The House of Favourite Newspapers

Kim Poulsen Atajwa Taifa Stars

0

ALIYEWAHIkuwa mshauri wa ufundi kwa timu za taifa za vijana hapa nchini, Kim Poulsen raia wa Denmark, anatajwa kuja kuchukua mikoba ya Etienne Ndayiragije katika kikosi cha Taifa Stars.

 

Poulsen ambaye pia aliwahi kuinoa Taifa Stars, ametajwa kuchukua mikoba ya Ndayiragije baada ya kocha huyo raia wa Burundi kuonekana kushindwa kuipa mafanikio Stars. Pia inaelezwa anatakiwa kuongezwa kwenye Benchi la Ufundi la Ngorongoro Heroes katika michuano ya AFCON U20.

 

Ndayiragije ambaye aliiongoza Taifa Stars kufuzu na kushiriki michuano ya CHAN 2021, amekuwa akipigiwa kelele za kutakiwa aondolewe na kuletwa kocha mpya.

 

Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, zinadai kwamba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lipo kwenye mazungumzo na Poulsen kumpa majukumu ya kuinoa Taifa Stars.“Poulsen anatajwa kurudi Taifa Stars, kwa taarifa ambazo ninazo ni kwamba muda wowote atakuwa hapa nchini kumalizana na TFF, anakuja kuchukua mikoba ya Ndayiragije,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Spoti Xtra lilimtafuta Ofisa Habari wa TFF, Cliffod Ndimbo kuthibitisha hilo, ambapo alisema: “Taarifa hizo hatujaziposti katika mitandao yetu ya kijamii, kama kukiwa na kitu lazima tutoe taarifa kila mmoja afahamu.”

 

Hivi karibuni, Rais wa TFF, Wallace Karia, aliliambia Spoti Xtra kuwa, uamuzi wa Ndayiragije kuendelea kuinoa Taifa Stars au kuondoka utategemea na ripoti yake atakayoiandaa baada ya kurudi hapa nchini kutoka kwenye michuano ya CHAN.

 

Alipotafutwa Poulsen kwa njia ya WhatsApp na kuulizwa kama anakuja Tanzania kuinoa Taifa Stars, hakujibu ingawa aliusoma ujumbe aliotumiwa.

Leave A Reply