The House of Favourite Newspapers

Kisa Kipigo, Sven Awatupia Lawama Mastaa Simba SC

0

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck, amesema timu yake ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wa kucheza dhidi ya timu yoyote lakini anashangaa kuona wakishindwa kupata matokeo mazuri katika michezo ya Ligi Kuu Bara.

 

Kauli hiyo ya kocha huyo, ilitoka mara baada ya kuchezea kipigo cha bao 1-0 Ijumaa iliyopita kwenye mchezo wa ligi walipocheza na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Kocha huyo mara kadhaa alisikika akiitupia lawama safu yake ya ulinzi inayochezwa na Muivory Coast, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Kennedy Juma na Tairone Do Santos ambayo imekuwa ikiruhusu mabao mengi.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Sven alisema katika kila mchezo wachezaji wake wamekuwa wakifanya makosa yanayojirudia licha ya kuwapa maelekezo mazoezini, kitu ambacho ameona siyo sawa, kuona matatizo hayo yakijirudia.

 

Sven alisema mabeki wake wamekuwa wakifanya makosa ya kizembe ya kuruhusu bao kwa kila mchezo watakaocheza hali inayomfanya ajisikie vibaya, hivyo amepanga kuendelea kuisuka safu hiyo ya ulinzi ili icheze vizuri.

 

Aliongeza kuwa safu yake ya ushambuliaji nayo tatizo imekuwa ikishindwa kutumia vema nafasi nyingi ambazo imezipata, ikiwemo katika mchezo na JKT Tanzania ambao walipoteza kwa kufungwa bao 1-0.

 

“Ipo wazi Simba ina wachezaji wengi wazuri ambao wanaweza kucheza mechi yoyote na kupata matokeo mazuri, lakini kwenye mechi ya juzi Ijumaa tulishindwa kutumia nafasi tulizokuwa tumezipata na hiyo imetokana na umakini mdogo wa washambuliaji wangu.

 

“Pia makosa ya kizembe yanakuwa yakifanywa na safu yangu ya ulinzi yameonekana kuwa sugu, mfano mchezo tuliopoteza na JKT Tanzania ni makosa ya mabeki wangu kabla ya wapinzani wetu kuyatumia vema na kutufunga.

 

“Hivyo, nimepanga kuzifanyia maboresho safu zangu zote zenye upungufu kwa kuanzia ulinzi na ushambuliaji ili kuhakikisha timu yangu inapata matokeo mazuri ya ushindi,” alisema Sven.

 

Leave A Reply