The House of Favourite Newspapers

King Majuto Tumuombe! – Video

TUMUOMBEENI! Mungu afanye uponyaji kwa mzee wetu. Ndiyo kauli inayozungumzwa na Watanzania wengi waliomuona mkongwe wa vichekesho, Amri Athuman ‘King Majuto’ mara baada ya kurejea nchini akitokea India alikokuwa amekwenda kwa ajili ya matibabu.

Majuto alirejea nchini Ijumaa iliyopita akitokea nchini India alipokuwa amekwenda kutibiwa ugonjwa wa tezi dume katika Hospitali ya Apollo ambapo mara baada ya kuwasiri katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, alipelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uangalizi wa muda wa afya yake kabla ya kuruhusiwa kurudi nyumbani kwake mkoani Tanga.

WALIOMSHUHUDIA WANENA

Uwazi lilizungumza na baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar waliojitokeza kumpokea Majuto katika Uwanja wa Mwalimu Nyerere ambao wengi wao walihamasisha maombi ili mzee huyo aweze kurejea katika hali yake ya kawaida.

Juma Kimoyo aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa Jeti jijini Dar, aliwaomba Watanzania wamuombee Majuto kwani ana mchango mkubwa katika sanaa ya maigizo na bado mchango wake unahitajika.

“Jamani nawahamasisha Watanzania wenzangu tumuombee Majuto. Huyu ni chachu ya sanaa nchini, wengi wamepita kwenye mikono ya mzee huyu.

“Mchango wake bado unahitajika. Busara, mawazo yake na hata vituko vyake ni tunu kubwa katika sanaa ya Bongo.

“Nawaomba sanasana jamani kila mmoja kwa imani yake tumuombee ili tuweze kumuona tena kwenye luninga akitupa vimbwanga vipya,” alisema Kimoyo.

Naye Baraka Duma, aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa Buguruni jijini Dar, alisema amemtazama Majuto alivyoondoka na alivyorudi, anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kwenda kutibiwa India lakini bado akasisitiza juu ya umuhimu wa maombi.

“Jamani kuna siri kubwa katika maombi. Mungu wetu wa Mbinguni hashindwi na kitu, tumuombee na ninaamini kwa kuwa tayari ameshapata tiba ya kidaktari, maombi yetu yatasaidia sana kwa sasa,” alisema.

WASANII WAMUOMBEA

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Uwazi, wasanii mbalimbali wa filamu waliishukuru Serikali kwa kugharamia matibabu ya mzee huyo lakini kubwa wanalolifanya kwa sasa ni kumuombea kwani wanatamani kumuona amepona haraka na arudi kwenye sanaa.

“Kwa kweli tunaishukuru Serikali lakini tunamuombea apone haraka maana sisi kama wasanii tunahitaji kumuona amerejea kwenye ubora wake ule wa zamani, Majuto ana identity yake katika suala zima la kuchekesha,” alisema Kulwa Kikumba ‘Dude’, msanii wa Bongo Muvi.

Muigizaji mkongwe wa sinema nchini, Blandina Chagula ‘Johari’ alipozungumzia kuhusu afya ya mzee huyo, alisema anamshukuru Mungu kumuona Majuto amerejea na anazidi kumuombea.

“Namuombea Mungu mzee wangu apone azidi kuwachekesha Watanzania kwani kuchekesha ndiyo maisha yake na kama mnavyojua Majuto kabla hajachekesha ukimuangalia tu tayari unacheka mwenyewe. Ni mtu ambaye Mungu amempa kipaji cha aina yake,” alisema Johari.

MITANDAONI NAKO NI MAOMBI

Baada ya picha mbalimbali zinazomuonesha Majuto akiwasiri kuwekwa mitandano, wafuasi mbalimbali wa mitandao wameonekana kuguswa na afya na King Majuto na kutoa maoni mbalimbali ya kumuombea.

“Jamani natamani nimemisi Majuto, huyu mzee ni zaidi ya mchekeshaji kwa kweli Mungu ampe nguvu arudi atupe raha sisi mashabiki wake,” alichangia mdau aliyejiita Kikoti katika mtandao wa Instagram.

