
Mark Carney amechaguliwa kuwa kiongozi mpya wa chama tawala nchini Canada, Liberal Party, baada ya kuwashinda wapinzani wake watatu. Ushindi wake unaashiria kuwa atakuwa Waziri Mkuu mpya wa Canada, akimrithi Justin Trudeau katika siku chache zijazo.
Katika hotuba yake ya ushindi, Carney alisisitiza dhamira yake ya kuimarisha uchumi wa Canada na kudumisha mahusiano thabiti ya kimataifa. Hata hivyo, hakusita kumkosoa Rais wa Marekani 🇺🇸 Donald Trump kwa kuongeza kiwango cha ushuru kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Canada, akisema kuwa hatua hiyo itaathiri uchumi wa nchi yake na kusababisha matatizo kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Carney, ambaye ni mchumi na aliyewahi kuwa Gavana wa Benki ya Canada na Benki ya England, anaingia madarakani wakati ambapo Canada inakabiliana na changamoto za kiuchumi na kisiasa. Wananchi wanatarajia uongozi wake kuleta mabadiliko chanya kwa taifa.