo niwaeleze, awali nilitaka kuwaficha lakini nilisikia sauti ikiniambia niwaeleze kila kitu kilichonitokea.

Niliwafahamisha kwamba kuna mambo yalinitatiza ndiyo yaliyonifanya niwe safarini kwenda Mbeya kwa mama mkubwa, yule mama akaniuliza ni mambo gani, nikawaeleza waelewe tu hivyo nilivyowaambia.

Yule mama na dada walibaini niliwaficha kitu wakanibana kwamba niwaeleze, nilipokumbuka mambo waliyonifanyia mama na Evance nikajikuta natiririkwa na machozi.

Jambo hilo liliwapa wakati mgumu ndipo wakaanza kunibembeleza ninyamaze na kuwasimulia kila kitu, nikaamua kuwaeleza mkasa wangu mwanzo hadi mwisho.

Nilipofika mwisho, yule mama alishindwa kujizuia kulia, yule dada akawa mpole na kuniuliza kama yote niliyowaeleza yalikuwa kweli, nikawaambia yalikuwa kweli, wakasikitika sana.

Yule kijana aliyekuwemo kwenye lile gari alisema mama wa Shinyanga pamoja na Evance walitakiwa kushtakiwa ili sheria ichukue mkondo wake, nikawaambia sikuwa na mpango huo Mungu angenilipia.

Wote walimuunga mkono yule kijana kwamba nikafungue mashtaka dhidi ya mama na Evance, nikawaambia niliwasamehe na sikuwa tayari kuwashtaki nikaanza kulia tena.

Je, nini kilimfanya Dorcas aanze kulia tena na kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wa mkasa huu wiki ijayo.

Maoni tumia namba za juu.

Leave A Reply