WENGINE WAPATA HOFU

Baadhi ya wafuasi hao wameonesha kuwa na hofu na kitendo cha kurudi na kufikia hospitali badala ya nyumbani jambo ambalo limetolewa ufafanuzi mzuri na mtoto wa Majuto, Hamza Amir ambaye amesema kitendo cha kupelekwa hospitali ni cha kawaida kutokana na uchovu wa safari.

“Amefikia hospitali kwa ajili ya uangalizi wa muda mfupi. Ni jambo la kawaida kwa mgonjwa aliyesafiri umbali mrefu kufikia hospitali ili aweze kupumzika na madaktari wamuangalie kidogo kabla ya kumruhusu,” alisema Hamza alipozungumza na Uwazi, juzi Jumapili.

Hamza alipoulizwa kuhusu maendeleo ya afya ya baba yake na pengine ni lini wanatarajia anaweza kuruhusiwa, alisema anaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani.

“Anaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa,” alisema Hamza.

AFISA HABARI KINONDONI

Afisa Habari wa Chama cha Waigizaji Kinondoni, Masoud Kaftany ambaye pia alikuwa mstari wa mbele katika kuratibu matibabu ya Mzee Majuto alisema wanamshukuru Mungu amerudi salama na kuwataka watu wasiwe na wasiwasi kwa kitendo cha kufikia hospitali.

“Ni kawaida kabisa ukitokea nchi za mbali kwa ajili ya matibabu, lazima uchekiwe kidogo hivyo wasiwe na wasiwasi,” alisema Kaftany.

MSEMAJI WA MUHIMBILI ANENA

Msemaji wa Muhimbili, Aminiel Aligaesh alipoulizwa juzi na Uwazi kuhusu maendeleo ya Majuto alisema bado wako naye na anaendelea vizuri.

“Bado tunaye, anaendelea vizuri lakini kama mnataka maelezo zaidi mnaweza kuwatafuta wanafamilia,” alisema Aligaesh.

KINACHOWATIA HOFU WENGI

Imani ya wengi waliojitokeza kumpokea mzee huyo uwanja wa ndege na wanaokwenda kumjulia hali hospitalini ni kumuona akiwa mwenye afya iliyoimarika.

“Mi bado naona kama mzee Majuto bado anaumwa, kwa sababu nilitarajia akitoka India awe anaweza kutembea mwenyewe.

“Lakini nimeona anabebwa, nadhani ipo haja kwa madaktari kuendelea kumfanyia matibabu zaidi, ili kama kuna vitu havijawekwa sawa India vimaliziwe hapa,” alisema msichana aliyejitambulisha kwa jina moja la Aneth mkazi wa Sinza jijini Dar.

Matarajio ya Aneth kwa baadhi ya watu ndiyo yanayochangia kuwepo kwa mijadala yenye mitazamo tofauti juu ya afya ya King Majuto kwa wengine kuona hajapata nafuu itarajiwayo na wengine kuona angalau kuna hatua za kimatibabu zimepigwa.

Uwazi nalo lilipotafuta undani wa mwenendo wa afya msanii huyo liliishia kwenye pande mbili za ‘nafuu’ na ‘bado anahitaji tiba,’ jambo linalokomea kwenye fikra za wengi juu ya afya za wanadamu kuwa zinahitaji mapenzi ya Mungu.

TUJIKUMBUSHE

Kabla ya kupelekwa nchini India Mei 4, mwaka huu, King Majuto ambaye pia alikuwa akisumbuliwa na tatizo la nyonga, alilazwa katika Hospitali ya Tumaini jijini Dar, kisha akahamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Matibabu ya mzee huyo kwa kipindi cha takriban miezi miwili, yaligharamiwa na serikali inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli.

MAJUTO: “MIMI NI MZIMA, NIKIFA MNIZIKE KWA WINGI”, AMTAJA KANUMBA – VIDEO

Comments are closed.