The House of Favourite Newspapers

KIMBEMBE !ALICHOKIFANYA TRAFIKI HUYU HUWEZI KUAMINI

MOROGORO: NI patashika nguo kuchanika! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kijana mmoja wa Kimasai kuibua kimbembe cha aina yake baada ya kutoa sime na kutaka kuwajeruhi watu waliokuwa wamemzunguka, Ijumaa limeshuhudia tukio mwanzo mwisho.

 

ENEO LA TUKIO

Tukio hilo lililotokea mwishoni karibuni eneo la Masika, katikati ya Mji wa Morogoro, halikumuacha salama askari wa usalama barabarani (trafiki) ambaye alijitosa kuamulia na bila kujali tishio la kukatwakatwa na sime na kujikuta katika wakati mgumu.

 

Trafiki huyo aliyefahamika kwa jina la Ramadhan Said alilazimika kuacha kazi ya kuongoza magari na kuvamia kwenye kundi hilo la watu baada ya kuona masai huyo amepandisha mori na kumkata mtu na sime.

ISHU ILIKUWA HIVI…

Mashuhuda wa tukio hilo walipotakiwa kuelezea chanzo cha sekeseke hilo mpaka masai huyo kufikia hatua ya kupandisha mori na kucharanga sime wananchi walisema;

 

“Huyu masai alikuwa na wenzake wawili pamoja na huyu mke wake, walikuwa wanacheza kamari ya karata tatu pale relini, jirani na ofisi za Tanesco-Mkoa. Jamaa amecheza mara 10, akajikuta analiwa zote mbele ya mkewe na hakula hata mara moja.

 

“Ndipo alipokuja juu na kuhoji kamari gani hiyo anakula anayechezesha tu anayecheza hali? Hapo ndipo kimbembe kilipoanzia. “Jamaa (masai) alianza kudai arudishiwe pesa yake huku akisapotiwa na wenzake, lakini waliokuwa wakichezesha karata tatu waligoma kurudisha shilingi elfu 50 walizomla mmasai huyo.

 

MASAI AKINUKISHA

“Baada ya wale jamaa kugoma ndipo masai akachomoa sime na kumkata kichwani na begani jamaa aliyekuwa akichezesha kamari akaanguka chini huku akilia kwa maumivu.

WENZAKE WAMSAIDIA

“Wachezesha kamari wenzake waliokuwa pembeni walipoona tukio hilo ndipo wakamvaa masai aliyekuwa anataka arudishiwe chake la sivyo atalipa kisasi kwa kuwakata na sime, lakini hata hivyo, walijikuta wakichemka kwani wananchi waliingilia kati kumsaidia masai na kuwashutumu wachezesha kamari hao kwamba wanawaibia watu mchana kweupe hivyo acha wakatwe na sime.

 

“Jamaa hao wawili wa kamari, mmoja alikuwa na koti na mwingine bukta ya njano ndani wakazidiwa nguvu na wananchi wakaamua kukodi bodaboda na kumkimbiza mwenzao hospitalini.

 

WAREJEA, TIFU LAIBUKA

“Cha ajabu waliporudi Masika na kumuona yule masai na wenzake, wakaanza kwa kuwavamia wakitaka kuwanyang’anya sime yao ili walipe kisasi kwa wamasai ndipo alipotokea trafiki huyu kibabe na kuzima shambulio hilo lililokusudia kusababisha mauaji,” alisema shuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Agoustino Damas huku shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Athuman Ally akiongeza;

 

“Yaani alichokifanya huyu trafiki ni kitendo cha kishujaa, hata sisi tulishindwa kuamini kama kweli anaweza kuingilia na kumkamata mtu aliyekuwa na sime akitaka kukatakata watu. Wewe unaona kabisa unayekwenda kumuamua ameshika sime halafu unategemea nini?”

 

ALICHOSHUHUDIA PAPARAZI

Mara baada ya kutonywa na vyanzo, mwandishi wetu aliyekuwa akipiga misele eneo hilo, alimshuhudia trafiki Rama aliyekuwa stendi bubu ya daladala eneo la Masika akiacha kazi ya kuongoza magari na kwenda kumdhibiti ‘baba yoyoo’ huyo asisababishe mauaji na kama siyo yeye tungekuwa tunazungumza mengine.

 

APATA WAKATI MGUMU

Hata hivyo, Afande Rama alipata wakati mgumu wa kuamua vita hiyo kwani mkononi alikuwa mashine ya faini na faili. Wakati trafiki huyo akiendelea na mapambano hayo, ghafla aliibuka askari kanzu aliyekuwa doria huku amevaa kiraia na kumuongezea nguvu trafiki huyo na kufanikiwa kumkamata mmasai huyo aliyekuwa na mkewe na kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi (Centeral).

KAMANDA ANASEMAJE?

Gazeti la Ijumaa lilitinga katika Kituo Kikuu cha Polisi na kumhoji Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Wilbroad Mutafungwa ambaye alisema taarifa hiyo ilikuwa bado haijamfikia na kwamba huenda iko kwa wasaidizi wake. “Shekidele (Mwandishi wa Ijumaa) najua wewe utakuwa umeshapiga picha za tukio hilo, hebu nioneshe na mimi nilione,” alisema Mutafungwa.

 

Baada ya kuoneshwa picha za tukio hilo zima, kamanda huyo alishtuka na kuahidi kulifuatilia sakata hilo ili wote waliokuwa na makosa wachukuliwe hatua za kisheria. “Hapo lazima nifuatilie nijue kilichojiri na sheria ichukue mkondo wake maana kwa vyovyote kutakuwa na uvunjifu wa sheria na sisi tunataka kuhakikisha kunakuwa na usalama wa raia na mali zao,” alisema Mutafungwa.

Stori: DUNSTAN SHEKIDEKE, IJUMAA

Comments are closed.