The House of Favourite Newspapers

Kiongozi wa Upinzani Bahrain Ahukumiwa Jela Maisha

Sheikh Ali Salman

KIONGOZI wa upinzani nchini Bahran,  Sheikh Ali Salman,  amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya mahakama ya rufaa kumpata na hatia ya kupeleleza kwa niaba ya Qatar. Hukumu hiyo inakuja miezi michache baada ya mahakama ya juu nchini Bahrain kumuondolea mashtaka Salman kwa kushirikiana na taifa hasimu.

Bahrain ilikata uhusiano wake na Qatar mwaka 2017. Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty limetaja uamuzi huo kama ukiukaji wa haki wakati huu ambapo Bahrain inaendelea kuwazima wakosoaji. Ali Salman ambaye aliongoza vuguvugu ambalo sasa limepigwa marufuku la Al-Wefaq, alilaumiwa kwa kushirikiana na Qatar kuendesha vurugu dhidi ya serikali mwaka 2011 pamoja na viongozi wenzake wa upinzani Hassan Sultan na Ali al-Aswad.  Wawili hao hawakuhukumiwa vifungo vya maisha.

Mwendesha mashtaka nchini Bahrain alisema watu hao watatu walifungwa kwa kuwasiliana na maofisa wa Qatar kuipindua serikali. Lakini madai hayo ambayo ni ya miaka saba iliyopita yalifichuliwa mwaka uliopita baada ya Bahrain, Saudi Arabia, UAE na Misri kukata uhusiano na Qatar. Washirika hao waliilaumu Qatar kwa kuunga mkono makundi ya kigaidi na kuwa karibu sana na Iran, madai ambayo Qatar inayakana

Waandamanaji wakiongozwa na jamii kubwa ya Shia waliingia barabarani Februari mwaka 2011 wakitaka demokrasia ziaidi. Lakini familia ya kifalme ya Al Khalifa inayoshikilia nafasi nyingi za kisiasa na kijeshi ilizima maandamano hayo kwa msaada ya nchi majirani hasa Saudi Arabia.

Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu 30 wakiemo polisi watano. Tangu wakati huo Bahrain imekumbwa na misukosuko. Katika kukabiliana na hali hiyo, Bahrain imepiga marufuku vikundi vya upinzani huku mamia ya wakosoaji wa serikali wakitupwa jela.

Comments are closed.