Mayanja afanya kikao na mastaa wake
Bosi mkuu wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja.
Said Ally, Dar es Salaam
BOSI mkuu wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja, amelikabidhi jina la straika wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, mikononi mwa wachezaji wa kikosi hicho kwa kuhakikisha straika huyo hafanikiwi kutwaa kiatu cha mfungaji bora kwa msimu huu na badala yake wawekeze nguvu kubwa katika kumsaidia mshambuliaji wao, Hamis Kiiza.
Kiiza na Tambwe kwa sasa wapo katika vita kubwa ya kugombania ufungaji bora kwa msimu huu baada ya kumvua Simon Msuva aliyetwaa msimu uliopita, ambapo mpaka sasa Kiiza anaongoza akiwa na mabao 18 akifuatiwa na Tambwe mwenye mabao 17.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mayanja alisema amezungumza na wachezaji wake na kuwapa jina hilo la Tambwe ili kuwakumbusha juu ya namna ya kumsaidia Kiiza kuwa mfungaji bora.
“Sisi tunatakiwa kuwa nyuma ya Kiiza kwa kuhakikisha tunamsaidia kwa nguvu zetu zote kumfanya awe mfungaji bora katika msimu huu.
“Nimewaambia wachezaji wangu ni lazima wajitahidi kumtengenezea nafasi nyingi Kiiza ili aweze kuwa mfungaji bora, naamini kama tukifanikiwa kufanya hivyo, basi tutakuwa tumemsaidia kwa kiasi kikubwa katika mchakato huo wa kutwaa ufungaji bora.
“Ingawa natambua kuwa haitakuwa kazi nyepesi kwani naye Tambwe amekuwa akiungwa mkono na timu yake lakini wazo letu hilo litaweza kufanikiwa kwa asilimia kubwa kama wachezaji wote wakiweza kujitoa kushiriki katika mpango huo,” alisema Mayanja.