The House of Favourite Newspapers

Kisa Maguri, Aveva avamiwa Dar

1

aveva.jpg Rais wa timu ya Simba, Evans Aveva.

Wilbert Molandi,
Dar es Salaam
MASHABIKI wa Simba wikiendi iliyopita walishindwa kuzizuia hasira na kuvamia Jukwaa Kuu la Uwanja wa Taifa na kuwatupia lawama viongozi wa timu hiyo mara baada ya mshambuliaji wa Taifa Stars, Elias Maguri kuifungia Stars bao la kwanza.

Elius-Maguli1.jpgMshambuliaji wa Taifa Stars, Elias Maguri.

Maguri alifunga bao hilo wakati Stars ilipopambana na Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia akiunganisha krosi safi ya Haji Mwinyi na kufunga kwa kichwa.
Hiyo siyo mara ya kwanza kwa mashabiki hao kulalamikia maamuzi ya uongozi wa timu hiyo kupendekeza kumuacha Maguri kwenye usajili wa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Kundi hilo la mashabiki, lilivamia jukwaa na kuanza kuwashambulia kwa maneno Rais wa timu hiyo, Evans Aveva na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Said Tulliy waliokuwepo uwanjani hapo wakifuatilia mechi hiyo.
Mashabiki hao walisikika wakihoji sababu za mshambuliaji huyo kuachwa akiwa bado ana kiwango kikubwa cha kuichezea timu hiyo.
“Tumechoka na aina hii ya viongozi wetu wa Simba, tunashindwa kujua sababu ya kumuacha Maguri wakati akiwa ana uwezo mkubwa wa kuichezea timu yetu.
“Hiyo siyo mara ya kwanza kufanya maamuzi hayo yanayoigharimu timu yetu ya Simba, walianza kwa kumuacha Tambwe, leo hii tunamkumbuka kwa uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao akiwa kwa watani wetu wa jadi wa Yanga.
“Hiyo ni kwenye usajili wa msimu uliopita wa ligi kuu, ikaja kujitokeza tena kwa Maguri ambaye wamemuacha kwa chuki zao zisizokuwa na msingi, leo hii angalia ni nuru Stars na klabu yake ya Stand United, anaongoza kwenye ufungaji bora akifunga mabao 9.
“Mbaya zaidi mnamuacha Maguri, halafu mnamsajili N’daw (Pape) ,” alihoji mmoja wa mashabiki hao waliovamia jukwaa hilo.
Katika hatua nyingine, mashabiki wanaodaiwa ni wa Yanga, walimvamia Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, wakimuomba wamuongeze Maguri kwenye usajili wa dirisha dogo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao.
Wakati mashabiki hao wakifikisha ujumbe huo kwa kocha huyo kwa kutumia Lugha ya Kiswahili na Kiingereza, mwenyewe alionekana akitabasamu na kuwaonyeshea ishara ya dole kama kukubali.
Kocha huyo, hivi karibuni alitamka kuwa anaendelea kumfuatilia Maguri uwezo wake wa kufunga mabao katika mechi za ligi kuu, licha ya kuutambua uwezo wake.
Maguri mwenye mabao tisa, anachuana na washambuliaji wa kimataifa Mzimbabwe, Donald Ngoma (Yanga) na Hamis Kiiza (Simba) kwenye ufungaji bora wakiwa na mabao nane kila mmoja.

1 Comment
  1. ahady kidehele says

    ukuje jangqanii eliasi magolii simba mizengwe mingi njaa nyingui huko

Leave A Reply