The House of Favourite Newspapers

KIMENUKA KULANGWA-TEGETA ‘A’, WANANCHI WAMLILIA LUKUVI

Kiongozi wa wananchi hao, Venance Mpihigwa akiongea na wanahabari.

WAKAZI wa Tegeta A, eneo la Kulangwa lililopo Goba jijini Dar es Salaam wamepatwa na taharuki kubwa na kulazimika kuingia mtaani kuandamana baada ya kukuta nyumba zao zimeandikwa maneno ya ‘SIMAMISHA UJENZI’ bila kufahamika nani kafanya hivyo, katumwa na nani na kwa sababu zipi.

Wananchi hao wapatao 100, jana  wakiwa kwenye mkutano wa kujadili tukio hilo lililoibua taharuki kubwa walisema kuwa, wanachojua wao ni wakazi halali wa eneo hilo kwa muda mrefu lakini wameshangazwa na kitendo cha nyumba zao kuwekewa alama hizo bila kuwepo kwa maelezo yoyote.

Wananchi hao wakiandamana huku wakiwa na mabango yenye ujumbe kwa Magufuli, Lukuvi na Makonda.

 

Akiongea na mtandao huu, kiongozi wa wananchi hao, Venance Mpihigwa alisema kuwa, awali eneo hilo lilikuwa na mgogoro kati ya wananchi na familia ya mtu aliyefahamika kwa jina la Seif Ngane lakini Mkuu wa Wilaya ya Ubungo alifika na kuumaliza mgogoro huo kisha kuwaamuru wananchi kuendelea kujenga kwa kuwa walikuwa na uhalali wa umiliki.

Wananchi wa Kulangwa Tegeta ‘A’ wakiandamana.

 

“Sisi tuko eneo hili kihalali kabisa, na tunamshukuru sana mkuu wa Wilaya ya Ubungo ambaye kuna wakati alifika eneo la tukio ikiwepo familia ya Ngane iliyokuwa ikidai eneo hilo ni lao lakini mwisho kwa vielelezo vilivyopo visivyo na makengeza, aliamuru wananchi waendeleze makazi hayo.

“Cha ajabu sasa kuna watu kutoka Manispaa ya Ubungo ambao bado wamekuwa wakituletea usumbufu akiwemo Mrando (Afisa Ardhi Ubungo). Usumbufu huo ulitulazimu tufanye jitihada za kutaka kumuona Waziri Lukuvi ili ajue kwamba kuna watendaji wake huku chini wanasumbua raia.

“Lakini sasa wakati tukifanya jitihada za kumuona Lukuvi, juzi kuna gari ambayo ilikuja ikiwa na polisi wawili na watu wengine kama 8 hivi, wakaanza kuchora nyumba za raia kwamba wasimamishe ujenzi. Nyumba takribani 40 zimechorwa.

“Jambo hilo lilizua taharuki kubwa sana, lingekuwa ni zoezi lililofuata utaratibu isingekuwa tatizo lakini watu ambao hawajulikani, kufika kwenye makazi ya watu na kuanza kuandika, huoni inaweza kuleta uvunjifu wa amani?

“Tumejaribu kwenda kuuliza Manispaa ya Ubungo kujua kama kuna watu wamewatuma kufanya hivyo na kwa sababu zipi lakini hakukuwa na majibu ya kueleweka. Wananchi wako njia panda. Kwa hiyo tunamuomba Waziri Lukuvi ajue kuna tatizo katika eneo letu na ikibidi afike kwani akichelewa kuna siku damu itamwagika,” alisema kiongozi huyo.

Naye Benitho Chiwinga ambaye nyumba yake imeandikwa ‘SIMAMISHA UJENZI’ alisema: “Kuna mambo ya ajabu sana yanafanyika huku na ni vyema Lukuvi akajua. Hivi ‘from no where’ unakuta nyumba ambayo umeihangaikia kwa muda mrefu, leo anakuja mtu na kuandika bomoa kienyeji tu, haya yanawezaje kufanyika kwenye nchi hii inayoongozwa na rais anayetetea wanyonge? Lukuvi njoo Tegeta A, Kulangwa. Watendaji wa Manispaa ya Ubungo wanakuharibia kazi.”

Mtandao huu ambao ulikuwa eneo la tukio jana Jumapili ulishuhudia wananchi wengi wakiwa mtaani na mabango yaliyoandikwa; ‘RAIS MAGUFULI, SISI WANYONGE WA KULANGWA TEGETA ‘A’ TUNANYASIKA, TUSAIDIE.

Lingine liliandikwa; MAKONDA NJOO KULANGWA UTUSAIDIE BABA. Lingine lilikuwa na maneno haya: WAZIRI LUKUVI, WATENDAJI MANISPAA YA UBUNGO WANAKUHARIBIA KAZI, NJOO TEGETA ‘A’ TUNAONEWA!

Aidha, mwandishi wetu pia alipata fursa ya kuziona nyumba hizo zipatazo 42 zikiwa zimeandikwa ubavuni maneno ya SIMAMISHA UJENZI wakati zimeshakamilika na watu wanaishi.

Comments are closed.