testiingg
The House of Favourite Newspapers

Kilimanjaro Marathon Yatoa 11.3m/- Kwa Watoto Wenye Saratani

0

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TLM, Dk Trish Scanian.

UONGOZI wa Mbio ndefu za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon umetoa msaada wa shilingi milioni 11.3 (sawa na Dola za Marekani 4,898) kwa shirika la hisani la Tumaini La Maisha (TLM) linalojishughulisha na matibabu ya watoto wenye saratani katika Hospitali ya KCMC mjini Moshi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji wa mbio hizo zinazofanyika kila mwaka, ilisema kuwa msaada huo umetokana na mapato ya hisani kupitia mbio zilizofanyika mwaka huu (2023) ambayo alisema yote yatakwenda kuhudumia watoto wanaopatiwa matibabu ya saratani katika hospitali ya rufaa ya kanda ya KCMC, iliyoko Moshi, mkoani Kilimanjaro.
“Tunamshukuru kila mshiriki kwa kuchangia jambo hili muhimu la matibabu  ya saratani kwa watoto wadogo; sehemu ya mapato yaliyopatikana katika mbio za mwaka huu kama ada za viingilio,
zitakwenda kuchangia matibabu ya watoto wengi ambao wanahudumiwa kupitia taasisi ya TLM”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya waandaaji msaada huu  unatolewa kwa mwaka wa pili mfululizo, ikiwa ni juhudi za kuwahudumia watoto wanaopata matibabu ya ugonjwa wa saratani kwa ushirikiano na TLM katika kupitia mpango huo wa hisani.
Aidha uongozi wa mbio hizo pia umeishukuru uongozi wa kampuni ya Hoteli ya Kibo Palace yenye kumiliki hoteli katika Jiji la Arusha na Moshi mjini kwa kukubali kushirikiana na ta TLM katika mpango huo wa hisani kwa ajili ya matibabu ya saratani kwa watoto wadogo.
“Kupitia mpango huo, wageni waliokaa katika hoteli zao wakati wa mbio za Kili Marathon 2023 walichangia shirika hilo kupitia ufadhili wa kampeni iliyopewa jina la First Dollar-a-Bed-Night (kwa kila Dola ya kwanza kwa kila kitanda) ambapo mchango huo umepelekea msaada uliotolewa kwa ajili ya matibabu ya saratani kwa watoto kupitai TLM”, iliendelea kusema taarifa hiyo.
Zaidi ya hayo, waandaaji wa mbio hizo pia wamempongeza mhamasishaji maarufu kwa jina la Bongozozo, ambaye alitoa hamasa kubwa kwa washiriki wa mbio hizo hususan zile za kilomita 21 maarufu kama Tigo Half Marathon, uliopelekea upatikanaji wa jumla ya shilingi milioni 2.5 za ziada ikiwemo shilingi laki moja (100,000/-) kutoka kwa bondia maarufu hapa nchini Karim Mandonga.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa TLM, Dk Trish Scanian alisema taasisi hiyo imefarijika sana kupata msaada kutoka Kilimanjaro Marathon, mashindano ambayo alisema ni moja ya tukio la kimichezo maarufu Barani Afrika linalowakutanisha zaidi ya washiriki 11,500 kutoka zaidi ya mataifa 50 duniani kote.
“Kwa kweli ni jambo la kustaajabisha kwamba tukio kama Kili Marathon linaweza kusaidia kufadhili huduma za saratani ya watoto nchini kote kwa ushirikiano na TLM, kupitia matibabu na matunzo kwa watoto wenye saratani katika hospitali nchini kote”, alisema.
Dk Trish alisema mbali na kuunga mkono juhudi za TLM kupitia ufadhili huo maalum, ushirikiano wa taasisi hizo mbili pia utasaidia kuongeza uelewa kwa umma juu ya kazi inayofanywa na TLM katika
kuwahudumia watoto ambao wanakabiliwa na ugonjwa wa saratani nchini.
“Nitumie fursa hii kuwaomba wadau wengine na watu wenye mapenzi mema kwa ujumla kuungana nasi katika kusaidia shughuli za TLM zinazolenga kuimarisha na kuongeza wigo wa huduma za saratani kwa watoto katika mikoa yote ya Tanzania”, alisisitiza.
Kili Marathon huandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa kitaifa na kampuni ya Executive Solutions, ambayo inajihusisha na uaandaaji wa matukio, mahusiano ya umma na
uwakala katika usimamizi wa maswala ya habari na matangazo aina mbalimbali.

Leave A Reply