The House of Favourite Newspapers

KISA ‘KUCHEZA’ NA BINTIYE, BABA AMPA KIPIGO MTOTO WA JIRANI

CHEZA na pesa usicheze na mwanangu! Hakimu Mwampondela (40) mkazi wa Mwakibete, Iyunga mkoani hapa amethibitisha usemi huo kwa kumpa kichapo mtoto wa jirani yake, Emanuel Mwamhoji (14) kisa kikidaiwa ni kucheza na bintiye (jina linahifadhiwa). Risasi Jumamosi lina mkasa mzima.

 

Kwa mujibu wa chanzo, tukio hilo lilitokea usiku wa Januari 30, mwaka huu maeneo ya Itongo ambapo mara kwa mara Hakimu alikuwa akimtuhumu Emanuel kutembea na bintiye. “Siku hiyo ya tukio, Hakimu alitokea na fimbo kisha kumpiga Emanuel kichwani, usoni na kifuani akimtuhumu kutembea na bintiye.

 

“Baada ya kipigo hicho kilichomjeruhi vibaya mtoto huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kupatiwa matibabu,” kilisema chanzo.Hata hivyo kitendo hicho cha kumpiga mtoto kipigo cha mbwa mwizi kiliwakera baadhi  ya majirani akiwemo mama mzazi wa Emanuel ambapo ililazimika taarifa za shambulio hilo kufikishwa polisi na mtuhumiwa kutiwa mbaroni.

 

Akizungumza na Risasi Jumamosi, mama wa mtoto aliyejeruhiwa, Latifa Mwamhoji (picha ndogo uk. 16) alisema kwa kipindi kirefu mzee huyo amekuwa akimlalamikia Emanuel kuwa anamharibu bintiye lakini bila kuweka ushahidi. “Huyu ni jirani yangu, nimekuwa nikimuambia awe makini na mambo ya watoto kwani bila ushahidi ni vigumu kuamini.

 

“Siku ya tukio mimi sikuwepo lakini naambiwa alimwita mwanangu nyumbani kwake na kumfungia ndani kisha kuanza kumpiga. “Baadhi ya majirani waliposikia kelele za mwanangu akiomba msaada walikwenda nyumbani kwa Hakimu lakini nao alianza kuwatukana na wengine kuwapiga.

“Hapo ikabidi polisi waitwe, walipofika ndiyo wakasaidia kumuokoa mwanangu, sijui wangechelewa nini kingetokea maana alikuwa amempiga mpaka ameishiwa nguvu,” alisema Latifa.

 

Kuhusu hali ya mwanaye mama huyo alisema kuwa ni mbaya kwa sababu madaktari wamemfahamisha kuwa amepata tatizo kubwa kwenye taya na maeneo ya kifuani.  Hivi ninavyoongea na wewe mwanangu hawezi kula kwa sababu mbali na tatizo kwenye taya lakini kavunjika pia meno matatu, nadhani alikuwa amepanga kumuua mwanangu na siyo kumuonya kama alivyokuwa anadai kuwa anamharibia bintiye,” alisema Latifa.

 

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanamshikilia Hakimu ambaye ni mtuhumiwa kwa ajili ya uchunguzi kwa RB namba MB/ IR/590/2019- KUJERUHI. “Tunam-shikilia kwa upelelezi, maana anasema alifanya tukio hilo kwa sababu Emanuel alikuwa akijihusisha kimapenzi na binti yake, tukimaliza kuchunguza na kubaini ipo jinai tutalipeleka shauri hili mahakamani,” alisema Matei.

 

Gazeti hili linawaomba wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa sababu kufanya hivyo ni kosa kisheria, badala yake utaratibu wa kufikishana kwenye vyombo vya sheria ufuatwe ili kila upande upate haki stahili

STORI: Ezekiel Kamanga, Mbeya

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.