The House of Favourite Newspapers

Kiongozi wa ACT Wazalendo Atangaza Mabadiliko katika Baraza Kivuli la Mawaziri

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Manka Semu

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Manka Semu, ametangaza mabadiliko katika Baraza Kivuli la Mawaziri la chama hicho baada ya mashauriano na Waziri Mkuu Kivuli Isihaka Mchinjita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Kiongozi wa chama hicho, Idrisa Kweweta, na kuwasilishwa na Abdallah Khamis, Afisa wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa ACT Wazalendo, uteuzi huo umeanza rasmi, Januari 28, 2025.

Katika mabadiliko hayo, viongozi mbalimbali wamepewa nafasi mpya ndani ya Baraza Kivuli, ikiwa ni hatua ya kuboresha usimamizi wa serikali kwa upande wa upinzani.

Walioteuliwa ni pamoja na Riziki Shahari Mngwali, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kabla ya uteuzi huu, Riziki alikuwa Waziri Kivuli wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Shangwe Mika Ayo ameteuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Hapo awali, Shangwe alikuwa Naibu Waziri Kivuli wa Fedha, Mipango na Hifadhi ya Jamii.

Mhandisi Fidel Hemed Christopher ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Kivuli wa Uchukuzi. Kabla ya uteuzi huu, alikuwa Naibu Waziri Kivuli wa Miundombinu.

Miraji Mwadini Ali ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Kivuli wa Fedha, huku Marijani Rajibu Nandavale akiwa Naibu Waziri Kivuli wa Mipango na Hifadhi ya Jamii. Kabla ya uteuzi huu, Nandavale alikuwa Naibu Waziri Kivuli wa Mifugo na Uvuvi.

Julius J. Massabo ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara. Kabla ya uteuzi huu, alikuwa Naibu Waziri Kivuli wa Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika.

Felix Kamugisha sasa ni Naibu Waziri Kivuli wa Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika. Awali, alikuwa Naibu Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara.

Hussein H. Kalyango amekuwa Naibu Waziri Kivuli wa Utumishi na Utawala Bora. Kalyango aliwahi kuwa Diwani wa ACT Wazalendo kati ya 2015-2020 na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii.

Lushona Mathias Kamwina ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Kivuli wa Miundombinu.