The House of Favourite Newspapers

KISA DILI LA KUSUKA BINTI APATA MAJANGA MAZITO!

DUNIANI kuna taabu, lakini jipe moyo! Mwanadada aitwaye Adelina Peter (25) (pichani), mkazi wa Yombo-Kilakala jijini Dar, amepatwa na janga zito na kujikuta akiangua kilio baada ya kufanyiwa kitu kisichokuwa na tiba kilichomsababishia ulemavu wa uti wa mgongo na mguu.  

 

Binti huyo alilisimulia Uwazi kuwa, alipata tatizo hilo baada ya kupata dili la kwenda kusuka jijini Arusha, kazi ambayo ndiyo iliyokuwa ikimuingizia kipato na kulea familia yao. Alieleza kuwa, ni miaka mitano sasa tangu alipotokewa ghafla na tatizo hilo ambalo lilimuanza baada ya kupata dili hilo kutoka kwa mmoja wa wateja aliokuwa akiwapatia huduma maeneo hayo ya Yombo-Kilakala.

 

Alisema ilikuwa mwaka 2014 ambapo alimsuka dada mmoja nywele zijulikanazo kama Yeboyebo ambaye alimlipa shilingi elfu saba. Baada ya kumsuka, alisema mteja wake huyo alifurahishwa na huduma yake lakini alikuwa anapata pesa kidogo hivyo alimuahidi kumfanyia mpango wa kwenda kusuka jijini Arusha ambako kazi hizo zinalipa.

 

Adelina alisema alibadilishana namba za simu na mteja wake huyo ambaye alipofika Arusha alimpigia simu na kumuunganisha na wahusika kwa ajili ya kazi hiyo, lakini tangu alipopokea simu hiyo ndipo alipopatwa na mauzauza. “Ghafla tu nilianza kujisikia maumivu katika maeneo ya kiuno na kushindwa kabisa kuendelea kusuka hivyo nikalazimika kulala tu kitandani muda wote,” alisimulia Adelina.

 

Alisema, alianza kujitibu kwa tiba za kienyeji na kumeza dawa za kutuliza maumivu ili aweze kuendelea na kazi yake hiyo ambayo ndiyo pekee iliyokuwa ikimuingizia kipato. “Lakini kadiri siku zilivyosonga ndivyo maumivu nayo yalizidi hadi kufikia hatua ya kushindwa kabisa kukaa,” alisema Adelina na kuendelea:

 

“Ilibidi nimweleze yule mteja wa dili la Arusha kuwa siwezi kwenda kwani nilivyokuwa ninaongea naye nilikuwa kitandani na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mawasiliano naye hadi sasa nimelala tu kitandani.”

 

Kuhusu kwenda hospitalini, Adelina alisema kuwa baada ya kuona maumivu hayo yanazidi alianza kwenda dispensari kisha Hospitali ya Amana-Ilala. Alisema huko hospitalini alichukuliwa vipimo vikubwa, lakini majibu ya vipimo vyake yalikuwa tofauti.

“Kuna waliosema nina tatizo, wengine waliona ugonjwa wa TB ya mifupa, wengine waliona tatizo la nyonga kujaa maji na wengine walisema mfuniko wangu wa nyonga wa mguu wa kulia ulikuwa wazi,” alisema Adelina kwa masikitiko na kuendelea: “Baada ya kuelezwa hivyo nilipata wakati mgumu mno ambapo niliambiwa natakiwa niende Hospitali ya Muhimbili kwenye Taasisi ya Mifupa ya Moi.

 

“Nilipofika Moi nililazwa kwa mwezi mmoja ndipo nikafanyiwa operesheni ya mguu wa kushoto na siyo wa kulia ambao awali niliambiwa ndiyo wenye tatizo.” Alisema alipomaliza aliruhusiwa kurudi nyumbani, lakini bado maumivu yalikuwa palepale huku mguu wa kulia ukianza kuwa mfupi.

 

Kwa upande wake, mama mzazi wa Adelina, Yasinta Ignasi alieleza namna anavyoshindwa kuelewa mwanaye anasumbuliwa na nini maana siku zinavyozidi kwenda ndivyo anavyolalamikia maumivu zaidi. Kufuatia hali hiyo, mama huyo alisema wameshahangaika sehemu mbalimbali, lakini hali bado ni tete hivyo kufikia hatua ya kukata tamaa na kumwachia Mungu atende muujiza.

 

Alisema anaomba msada kwa wasamaria wema waweze kumsaidia mwanaye kupata matibabu ya kina yanayoweza kumsaidia ili arudi katika hali yake ya zamani ya kujishughulisha kwa kuwa bado ni mdogo na ndiye tegemeo kwenye familia.

 

Adelina ni mtoto wa nne kati ya watoto watano wa familia ya Robert Peter na Yasinta Ignasi ambapo katika hali ya sintofahamu, watoto wao wengine walipata matatizo ya afya ya akili isipokuwa Adelina ambaye naye ana tatizo hilo. Kwa anayeguswa kumsaidia Adelina awasiliane naye kwa namba 0689 24 69 37 kwani kusaidia ni ibada pia!

Na Zaina Malogo na Richard Bukos

Comments are closed.