The House of Favourite Newspapers

Kilichotokea Mahakamani Leo Wakili wa Wema na Serikali

WAKILI Albert Msando wa mwigizaji na mrembo wa mwaka 2006 nchini, Wema Sepetu,  amehoji sababu za shahidi wa upande wa mashtaka (serikali) katika kesi inayomkabili mnyange huyo kutofika mahakamani, huku zikitolewa sababu zisizokuwa na ushahidi.

 

Msando ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 4, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomuachia huru Wema ambaye baadaye alikamatwa tena na askari wa Jeshi la Magereza.

 

Hakimu Mkazi Mkuu, Maira kasonde  alimwachia huru mshtakiwa huyo chini ya kifungu cha 225 (5) cha mwenendo wa mashtaka ya makosa ya jinai.

 

Wema anakabiliwa na mashtaka ya kurekodi video ya ngono na kuisambaza katika mitandao ya kijamii. Hatua hiyo imekuja baada ya wakili wa Serikali,  Gloria Mwenda,  kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Maira Kasonde, kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili kusikilizwa lakini shahidi waliyekuwa wakimtegemea wamepewa taarifa kuwa anaumwa.

 

Baada ya maelezo hayo Msando amedai taarifa iliyotolewa mahakamani hapo haijajitosheleza,  na kuhoji kama mhusika alianza kuumwa jana au juzi, ilitakiwa kutolewa taarifa zinazojitosheleza.

 

“Pande zote mbili zinatakiwa kutoa taarifa zinazojitosheleza. Nakumbuka mahakama ilitoa agizo kama ikitokea mtu anaumwa anatakiwa apeleke hati inayothibitisha

 

“Hilo ndio lilisababisha Wema kuwekwa rumande kwa wiki moja iweje huyo shahidi asifanye kama mahakama inavyotaka,” amedai Msando akidai kwa zaidi ya siku 60 shauri hilo limekuwa likiahirishwa.

 

Kutokana na hali hiyo,  Msando ameiomba mahakama hiyo kutopokea ombi la upande wa mashtaka la kuahirisha shauri hilo.

Hata hivyo, Hakimu Kasonde amesema mahakama ilikuwa tayari kusikiliza kwa ushahidi tangu Machi 28, 2019,  lakini ilishindikana kutokana na upande wa mashtaka kutokuwa na mashahidi.

 

Kasonde amesema Aprili 18, 2019,  pia ilitakiwa isikilizwe lakini upande wa mashtaka hawakuleta mashahidi hadi leo, na kwamba  upande wa mashtaka wamekuwa wakitoa sababu mbalimbali ikiwemo shahidi waliyemuandaa ana udhuru au mgonjwa.

 

“Maofisa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ndiyo waliobaini tukio hili na hawa wapo hapa jijini Dar es Salaam ndiyo waliotoa taarifa polisi,  kwa nini wasije TCRA wa karibu?  Mnataka mashahidi kutoka Arusha?” amehoji Kasonde.

 

Kasonde alisema kesi inapoamriwa kwa wakati inamfanya  mshtakiwa afanye maendeleo yake ya kiuchumi ili aweze kupata kipato na taifa kwa ujumla.

 

Kutokana na hoja hizo, Hakimu alimuachia Wema huru chini ya kifungu cha 225(5) cha mwenendo wa mashtaka ya makosa ya jinai.

 

Katika kesi hiyo, Wema anadaiwa Oktoba 15, 2018, katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam alirekodi video ya ngono na kuisambaza katika ukurasa wa  mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

 

Comments are closed.