The House of Favourite Newspapers

Kipigo cha Stars, Makocha wa Vilabu Lawamani

0

KUFUATIA kipigo cha mabao 2-0 walichokipa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwenye michuano ya CHAN kundi D dhidi ya timu ya taifa ya Zambia, kocha mzoefu  nchini ambaye ni Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ametupa lawama kwa makocha wa vilabu kushindwa kuwaanda wachezaji washindani.

 

Mingange amewahi kuvinoa vilabu vya Azam FC, Ndanda FC na sasa akiwa na kikosi cha Lipli ya Iringa.

 

“Hata ukiangalia mchezaji mmoja-mmoja, Wazambia walikuwa bora kuliko sisi na hii yote inatokana na sisi walimu kutofanya kazi huko kwenye vilabu wanakotoka wachezaji.  Kuna makosa ya utumiaji wa miguu, kuna makosa ya upigaji wa pasi na makosa kwenye ile miondoko mitatu yaani tukiwa hatuna mpira tunatakiwa twende wapi tukiwa na mpira twende wapi.

 

“Yaani uwezo wa mchezaji kujitambua wakati huu kuna jukumu gani, Hili si jukumu la kumfundisha mtu timu ya taifa anatakiwa awe na misingi hiyo akiwa katika klabu yake,” alisema.

 

Licha ya kipigo hicho kwenye mchezo huo ambao ni wa kwanza kwenye hatua ya makundi,  Taifa stars bado ina michezo miwili ya kujiuliza dhidi ya Namibia na Guinea, lakini Meja Mingange akaweka wazi juu ya kipi kocha Etienne Ndayiragije anapaswa kufanya ili kuhakikisha anapata ushindi kwenye michezo hiyo.

 

“Kwanza mwalimu abadilishe mbinu za mchezo, pili awaambie wachezaji wasifikirie matokeo yaliyopita, waanze na mechi inayokuja, akili yao itoke kwenye mechi iliyopita, kwa sababu tumeshaipoteza hatuhitaji tena kuihesabu.

 

“La tatu wachezaji wajue walichokikosea wasirudie tena, wayafanyie mazoezi makosa tuliyoyaona hasa kwenye kukaba, uasusani tunapokuwa hatuna mpira, nani anatakiwa awe wapi na kwa sababu gani, na hili ni tatizo kubwa sana kwa wachezaji wa Tanzania, tena inatokana na uvivu,” alisisitiza.

 

Taifa Stars itatupa tena karata yake ya pili Januari 23 dhidi ya timu ya taifa ya Namibia, mchezo utakaochezwa saa 4:00 usiku.

Leave A Reply