Kisa Nyumba Bibi Miaka 85, Wajukuu Pachimbika

BIBI mmoja aliyefahamika kwa jina la Fatuma Kirobo (85) amejikuta katika wakati mgumu baada ya wajukuu zake Maua Mwalami (28), Shakira (25) na Khairuni Mwalami (23) na mwingine wa kiume ambaye jina lake halikuweza kupatikana, kumjia juu na kudai kuwa amewatapeli nyumba ya baba yao mzazi, Mwalami Ally aliyefariki mwaka 2003.

 

Gazeti la Uwazi lilifanikiwa kufika mpaka nyumbani kwa bibi huyo, maeneo ya Tandika jijini Dar na kuonana na vijana hao ambao walifika wakiwa wameongozana na mama zao, shangazi na mwenyekiti wa zamani wa eneo hilo kwa lengo la kumtoa bibi huyo katika nyumba hiyo ili wajukuu zake hao waingie.

 

Wakizungumza na Uwazi, vijana hao walisema ni lazima bibi huyo atoke kwenye hiyo nyumba. “Lazima huyu bibi atoke kwenye hii nyumba ya wajukuu zake, tumechoka na ngonjera zake zisizoisha, tena safari hii hatuogopi kituk, ” alisikika akisema mama mmoja wa vijana hao akiwa na vijana hao.

HUYU HAPA MKE WA MAREHEMU

Uwazi liliongea na mke wa marehemu, Zainabu Hamis ambaye alifunguka kuwa nyumba hiyo ni ya mume wake ambapo Mahakama ya Kizuiani ilipitisha uamuzi wa kumtaka bibi huyo kuishi katika nyumba hiyo mpaka pale wajukuu zakee watakapokua kisha awakabidhi lakini ameshindwa kufanya hivyo.

 

“Hii nyumba alijenga mume wangu wakati nipo naye na alifariki dunia ghafla mwaka 2003, nakumbuka baada ya msiba kiliitishwa kikao cha familia tukaambiwa tutaitwa siku ya 40 kwa ajili ya mirathi, kwa sababu marehemu alikuwa na wake watatu na watoto wanne.

 

“Lakini cha kushangaza ni kwamba 40 ilipofika hatukuitwa hivyo ikabidi niende kwa mwenyekiti wa mtaa, akaitwa mama mkwe wangu pamoja na shemeji yangu mkubwa tukakubaliana kwamba wakagawe vyumba kwenye ile nyumba ili na sisi tuweze kuishi, lakini baada ya wiki moja kupita yule shemeji yangu akanitumia ujumbe kwamba tukapambane mahakamani, sasa tangu kipindi kile mpaka sasa bado tunahangaika tu hatujui nini hatima yetu,” alisema mama huyo.

 

MJUKUU AONGEA

“Sisi tumekua tumeikuta hii nyumba na tulipofuatilia tukaambiwa kwamba ni nyumba ya marehemu baba yetu kwa sababu alifariki dunia wakati sisi tukiwa wadogo. Sasa bibi hataki kabisa kutupa mali yetu ambayo ni halali yetu, anatufukuza hataki kukaa na sisi, tunaomba serikali iliingilie hili ili haki itendeke, kwa sababu tunampenda sana bibi yetu na hatutaki tufikie mwisho mbaya,” alisema Shakira.

 

BIBI ANENA

Naye bibi Fatuma alipohojiwa na Uwazi alisema kuwa wajukuu zake hao wamekuwa wakimwandama siku nyingi bila kujali umri alionao na wamekuwa wakimhangaisha kila siku mahakamani ambapo anawashinda.

Alisema hata baada ya yeye kushinda kesi bado hawataki kukubaliana na ukweli uliopo kwamba nyumba hiyo ni ya kwake na sio ya baba yao kwa hiyo ‘kama mbwai na iwe mbwai’.

 

“Hawa watoto sijui wanataka nini toka kwangu, yaani hawanionei huruma hata kidogo mimi bibi yao, kutwa wananishindisha mahakamani wakitaka urithi.

Aliongeza: “ Yaani hapa nilipo mapigo ya moyo yananienda mbio sina amani na maisha yangu, naona wanataka nife ndio watafurahi, hii nyumba ni yangu sio ya baba yao, kwa sababu nakumbuka mwaka 1988 nilimpa mwanangu shilingi 40,000 ili anunue kiwanja ajenge nyumba kwa sababu kipindi kile viwanja vilikuwa bei rahisi.

 

“Basi mwanangu akachukua zile pesa akaongeza na zake akanunua kiwanja kwa jina langu kisha akajenga hii nyumba ambayo wanasema ni yao, baada ya kumaliza kujenga aliitisha kikao cha familia na akasema kwamba nilipewa pesa ya kununua kiwanja na mama na nimeshamaliza kujenga hii nyumba.

“Nashangaa wanaposema hii nyumba ni ya baba yao wakati pesa ya kiwanja hata kujenga nilimpa mimi na nyaraka zote zinaonyesha jina langu (anatoa hati za nyumba kuthibitisha).”

MJUMBE AZUNGUMZA

Mjumbe wa eneo hilo, Idd Njechele naye alikiri kulifahamu tatizo hilo la muda mrefu na kusema kwamba hata yeye anashangaa kuona malumbano yakiendelea kwa sababu hati zote zina jina la huyo bibi lakini bado watoto wanadai nyumba ni yao.

“Hili tatizo nimeanza kulisikia muda mrefu sana sasa nashindwa kuelewa kwa nini malumbano yanaendelea? Ninavyokumbuka ni kwamba huyu bibi ameshashinda kesi mahakamani na hati zote zina jina lake,” alisema mjumbe huyo.

Hata hivyo Uwazi linashauri bibi na wajukuu zake hao kukaa na kuona namna wanavyoweza kulimaliza tatizo hilo kuliko kuendeleza malumbano ambayo hayawezi kuwapa faida.


Loading...

Toa comment