The House of Favourite Newspapers

Kimwaga aipangua ‘first eleven’ Simba

0

KIMWAGA

Mshambuliaji Joseph Kimwaga.

Na Hans Mloli, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, amelazimika kupangua kikosi chake cha kwanza kwa ajili ya kuingia mshambuliaji Joseph Kimwaga aliyeonyesha kiwango cha juu na kuisaidia Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, juzi Jumatano dhidi ya Stand United.

Kimwaga aliingia kwenye mechi hiyo akitokea benchi na kuchukua nafasi ya Said Ndemla dakika ya 46 na kisha katika dakika ya 57 akaifungia bao la ushindi katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Baada ya mchezo huo, Kerr alizungumza na Championi Ijumaa kuhusiana na mechi hiyo lakini kubwa lilikuwa juu ya kuridhishwa na uwezo ulioonyeshwa na Kimwaga katika mchezo huo huku akiahidi kumtumia pia kuiangamiza Mbeya City katika mchezo wao unaofuata.

“Kimwaga ni mzuri nimekuwa nikimuona tangu mazoezini, ni mchezaji anayejua anatafuta nini na kwa ajili gani, amekuwa anajituma ana tabia nzuri na mwenye kutaka mafanikio kila wakati ndiyo maana akawa ‘sub’ yangu ya kwanza nikijua kwamba atakwenda kubadili mchezo na kweli ikawa hivyo.

“Huwezi kujiuliza mara mbili kwa mchezaji kama huyu katika kumuanzisha kwenye mechi inayofuata kwa ajili ya kutaka mafanikio. Mechi inayofuata ya Mbeya City ni ngumu na nitamhitaji Kimwaga kwa ajili ya kusaidiana na wenzake kuchukua pointi tatu na si vingine,” alisema Kerr.

Kimwaga alisajiliwa Simba hivi karibuni kwa mkopo akitokea Azam FC na kwenye mchezo wa juzi ndiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza kuitumikia Simba na kufunga bao hilo.

Leave A Reply