The House of Favourite Newspapers

Kimenuka! Kigogo, Diwani CCM Watoleana Siri za Chumbani

 

UKISIKIA kimenuka; jua hali ya hewa imechafuka na kweli ndivyo ilivyo kwa kigogo mmoja na diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao ni mume na mke kuamua kutoleana siri za chumbani; Uwazi linakupakulia uhondo kamili. 

 

Kigogo anayetajwa kwenye sakata hilo ni Oberd Haruna Mapesa (59) ambaye ni ofisa wa juu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na mkazi wa Njiro Kontena jijini Arusha, huku Hawa Simbe (58) (pichani) akiwa ni Diwani wa Kata ya Handeni (CCM), mkoani Tanga.

Habari ilianza kuenea kama upepo wa kisulisuli na kulifikia dawati la Uwazi kwamba, wanandoa hao hawaelewani na kwamba wako kwenye mnyukano mkali.

 

MKE AFUNGUA PAZIA

Hawa alikuwa mtu wa kwanza kulifikia Uwazi na kulilalamikia kuwa, mumewe amemtelekeza yeye na watoto na kwamba sasa anajirusha vilivyo na akina mama wa pembeni.

 

“Tulifunga naye (Mapesa) ndoa ya Kiislamu mwaka 1985 wilayani Bariadi (mkoani Simiyu) na kujaaliwa kupata watoto watatu. “Lakini mwenzangu aligeuka kuwa kinara wa kuhudumia vimada, nilipoona mambo yanazidi kuwa ovyo niliamua kuondoka na kwenda Tanga.

“Baada ya mimi kuondoka, aliwafukuza pia watoto wetu hapo nyumbani na kubaki akiishi pekee yake na kuingiza wanawake wa kila aina nyumbani kwangu nyakati za usiku tena anatumia gari la ofisi,” alidai Hawa.

KIGOGO AJIBU MAPIGO

Raha ya kutafuna ni ugeuze shavu; ndivyo ilivyokuwa kwa mwandishi wetu ambapo baada ya kusikia madai ya Hawa ambaye ni mke wa Mapesa alilazimika kumtafuta kigogo huyo naye aseme chochote. “Kwa kuwa mke wangu ameamua kulipeleka suala hili kwa waandishi wa habari, acha na mimi nieleze ukweli.

“Mimi sijamfukuza, sema yeye ndiye ameondoka kwangu na kubeba watoto wote, nadhani suala kubwa anataka talaka yake lakini mimi siwezi kumpa talaka kwa sababu aliyeondoka ni yeye na wa kutoa talaka anapaswa kuwa yeye.”

AZUNGUMZIA WATOTO

Kuhusu suala la kutelekeza watoto, Mapesa alisema kuwa hajawatelekeza na kwamba anawahudumia kama kawaida.

“Nampatia fedha za matumizi kiasi cha shilingi laki sita kila mwisho wa mwezi pia anachukua bonasi ya dola 150 (shilingi 347, 730) inayotolewa na ofisi yangu kama motisha kwa wafanyakazi. “Lakini yeye amekuwa akihonga wananchi ili wampigie kura na kuonesha maisha ya kifahari,” alisema Mapesa.

ATUHUMU MKE KUNYIMWA UNYUMBA

Kama alivyosema awali kwamba naye ameamua kusema ukweli, Mapesa alimwambia mwandishi wetu kuwa amekuwa akinyimwa unyumba na mkewe kwa zaidi ya miaka miwili mfululizo.

“Nimekuwa nikienda Tanga, hata juzi nilikuwa natoka Dar es Salaam kikazi na kupitia hapo anapoishi ambapo ni nyumbani kwangu; ile nyumba nimejenga mimi. “Lakini wakati wa kulala anachukua magauni yake mazito ya CCM anavaa ili nisipate haki yangu ya ndoa, ukimgusa anakuwa mkali.

“Mpaka sasa nina miaka miwili na nusu siujui mwili wa mke wangu na mimi kama mwanaume rijali nashindwa kujizuia kutokana na mfadhaiko wa moyo, ndiyo maana nikatafuta hawara wa kunituliza,” alisema Mapesa.

MKE ALIPUKA NA ZITO

Kufuatia madai hayo, Hawa alimwambia mwandishi wetu kuwa: “Si kweli kwamba namnyima unyumba (Mapesa) sema yeye ni wa baridi hata ukimsogelea hakuna kitu, hasisimki. “Sasa nifanye nini? Najifunika  shuka nalala, maana kazi hawezi tena,” alidai Hawa; kwa wenye ufahamu wao wanajua alichokuwa akimaanisha.

HUYU HAPA MAPESA

Wakati mwingine raha ya mpira ni kupasiana, Mapesa baada ya kutuhumiwa kuwa ni ‘wa baridi’ alisema: “Sasa hao vimada anaosema ninao wanafuata nini kwangu? Huyu mwanamke ana wivu sana, akisikia tu nazungumza na simu na mwanamke fulani hata kama ni mfanyakazi mwenzangu, yeye anasema ni hawara yangu.”

HAWA AJIBU MAPIGO

Mapesa alipokiri kuwa kwa sasa anaishi na mwanamke mwingine hapo nyumbani kwake, mkewe aliibuka na madai kuwa wanawake wanaompapatikia wanafuata fedha na si kitu kingine.

“Muulize; kuna wakati hajataka kujiua baada ya kumhonga mwanamke mali na akamdhulumu? “Anawahonga ndiyo maana wanamfuata lakini mambo mengine hawezi,” alidai Hawa na kuongeza kuwa, anaendeleza mapambano ya kudai talaka yake hadi kieleweke.

ASIMULIA MWANAYE ALIVYOJIUA

Katika hali ya kusikitisha Hawa alidai kuwa, mtoto wao mmoja aliyemtaja kwa jina la Yusufu, hivi karibuni alijiua kwa kujichoma kisu kutokana na migogoro hiyo ya kifamilia.

Aliongeza kuwa, kifo cha mtoto wao kilileta mgogoro mkubwa kwenye familia hadi maiti yake ikakosa kuzikwa kwa heshima iliyostahili.

USHAURI WATOLEWA

Kutokana na siku za hivi karibuni kuwepo kwa taarifa za migogoro mingi kwenye ndoa, baadhi ya watalaam wa masuala ya kijamii wameshauri usuluhisho utumike zaidi kumaliza migongano kwenye ndoa.

“Kuanikiana siri, kukaa na visasi moyoni ni mambo ambayo hayawezi kuleta tija katika ndoa, kusameheana, kuvumiliana na kupendana ni mambo ya msingi kwenye ndoa,” alisema Joseph Alphonce mtaalam wa masuala ya kijamii aliyehitimu Chuo cha Ustawi wa Jamii, jijini Dar es Salaam.

Comments are closed.