Kisa Rivers… Nabi Awaonya Mayele, Musonda Dhidi ya Rivers United Uwanja wa Mkapa
KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ametoa onyo kwa wachezaji wake wakiwemo washambuliaji, Kennedy Musonda na Fiston Mayele kwa kuwaambia kuwa bado hajawafuzu nusu fainali licha ya kufanikiwa kupata ushindi katika mchezo wa kwanza wa robo fainali dhidi ya Rivers United, hivyo wanatakiwa kutumia nafasi za kufunga kwenye mchezo kesho Jumapili ili kuweza kufuzu nusu fainali.
Yanga imejiwekea mazingira mazuri ya kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Rivers, katika mchezo wa kwanza uliopigwa wikiendi iliyopita huku mchezo wa marudiano ukitarajia kupigwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Nabi alisema: “Hatuna presha kwa sababu tumefanikiwa kupata matokeo katika mchezo wa kwanza, ingawa bado tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunaendelea kupata matokeo katika mchezo ambao tutacheza nyumbani kwa sababu wapinzani wana timu yenye wachezaji wazuri ambao wanaweza kufanya mambo kuwa tofauti.
“Lakini sitaki kuona tunawadharau kwa kuwa tumefanikiwa kupata matokeo ya awali, hatua ambayo tupo kwa sasa inahitaji kuweka nguvu na kila mmoja kutoa mchango wake ili kuweza kupata matokeo kwa kutumia kila nafasi ambayo itakayoweza kupatikana kwa sababu watahitaji kupata matokeo mazuri kwetu hivyo lazima tuwe bora zaidi yao,” alisema Nabi.
Stori: Ibrahim Mussa