The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-35

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale mbuzi walipokatiza barabarani ghafla hivyo gari alilopanda Dorcas kuyumba na kusababisha mama wa Kiarabu aliyekuwamo kushtuka na kupoteza fahamu. Je, kilifuatia nini? Endelea sasa…

Kitendo cha yule mama kupoteza fahamu kilitukosesha raha, dereva alisimamisha gari tukaanza kumpepea kwa kutumia magazeti lakini hakuzinduka.

“Huyu atakuwa na tatizo la presha, sasa sijui tufanyeje?” dereva alimwuliza mama.

Kwa kuwa mama alikuwa na uzoefu wa mambo ya tiba alishauri tutafute sehemu iliyokuwa na kimvuli ili apulizwe na upepo wa kutosha angezinduka.

Alipotoa ushauri huo, dereva alilipeleka gari chini ya mti wenye kimvuli ambapo palikuwa na upepo wa kutosha akafungua milango yote. Mama hakuacha kumpepea, yule mama akafumbua macho na kuanza kuangaza huku na huko, hali iliyotupa matumaini, mama akamwuliza alijisikiaje!

Yule mama wa Kiarabu hakujibu badala yake aliendelea kuangaza tu macho yake, mama akasema tumuache kama dakika kumi au zaidi angezinduka kabisa.

Kweli, kama alivyosema, baada ya kupita dakika kumi na tano, yule mama aligeuza shingo upande aliokuwa mama na kumuuliza tulikuwa wapi.

“Tupo safarini tunaenda Dar es Salaam,” mama alimjibu.

Alipoambiwa hivyo, alishangaa na kuuliza; “Tunakwenda Dar es Salaam kwa nani?”

Kufuatia swali lake tulijikuta tukiangua kicheko ndipo mama alimwambia tulikuwa safarini lakini kwa bahati mbaya tulipata tatizo lililomfanya awe katika hali ile.

Mama alimwuliza kama hakukumbuka chochote, yule Mwarabu alitulia kwa muda na kuuliza begi lake lilikuwa wapi, mama akamuonesha, alipoliona alitabasamu.

Baada ya kufanya hivyo, aliinuka kisha kuuliza kwa nini dereva aliegesha gari chini ya mti, mama akamsimulia kila kitu kuhusu tulivyonusurika katika ajali.

Alipoambiwa hivyo, alimshukuru Mungu ndipo alituambia alikuwa na tatizo la presha, anaposhtushwa na jambo alikuwa akipoteza fahamu. Mama huyo, alifungua begi lake akatoa vidonge viwili akameza, baada ya kutulia kwa dakika kadhaa tukaendelea na safari.

Maongezi yaliyojiri yalikuwa kumlaani mmiliki wa wale mbuzi kufuatia kitendo chake cha kuwaacha wakirandaranda hovyo barabarani bila uangalizi.

Dereva aliendesha gari hilo kwa kasi hadi tulipofika Dodoma, tukaenda kula kisha safari ya Dar ikaendelea.

Mungu jalia tulifika Dar, salama salimini na kupokelewa na watoto wa yule mama, dereva ambaye mpaka muda huo sikufahamu walikuwa na uhusiano gani na mama alituaga akaondoka na yule kijana mwingine.

Baada kuweka mizigo na mabegi sehemu husika, yule mama alinikaribisha kwa kuniambia pale palikuwa  nyumbani kwake hivyo niwe huru kwa kila jambo.

Aliniambia mumewe hakuwepo, alinitambulisha kwa binti mmoja ambaye alisema ni dada yaani binti wa kazi, akasema anaitwa Tabu.

Alinitambulisha pia kwa binti mwingine aliyeonekana kama alisoma darasa la sita au la saba, akaniambia anaitwa Beatrice ambaye alizoeleka zaidi kwa jina la Bite.

Wakati ananitambulisha akafika dada mwingine ambaye alinipita kidogo umri, akasema alikuwa akiitwa Monica na kwamba ndiye alikuwa bintiye mkubwa.

Akiwa anaendelea na zoezi la utambulisho, nilimuona kijana akitokea kwenye korido akija sebuleni, umri wake haukuwa tofauti na wa Monica na walionekana kufanana.

Mama akamwita kwa jina la Barton, alipoitika akamwambia walipata mgeni yaani mimi ndipo akanitambulisha kwamba Barton na Bite walikuwa mapacha, nikasalimiana naye.

Je, kilifuatia nini katika maisha ya Dorcas? Usikose wiki ijayo. Maoni, tumia namba hiyo juu.

Leave A Reply