The House of Favourite Newspapers

KINARA UBAKAJI, UPORAJI

KINARA wa ubakaji na uporaji aliyetajwa kwa jina moja la Said maarufu kama Said Chiken mkazi wa Magomeni Makuti jijini Dar ameibua hofu kubwa kwa wakazi wa eneo hilo baada ya kudaiwa kufanya uhalifu mchana kweupe ambapo amekuwa akiwapora watu na kuwakata mapanga huku wakati mwingine akidaiwa kufanya vitendo vya ubakaji.

Wakazi wa eneo hilo walilieleza Risasi Jumatano kuwa kijana huyo pamoja na kundi lake wamekuwa wakitishia watu kiasi kwamba kila mwananchi amekuwa na hofu hata ya kutembea. “Yaani imefikia hatua tumekuwa tunaogopa kutembea hata mtaani kwani kijana huyo na wenzake wamekuwa tishio kubwa na wanafanya matukio ya uporaji hata mchana kweupe, kuna siku yeye na wenzake walimbaka dada mmoja,” alidai dada mmoja aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini kuhofia kufanyiziwa.

Dada huyo alidai kuwa, kijana huyo amewahi kumfanyia unyama kaka mmoja anayeitwa Mwinyi Pembe ambapo alimvamia usiku akiwa na wenzake na kumkatakata mapanga kisha akamuibia pikipiki na kumuacha akiwa na majeraha makubwa. “Sio huyo kijana tu ambaye ameshalizwa, kuna wamama wengi ambao wameporwa na wengine wamebakwa yaani imekuwa ni tishio kubwa ambalo linatuumiza kwani ni vijana ambao wameshindikana.

“Huyo Saidi aliwahi kufungwa miaka thelathini akatoka kwa msamaha wa rais lakini amerudi ndio matukio kila siku mchana na usiku, wakiamua siku wanafanya uhalifu nyumba kwa nyumba,” alisema. Baada ya kuongea na mtoa habari huyo, Risasi lilimsaka Mwinyi Pembe, mmoja kati ya watu waliowahi kujeruhiwa na kijana huyo na kuporwa pikipiki, naye alitoa ushuhuda.

“Ilikuwa usiku nilisimamishwa na kijana mmoja kama mtu ambaye ananifahamu, sikuwa na hofu, nikaamua kusimama na kumpa lifti, akapanda kwenye pikipiki mara akaniambia subiri kidogo.“Wakati nageuka ili nijue usalama wake ukoje akanikaba na vijana wanne wakatokea kichochoroni wakanipiga mapanga kichwani, kifuani na mkononi, nikawaachia pikipiki ili wasiendelee kunijeruhi.

“Walipanda pikipiki wakaondoka, mimi nikaamua kwenda kituo kidogo cha polisi usiku uleule, sikumkuta mtu nikatafuta pikipiki nikaenda kituo kikubwa cha Magomeni ndipo nikapewa PF3 na RB kwa sababu hali yangu ilikuwa mbaya sana nikapelekwa Hospitali ya Mwananyamala, baadaye nikaambiwa aliyenifanyia tukio lile anaitwa Said, ni kinara wa matukio hayo.“Kumbe wakati ananiomba lifti kuna watu ambao walimtambua,” alisema Pembe.

“Siku nyingine tukiwa ndani, Saidi na kundi lake la watu watatu walivamia nyumbani kwangu wakavunja geti wakaingia ndani na kuchukua pikipiki, sasa wakati wanahangaika kutoka nayo nje, mke wangu aliniamsha nikachungulia dirishani pikipiki nikawa siioni, nikaamua kutoka nje na kukuta geti liko wazi.

“Nilipotoka nje ya geti, nikawaona wanakata nyaya za pikipiki wakataka kuondoka nayo bila ya funguo, nikawaitia wezi sasa wakati wanakimbia, nilimuona Said kwa sababu nimesoma naye.

“Nilipomwambia Said unaniibia, akasimama na kuniita alipo eti tuongee, mimi sikwenda kwa sababu najua angeenda kuniua ili kupoteza ushahidi.“Wakaondoka, pikipiki wakaiacha palepale nje kwani ilizimika, nikaamua kwenda polisi Magomeni usiku uleule lakini sikupewa msaada wowote?”

Risasi Jumatano halikuishia hapo lilifunga safari hadi kwa baba wa Said aitwaye Mzee Chande kwa ajili ya malalamiko anayohusishwa mtoto wake ambapo alikiri kuzisikia habari hizo baada ya kuitwa na mwenyekiti lakini alishindwa kusema ndio au hapana.

“Juzi niliitwa na mwenyekiti wa mtaa, akanilalamikia sana kwa vitendo vinavyofanyika hapa mtaani kwa kile kinachosadikika kuwa kinafanywa na kijana wangu Saidi na kundi lake lakini mimi siwezi kusema ndio au hapana ila nilichomshauri mwenyekiti ni kuwa wafanye kila njia kuwadhibiti hao watu, basi.” Bada ya baba huyo kuongea hayo Risasi lilimtafuta mwenyekiti wa mtaa wa eneo hilo, Salum Mazowea ambaye alithibitisha kuibuka kwa kundi la Said na kufanya matukio hayo na kudai kuwa amepata malalamiko kibao kutoka kwa wananchi wake.

“Malalamiko nimeyapata hapa ofisini kwangu juu ya huyu mtu hatari, Said ni kweli aliwahi kufungwa miaka thelathini jela akatoka kwa msamaha wa rais. “Nimechukua hatua ya kwanza ambapo nilimuita baba yake mzazi Said na kuongea naye lakini nimegundua hana la kumfanya maana naye amehama kwake na anaishi msikitini kwa kukosa amani, ni mtu mzima sana.

“Hatua ya pili nimepanga kuitisha kikao cha wananchi wote wa eneo langu ili tujue tunafanyaje maana polisi wa Magomeni hawatujibu lolote licha ya kuwapa taarifa. “Kwa hali ilipofikia sasa tunaomba Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda aingilie kati, wananchi wa Magomeni Makuti hatuna amani kabisa,” alisema mwenyekiti huyo.

STORI: Shamuma Awadhi na Neema Adrian

Comments are closed.