The House of Favourite Newspapers

MAUAJI YA KASHOGGI, RAIA WA TUNISIA WAANDAMANA NA MISUMENO

RAIA na wanaharakati nchini Tunisia wameingia barabarani kuandamana wakipinga ziara ya Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman ambaye ndiye hasa aiyeshika hatamu za uongozi wa Saudia kutokana na baba yake na Mfalme Salman kuwa mgonjwa.

 

Wanahabari na wanaharakati mjini Tunis wanasema wanapinga ziara hiyo kutokana na rekodi mbovu ya Saudia juu ya uhuru wa habari na kuheshimu haki za binaadamu.

Mandamano yalianza Jumatatu jioni na kuendelea juzi Jumanne (Novemba 27) wakipinga ziara ya bin Salman ambaye yupo kikaangoni kwa tuhuma za mauaji ya mwanahabari wa Saudia Jamal Khashoggi ambaye alikuwa ni kinara wa kupinga sera zake.

 

Khashoggi aliyekuwa akiishi uhamishoni Marekani baada ya kukimbia nchi yake mwaka 2017 aliuawa Oktoba 2, mwaka huu katika Ubalozi wa Saudia jijini Istanbul nchini Uturuki.

Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi wa Shirika la Kijasusi la Marekani la CIA, iliyochapishwa na vyombo vya habari, uwezekano wa mauaji hayo kufanyika bila amri ya bin Salman ni mdogo sana.

 

Hata hivyo Saudia imekanusha uhusika wa bin Salman na kulaumu maafisa wake usalama kwa kutekeleza operesheni haramu ambayo haikupangwa na dola.

Rais wa Marekani, Donald Trump pia amemkingia kifua bin Salman na kusema hawezi kuhatarisha mahusiano na Saudia na kuathiri uchumi wa dunia kutokana na mauaji hayo.

 

Tunisia inajulikana kwa kuwa na raia na wanaharakati ambao hawaogopi kuingia mitaani na kupaza sauti zao kwa masuala ambayo wanaona si sahihi.

Mwaka 2011 maandamano ya raia kupinga umasikini na ukosefu wa ajira yalimng’oa madarakani aliyekuwa rais wao Zine al-Abidine Ben Ali, ambaye aldumu madarakani kwa miaka 23.

 

Maandamano hayo yalichagiza harakati za mapinduzi katika nchi nyengine za Arabuni kama Misri ambapo rais Hosni Mubarak aling’atuka, Libya ambapo Kanali Muammar Ghaddafi alipinduliwa na kuuawa, Yemeni ambapo rais Ali Abdullah Saleh alipinduliwa.

Vugu vugu hilo pia liliingia Bahrain lakini familia ya kifalme imesalia madarakani kwa msaada wa majeshi ya Saudia. Harakati za mapinduzi nchini Syria zilizaa vita ya wenyewe kwa wenyewe na mpaka sasa rais Bashar Al-Assad yungali madarakani kwa msaada wa Urusi.

 

Na juma lililopita, Tunisia pia yalipita maandamano makubwa zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka mitano baada ya wafanyakazi 650,000 wa sekta ya umma kuingia barabarani kupinga mishahara midogo wanayodai kulipwa.

Comments are closed.