The House of Favourite Newspapers

KINACHOSABABISHA MWANAMKE KUTOKWA NA UCHAFU MWEUPE SEHEMU ZA SIRI

WANAWAKE inawabidi kujichunguza kila siku ya maisha yao maeneo yao ya uzazi na matiti, vile vile kuichunguza nguo ya ndani aliyokuwa ameivaa siku hiyo kama kuna uchafu wowote umejitokeza.  Kufanya hivi kunaweza kumsaidia kugundua kuwa ana tatizo la kiafya sehemu zake nyeti. Nasema hivi kwani wapo baadhi ambao hawafahamu kuwa kila siku kuna uteute unaomtoka ambo ni hali ya kawaida. Ute huo unaweza kuwa mwingi au kidogo na huwa na rangi nyeupe au kahawia mpauko kama chai isiyokolea rangi bila kuwa na harufu mbaya.

Utokaji wa ute huo ni mojawapo ya njia ya uke kujisafisha wenyewe kwa kutiririka pamoja na mabaki ya hedhi au takataka za mwili au zilizotoka nje ya mwili. Ute huu huzalishwa na kuta za nyumba ya uzazi na huzifanya tezi za ukeni kushuka chini kutokana na nguvu za uvutano (gravity).

Kutokwa na uchafu mweupe au wa kijivu ulio kama maziwa ya mgando ukeni ni tatizo la kiafya, ni dalili mojawapo ya ugonjwa wa fangasi za ukeni kitabibu hujulikana kama Vaginal Candidiasis. Tatizo hili halipo katika makundi ya maradhi yatokanayo na kujamiana (STI), ingawa kugusana kwa kujamiana kunaweza kusambaza. Hata wanawake ambao hawashiriki tendo la kujamiana wanapata tatizo hili.

Kwa kawaida uke wenye afya njema huwa na bakteria rafiki na kiasi cha seli za fangasi (yeast cells), inapotokea mabadiliko ya usawa wa vimelea hawa wa fangasi huanza kujistawisha na kuzaliana.  Hali hii huweza kuleta viashiria na dalili za mwasho na kuvimba sehemu za siri. Kutoka uchafu mweupe kama maziwa ya mgando na mwasho huwa ni ndani au nje ya uke, uchafu huo huweza kuwa na harafu mbaya.

Mashavu ya sehemu za siri kuvimba, kuwaka moto wakati wa kutoa haja ndogo au kujamiana, maumivu wakati wa kujamiana, tishu za ukeni kuwa nyekundu, kutoka vidonda na vipele, hizo zote ni dalili. Tatizo hili linawapata wanawake mara kwa mara kutokana na maumbile ya uke yalivyo, huwa ni ya unyevunyevu hivyo mfumo wa ulinzi wa uke huweza kuharibiwa na kuwapa nafasi fangasi kustawi.

USHAURI

Tunashauri wanawake kuepuka kutumbukiza kitu chochote ukeni ikiwamo kuweka kemikali, manukato au vifaa vya plastiki, lengo ni kulinda mazingira ya ukeni yasiharibike ili bakteria rafiki walinzi waendelee kuwadhibiti fangasi.

Mambo mengine ambayo yanayochochea tatizo hili ni ujauzito, mabadiliko ya hali ya hewa (joto kali), mabadiliko ya viwango vya vichochezi vya kike (hormones), dawa za matibabu (antibiotiki), ulaji ovyo wa vyakula vya sukari, kutokuwa msafi kimwili na kutolala. Vile vile kuwa na maradhi ya akili (msongo wa mawazo na sonona), maradhi sugu ikiwamo kisukari na yanayopunguza kinga mwilini kama Virusi vya Ukimwi (VVU), saratani na lishe duni.

Ni kawaida tatizo hili likawa la muda likaisha lenyewe bila dawa yoyote au linaweza kuwa tatizo sugu linalodumu zaidi ya wiki mbili au likatibiwa na dawa mara kwa mara likawa linajirudiarudia. Kwakuwa katika hatua za awali ni rahisi kutibiwa na kupona, ni vizuri kufika mapema kwenye huduma za afya kama vile kwenye zahanati, kituo cha afya au hospitali apate unapoona dalili na viashiria nilivyovitaja hapo awali.

Na mtaalam wetu, A.Mandai

Comments are closed.