Kisa AS Vita, Gomes Ampa Kagere Kazi Maalum

KUELEKEA mchezo wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita utakaopigwa leo Ijumaa, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amefanya kikao kizito na washambuliaji wake wakiongozwa na Meddie Kagere na kuwataka kuhakikisha wanatumia kila nafasi watakayotengeneza kufunga mabao.

 

Baada ya kuwasili DR Congo, juzi, Simba iliyosafiri na kikosi chake chote ilianza mazoezi mara moja kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza wa hatua ya makundi unaotarajiwa kupigwa leo, kwenye Uwanja wa Martyrs jijini Kinshasa.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa jijini Dar es Salaam ikiwa ni kisasi cha kufungwa mabao 5-0 katika mchezo wa ugenini, hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/19.

 

Akiwazungumzia wapinzani wake AS Vita, Gomes ameliambia Championi Ijumaa kuwa tayari ame-pata nafasi ya kuwatazama wapinzani wake kupitia kanda za video katika michezo yote waliyocheza, ikiwemo michezo dhidi ya Simba na kugundua mbinu za kuweza kupata matokeo dhidi yao.

 

“Nimewataza AS Vita kupi-tia kanda za video za michezo yao, ikiwemo ile miwili waliyocheza na Simba katika hatua ya makundi msimu wa 2018/19, pia nimerejea michezo dhidi ya TP Mazembe pamoja na FC Platinum.

 

“Kupitia michezo hiyo tumepata nafasi ya kuona ubora na mapungufu yao na kujipanga vizuri kuhakikisha tunapata matokeo chanya katika mchezo huu.

 

“Kwa kuwa tutacheza ugenini hatutafunguka sana bali tutacheza kwa tahadhari kubwa ya kujilinda, na tumekaa na washambuliaji na kuwaasa kutumia kila nafasi ya kufunga tutakayotengeneza ili tuweze kupata matokeo,” alisema Gomes.

STORI: JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Toa comment