Kisa Penzi la Miss Tanzania… Mbasha Aitikisa Ndoa ya Masanja
Kisa kikidaiwa kuwa ni penzi la Miss Tanzania 2008, Jacqueline Chuwa ‘Jack’, muimbaji wa nyimbo za Injili, Emmanuel Mbasha ameitikisa ndoa ya Mchekeshaji Emmanuel Masanja ‘Mkandamizaji’ baada ya kuchukua picha ya Masanja aliyopiga na miss huyo kisha kuipamba na maneno ya kichochezi.
Picha hiyo Mbasha aliitupia kwenye Mtandao wa Instagram kitendo kilichosababisha hali ya hewa kuchafuka kwa saa kadhaa kwani wapo waliomshambulia Masanja lakini wengine walimshambulia yeye mwenyewe.
UJUMBE WENYEWE
Mbasha aliipamba picha hiyo ya Masanja na Jacqueline kwa kusindikiza na ujumbe uliosomeka hivi:
“Kweli ndoa ni pingu aisee… uvumilivu umemshinda mshikaji wangu kaona cha kufia…isiwe shida. Kamposti X wake. Imekaa poa au? Kama namuona Monika (mke wa Masanja) anavyoiangalia hii picha.”
MBASHA AITWA MCHOCHEZI
Vyanzo mbalimbali kwenye mtandao huo, vilieleza kuwa Mbasha alifanya hivyo kwa kuwa ana kinyongo na Jacqueline ambaye aliwahi kutembea naye kisha kumwagana mwaka jana.
“Mbasha mchochezi, kaamua kuweka hivi kwa sababu ya wivu si unajua naye aliwahi kutembea na Jack kisha wakamwagana, sasa kaona bora amharibie mwenzake kwa mkewe Monika,” alichangia mdau na mwingine akaongeza:
“Yaani hapa Mbasha anaichokonoa ndoa ya mwenzake unafikiri kweli kibinadamu Monika atajisikiaje akiona maneno haya? Asipokuwa makini kinaweza kikanuka.”
WENYEWE WAMEIPOKEAJE?
Amani liliwasaka wahusika waliotajwa kwenye ujumbe huo na kuongea nao kwa kina ambapo alianza kusakwa Miss Tanzania ambaye alisema ameshtushwa sana na imemkera kwani hakuelewa ni kwa nini Mbasha alifanya jambo hilo wakati anajua yule Masanja ni mchungaji na ana mkewe.
“Kwanza ieleweke kwamba siwezi kufurahia kabisa na imenistua hiyo ni kunichonganisha na mke wa Masanja ambaye kwa sasa najua ni mchungaji, mimi na yeye ni marafiki tu ni family friend hayo aliyoandika Mbasha sijui ameyatoa wapi na kwa nini amefanya vile wakati wao (Mbasha na Masanja) ni marafiki,” alisema Miss Tanzania huyo.
AELEZA KINACHOMSUMBUA MBASHA
Aidha, alisema kuwa anachojua yeye Mbasha atakuwa anaendeshwa na wivu na hajui ni kwa nini bado anamfuatafuata wakati walishaachana.
“Sijajua kwa nini ananifuata wakati tulishaachana, kama ana wivu asiharibu ndoa ya watu, mimi na Masanja tunaheshimiana kama nilivyokwisha kuambia,” alisema Jacqueline.
MASANJA ATOA YA MOYONI
Amani halikuishia hapo lilimsaka Masanja ili kuweka usawa ambapo alipopatikana naye alitoa yake ya moyoni.
Kwanza alisema, yeye ndiye aliyeiposti hiyo picha na kudai hata kama Jacqueline alikuwa mtu wa Mbasha zamani, haoni tatizo kwani yeye ni mchungaji ambaye anapiga picha na watu mbalimbali na kuziposti mtandaoni.
“Nimemshangaa Mbasha ila mimi sioni tatizo. Mimi ni mchungaji, napiga picha na mtu yeyote sasa niliona tu Mbasha ameichukua na kuweka maneno yake…mimi sina tatizo, nina familia yangu sasa hivi siwezi kutetereka na picha, napiga na mtu yeyote, namshukuru Mungu haijaniharibia chochote,” alisema Masanja.
MKE WA MASANJA SASA
Naye mke wa Masanja, Monica alipotafutwa kwa njia ya simu, aliomba apigiwe baadaye kwani alikuwa bize.
MBASHA AUFUTA UJUMBE
Mara baada ya Amani kunasa picha hiyo katika Mtandao wa Instagram na kumsomea mashtaka ya kuonekana kuitikisa ndoa ya Masanja, Mbasha aliufuta ujumbe huo haraka kisha akaomba atafutwe baadaye.
Hata hivyo, Amani lilimvutia waya baadaye hakupokea. Siku iliyofuata (juzi Jumanne), Mbasha alipokea na kusema yeye aliiweka picha hiyo na ujumbe huo kama utani lakini alishangaa kuona mapokeo mabaya.
“Niliweka kama utani. Yule ni X wake sasa Wabongo ndiyo wamejiongeza kwa mambo mengi hadi nikaona isiwe tabu ngoja niifute,” alisema Mbasha.
Alipoulizwa kama alifanya hivyo kwa sababu ya wivu kwa Jacqueline ambaye aliwahi kuwa mpenzi wake, Mbasha alikataa kwa kusema si kweli.
“Wewe umeshaona mimi nimekiri hata siku moja kwamba huyo Jacqueline ni mpenzi wangu? Yeye anakiri sawa lakini mimi sijakiri hivyo siwezi kuwa nimefanya hivyo kwa sababu ya wivu wala nini sababu sina mpango naye na haiwezi kutokea nikawa na wivu naye,” alisema Mbasha.
Stori: Waandishi Wetu, Amani |DAR ES SALAAM
Comments are closed.