The House of Favourite Newspapers

Kigogo Yanga Akanusha Uzushi, Amzungumzia Morrison

0

MKURUGENZI wa Sheria na Wanachama wa Klabu ya Yanga SC, Patrick Simon, jana mchana alitoa waraka kukanusha tuhuma zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa anaihujumu timu kwa watani wao Simba SC.

 

Katika waraka huo, Patrick ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, umefafanua mambo matano ambayo baadhi ya watu na mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, alitamka hadharani kuwa anawahujumu kwa mahasimu wao Klabu ya Wekundu wa Msimbazi, Simba.

 

Kupitia mitandao yake ya kijamii, Patrick ameanza kwa kuzijibu tuhuma anazozushiwa kuwa anakutana kwa siri na baadhi ya viongozi wa wapinzani wao, Simba, ikiaminika kuwapa taarifa nyeti za klabu ya Yanga kwa wapinzani wao.  Amanza kwa kuandika:

 

“Nakiri kukutana na mtendaji mwenye cheo kama changu  maeneo ya Yatch Club lakini siyo vikao vya siri kwani kilichonikutanisha na mtendaji huyo ni suala  muhimu ambalo viongozi wangu wakubwa watatu walikuwa wanajua na walinipa baraka zote, na mara baada ya kikao hicho nilirudisha mrejesho wa kilichonipeleka. Na hii tunaongelea tarehe 20/10/2020 hivyo hakuna siri yoyote .”

 

Hilo likiwa mosi, pili ni kuhusu tuhuma ya kufanya kazi kwa kuihujumu Yanga kwa sababu ana hofu ya kupoteza nafasi ya Ukaimu Katibu Mkuu kwa aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba msimu uliopita, Senzo Mazingisa, ili kuandaa mazingira ya kupokelewa Simba endapo akiondoka Yanga.

 

Patrick ameandika: “Mimi nakaimu nafasi ya katibu mkuu lakini nimeajiriwa kama Mkurugenzi wa Sheria, hivyo basi siwezi kumhofia Mr. Senzo kwani yeye siyo mwanasheria bali ni mshauri wa klabu”.

 

Tuhuma inayomuumiza Patrick ni kuambiwa aliihujumu kesi ya Bernard Morisson kwa Simba; “Mimi ndiye niliyetengeneza ule mkataba, kwa hiyo kisheria nilikuwa sifuzu kutetea ile kesi, hivyo basi klabu iliamua kuweka wabobezi wawili ambao wamenizidi seniority kuweza kupambana na hiyo kesi na ndiyo wanaotuwakilisha huko CAS”.

 

Masikio ya wapenzi wa Yanga na wafuatiliaji wa soka nchini yamesubiri kwa muda kusikia hatma ya kesi ya Yanga kwenye mahakama ya usuluhishi ya masuala ya kimichezo duniani (CAS) juu ya uhalali wa mkataba wa mchezaji Bernard Morisson ambaye hivi sasa anakipiga kwa watani wao wa jadi.

 

Katika waraka wa kujibia tuhuma zinazomkabili, Patrick amegusia kesi hiyo: “Kesi yetu CAS imesajiliwa kwa namba CAS2020/A/7397. Hii maana yake ni kesi ya 7397. Ikumbukwe CAS inapokea kesi kutoka nchi ambazo ni wanachama wa FIFA dunia nzima, na ina kesi nyingi sana kama ilivyo mahakama ya rufaa ya Tanzania. Hivyo msiwe na haraka sana kwenye masuala ya sheria,” alimalizia hivyo Patrick.

 

Vilevile Shauku ya wapenzi wa Yanga na wafuatiliaji wa soka nchini ilikuwa ni kutaka kujua ni kesi ngapi ambazo Yanga wamezipeleka kwenye Shirikisho la Soka nchini na zimefikia wapi, ambapo Kaimu Katibu huyo amefafanua kwenye waraka wake maana ametuhumiwa kutokuzipigania kesi hizo kwa kulinda maslahi ya Simba.

 

“Mpaka sasa Yanga ina kesi nne ambazo Shirikisho limeamua kuzipotezea.  Kesi ya Kabwili, Morisson kuhongwa $5,000 kushawishiwa kuihama Yanga, pingamizi la usajili wa Morrison na kesi ya mkataba wa nyota huyo wa Ghana ambao haujasainiwa na pande zote mbili na nina ushahidi wa kujitosheleza kwamba hizi kesi bado ziko pending kwenye shirikisho letu tukufu” ameeleza Patrick.

 

Kuhusu tuhuma za Kiongozi huyo kutopokea simu za Mwenyekiti wa Klabu hiyo na baadhi ya viongozi amesema: “Hili suala sitolitolea maelezo kwani mwenyekiti ndiye mtu ninayeongoza kwa kuwasiliana naye katika viongozi pale klabu.

 

Mwisho akamaliza kwa kuandika: “Kwa nafasi yangu kama ningekuwa mtu wa kuihujumu klabu ningekuwa milionea mpaka sasa, mimi nimekula kiapo cha maadili ya kazi yangu, mpaka natoka Yanga siwezi kufanya jambo lolote la kuihujumu klabu ambayo kwangu ni kama dini. Muda utaongea, muda ni wetu sote. Daima mbele nyuma mwiko.”

Leave A Reply